TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, July 16, 2011

HUKUMU YA USALITIU WA SHIBUDA KWA CHADEMA LEO
WAKATI Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikikutana leo jijini Dar es Salaam kumjadili Mbunge Maswa Magharibi, John Shibuda, mbunge huyo amesema hana taarifa za kikao hicho.

Kikao hicho kitakachofanyika kinatarajiwa kumjadili mbunge huyo ambaye alihamia Chadema akitoka CCM siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Kwa mujibu wa habari, kikao hicho tafanyika kwenye ukumbi wa Mbezi Garden. Shibuda aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa hajapatiwa barua yoyote na chama hicho inayomtaka ajieleze kwanini aliisaliti kambi ya upinzani Bungeni kuhusu posho wakati akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Lakini, kumekuwapo habari kuwa Chadema inafikiria kumchukulia hatua za kinidhamu. Tuhuma zinazomkabili Shibuda ni kutoa matamshi yanayopinga na msimamo wa kambi yake inayoongozwa na Chadema pale alipowapiga vijembe wabunge wale wanaopinga posho zinazotolewa kwao na watumishi wengine wa umma nchini. Hata hivyo, Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema tangu Shibuda atoe kauli hizo Bungeni hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa. Alisema kuwa kikao cha kamati kuu kitakachoketi leo pamoja na mambo mengine kitamjadili mbunge huyo. ’’Kesho (leo) atajadiliwa, ila hatua gani zinatachuliwa hilo sijui, pia suala la nidhamu ndani ya chama litakuwa moja ya ajenda za kikao hicho,’’ alisema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai. Awali, Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu alilieleza gazeti hili kwamba kitendo cha Shibuda kupingana msimamo wa kambi ya upinzani ambao ni kukataa kulipwa posho za vikao, kimewadhalilisha na kwamba lazima mhusika (Shibuda) atoe maelezo kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake.

"Kutokana na tukio la kudhalilisha uamuzi ya vikao vya kambi, kuna aina mbili za kumchukulia hatua Shibuda, kwanza ni kwa upande wa kambi ya upinzani na pili kumshitaki Chadema,”alisema Lissu na kuongeza:

“Mbunge anapokiuka uamuzi ya kambi anastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kupewa adhabu, na adhabu kubwa anayoweza kupewa na kambi hii kwa kanuni zetu ni kumtenga katika kambi na kumtangaza hadharani kuwa huyu ametengwa na kambi kwa sababu amefanya makosa kadhaa".

Kwa mujibu wa Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Shibuda mbali na kosa hilo, pia amekuwa akitoa matamshi ya kudhalilisha kambi ya upinzani na Chadema, pamoja na kuwadhalilisha viongozi wao.
Akizungumzia matamshi ya kudhalilisha kambi ya upinzani na Chadema yanayotolewa na Shibuda, Mbowe aliliambia Mwananchi Jumapili, kwamba kila mtu ana haki ya kuzungumza anachokitaka, lakini kama ni masuala ya chama anatakiwa kufuata utaratibu. ‘’Kama anaona hajakosea huo ni mtizamo wake, unajua chama kina taratibu zake, chama sio kundi la watu ambalo halina kitu kimoja (katiba na kanuni) ambazo wamekubaliana kuzifuata kama njia ya kuwaongoza katika maamuzi yao,’’ alisema Mbowe. Alisema kiongozi si yule anayesimamia fikra zake binafsi, bali ni yule ambaye anaafikiana na chama chake kwa kila jambo kwa kufuata katiba, kanuni na sera za chama. ‘’Kama chama hakifuati katiba hakina umuhimu wa kuwapo, Chadema sio kundi la watu, ni chama ambacho kina malengo..., malengo hayo ndio yaliyotuunganisha pamoja,’’ alisema Mbowe. Alisema maamuzi ya Kamati Kuu yatatolewa kulingana na Katiba ya Chadema inavyoeleza. ‘’Unaweza kumuudhi Mbowe.., Lakini unapoanza kukishutumu chama pamoja na viongozi wake ni jambo jingine, katika hilo lazima itizamwe katiba ya chama inasemaje,’’ alisema Mbowe. Alisisitiza kuwa tangu kuibuke kwa mvutano hio, ni mara ya kwanza kwa Kamati Kuu kukutana na kuongeza kuwa ripoti mbalimbali pia zitajadiliwa katika kikao hicho ambacho kinaonekana kuwa kitatoa picha halisi ya maamuzi mwelekeo wa Shibuda ndani ya Chadema. Kauli ya Zitto

Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini juzi alilieleza gazeti hili kuwa msimamo wa kumfukuza Shibuda upo pale pale, kwani kambi hiyo wala Chadema hawawezi kumwacha mbunge anayekiuka sera na kuwadhalilisha viongozi hadharani.

"Shibuda hatafukuzwa kinyemela, lazima taratibu zifuatwe kwa Mnadhimu Mkuu wa kambi yetu kumwandikia barua ya kumweleza makosa yake na yeye kupata fursa yakujibu shutuma hizo, pili ataitwa katika Kamati Kuu ya chama chetu (Chadema), nao watatoa uamuzi wao,"alisema Zitto na kuongeza:

“ Chadema si chama cha kihuni kwamba tutakurupuka ni lazima haki itendeke na mimi sipendi mtu aonewe, Shibuda atapata haki zake zote kama mwanachama. Mbunge yeyote wa Chadema anapaswa kujua akienda kinyume na sera ya chama atafukuzwa”.

Alisema suala la posho lipo kwenye Ilani ya uchaguzi wa 2010 kwa hiyo ni sera, na kwamba anayepinga atafukuzwa tu na kwamba Chadema wataanza na Shibuda.

Zitto alisema, "Shibuda anajua mie humtetea sana, lakini anapokwenda kinyume na sera ya chama tutamfukuza, aniite majina yoyote tu akienda kinyume na sera nitakuwa wa kwanza kumfukuza."

"Kuna masuala ya nidhamu kwenye Bunge na wabunge wa chama fulani inaitwa’ three line whip, masuala ya msimamo wa kitendaji mfano tulipokaidi kwenda Bungeni kutoka nje ya ukumbi wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia bunge (walk out), haya ni ya kawaida na hayana adhabu kali, lakini likiwa la sera adhabu ni kufukuzwa, Shibuda asipaparike," alisema Zitto.


Msimamo wa Shibuda
Akizungumza na Blog hii kwa njia ya simu, Shibuda alisema kwa kifupi kuwa hajui lolote kuhusiana na kikao hicho huku akisisitiza kuwa yeye ni mwanasiasa adimu na kwamba akizungumza jambo anakuwa ameshalifanyia kazi. Alipoulizwa kama atakubaliana na maamuzi yatakayotolewa na Kamati Kuu, Shibuda alisema, “Siwezi kujua utamu wa mboga wakati sijui viungo vyake vitakavyonunuliwa,’’. Wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2011/2012, Shibuda alitoa mpya pale alipopingana na misimamo wa Chadema huku akilikokotoa neno ‘posho’ kuwa maana yake halisi ni ujira wa mwia.

Alisema mwia (sasa posho) ni malipo anayopewa mtu kwa kazi anayoifanya ili kumwongezea hamasa ya kuendelea kuifanya kazi hiyo. Kwa mujibu Shibuda, kama maana ya posho ni ‘ujira wa mwia’ kama ilivyokuwa ikitumika na wakoloni, haina sababu kuifuta kwa kuwa ndiyo hamasa kwa wabunge na watumishi wengine wa umma kuendelea kufanya kazi yao.

Shibuda alilitahadharisha Bunge kuwa mjadala wa posho umetokana nalo kuwa na aina mbili ya wabunge; wabunge maslahi jamii na wabunge maslahi binafsi.

No comments: