TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, July 16, 2011

Maalim Seif aibana CCM kuhusu Rostam • Ataka CCM ieleze ukweli, iache unafiki

MAKAMU wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Sif Sharif Hamad

MAKAMU wa kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Sif Sharif Hamad, ameibuka na kusema Chama cha Mapinduzi (CCM), kinatakiwa kuwaeleza wananchi kama kujiuzulu kwa Mbunge wa Igunga na Mjumbe wa NEC, Rostam Aziz, ni mwanzo wa kujisafisha ama la.

Kauli ya Maalim Seif imetokana na hotuba ya Rostam kwa wazee wa chama hicho wilaya ya Igunga iliyofafanua sababu za kujiuzulu kwake ikisisitiza kwamba hatua hiyo haitokani na uamuzi wa kikao cha NEC cha kuwataka watuhumiwa wa ufisadi kujivua gamba.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kusema nyuma ya hatua hiyo zipo sababu ambazo CCM inazificha huku akiwataka viongozi wake kutekeleza kwa haki azimio la kujivua gamba lililotolewa na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Jakaya Kikwete.

“Mimi sio mwana CCM ni mtazamaji kama ninyi, lakini kwa kuwa aliyejiuzulu alisema hakujiuzulu kwa sababu ya shinikizo kutoka ndani ya chama chake…basi CCM yenyewe inao wajibu wa kuwaeleza wananchi juu ya kilichotokea kwa Rostam,” alisema Maalim Seif.

Alisema CCM inatakiwa ielezee uhalisia wa Rostam kuachia nafasi zake ili kuwaondolea wanachama wake hali ya kubabaika.

Wakati Maalim Seif akisema hayo, zipo taarifa kutoka chanzo chetu cha kuaminika kwamba Rostam amekabidhi barua ya kujiuzulu kwake kwa mwenyekiti wa chama hicho, Kikwete, na kwamba hivi sasa yuko kijijini kwake wilayani Igunga, Tabora.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Willson Mukama aliyezungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema hajapata barua inayohusu kujiuzulu kwa mbunge huyo na kuongeza kwamba hana taarifa zozote.

“Sina taarifa yoyote rasmi wala barua ya kujiuzulu kwa Rostam…nadhani bado yuko jimboni kwake Igunga mkoani Tabora,” alisema Mukama.

Rostam alitangaza kujiuzulu juzi na katika hotuba yake alisema ameamua kuachana na siasa uchwara zinazoendelea ndani ya CCM ili aendeleze biashara zake vizuri.

Rostam pia aliwatuhumu Nape Nnauye (Katibu Mwenezi Taifa wa CCM) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, kwa kupindisha ukweli wa dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ yenye lengo la kukisafisha chama hicho kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wao.

Alisema, wawili hao wamekwenda mbali kwa kulitaja jina lake kwa kulihusisha na ufisadi, wakati ukweli wa kimazingira na ushahidi wa wazi umeshathibitisha kuwa ni porojo za kisiasa zinazotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule wa 2015.

Miongoni mwa waliozungumzia kwa masikitiko uamuzi huo wa Rostam ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Watanzania wengine.

Rostam ni mfanyabiashara maarufu nchini, alikuwa Mbunge wa Igunga kwa miaka 18 baada ya kumrithi marehemu Charles Kabeho katika uchaguzi mdogo wa mwaka 1994.

No comments: