TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, July 18, 2011

Rostam aidatisha CCM,UAMUZI WAKE WA KUNG'ATUKA WAGONGANISHA MAKADA


Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Nape Nnauye

UAMUZI wa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kujivua nyadhifa zote ndani ya CCM, umeanza kukivuruga chama hicho, baada ya baadhi ya makada wake wakiwamo mawaziri kutupiana lawama hadharani huku wengine wakitaka uongozi wa chama kuwafukuza wenzao wanaoonekana kuwa mzigo.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayopingana kimtazamo kuhusu hatua ya mwanasiasa huyo kujiuzulu wiki iliyopita.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwapo kwa kundi linalopongeza uamuzi huo na kutaka watuhumiwa wengine waige mfano wake huku jingine likiwaponda wenzao wanaoshinikiza hatua hizo.

Hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa mpango mkakati wa chama hicho kujivua gamba unakifanya kiingie katika mtihani mgumu zaidi kisiasa.

Vita ya makundi kuelekea mbio za uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2015, nayo kwa kiasi kikubwa inachochea moto huo wa mpango wa kujivua gamba, kwani wapo wanaodhani kuwafukuza watuhumiwa wa ufisadi ni kete muhimu kimkakati kuelekea uchaguzi huo huku kundi linalotuhumiwa likiweka mbinu kuzuia utekelezaji wa mpango huo.

Genge la makada wa CCM linalojipambanua kuwa la wapambanaji dhidi ya ufisadi limekuwa likiuchukulia mpango huo wa kujivua gamba, kama kete muhimu kupunguza nguvu ya upande wa pili wa watuhumiwa wa ufisadi katika mbio hizo za urais mwaka 2015.

Vivyohivyo genge la watuhumiwa wa ufisadi ambalo limeonekana kumwandaa mgombea wao 2015, limekuwa likitumia ukwasi wake mkubwa kujiwekea mazingira mazuri ndani ya chama hicho huku wapambanaji wakitumia mtaji wa nguvu ya umma, katika kujipatia umaarufu.

Kufuatia upepo huo mbaya wa kisiasa unaovuma ndani ya CCM hasa baada ya kujiuzulu kwa Rostam, tayari baadhi ya makada wakongwe wa chama hicho waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wamesema chama hicho kwa sasa kinatakiwa kuongeza umakini katika utendaji wake kwa kuwa mambo yanayoendelea sasa, yanatishia hatima yake.

Kauli ya Guninita
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ambaye ni mmoja wa watu muhimu katika kundi linalozuia wapambanaji wa ufisadi kuchanua mbawa zao ndani ya chama, alisema ni unafiki kwa mwanachama wa CCM kujitokeza na kusema kwa sasa chama hicho ni shwari wakati anaona watu wanajiuzulu.
Guninita alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho, Kata ya Kimara katika mkutano uliojadili sababu za CCM kushindwa katika majimbo ya Ubungo na Kawe jijini Dar es Salaam, Majimbo hayo yote yamechukuliwa na Chadema.
“Unaona watu wanajiuzulu, halafu unasema shwari! Unamdanganya nani? …unaona mawaziri wanarushiana maneno halafu bado unasema shwari, unamdanganya nani?’’ Alihoji.

“Matatizo yapo…hali iliyopo sasa ndani ya chama haihitaji mtu uwe umehitimu shahada ya chuo kikuu kuhusu mambo ya migogoro ndio utambue kuwa kuna mgogoro ndani ya CCM,” alisema.

“Huu ni muda wa kutafakari na kuhakikisha kuwa mawimbi haya hayazamishi chama, unafiki umetawala ndio sababu tumefikia hapa,’’ aliongeza.
Guninita alisema makundi ni sababu za CCM kuanguka katika majimbo ya Ubungo na Kawe, hivyo chama kinapaswa kujitafakari kwa makini ili kuondoa tofauti zilizopo.

"Mmeingia kwenye uchaguzi mkiwa na makundi, na hata sasa yapo bado kuna unafiki, tumetanguliza maslahi ya viongozi mbele badala ya chama,” alisema na kuongeza:
‘’...Mchawi wa CCM ni chama chenyewe, wapinzani hawana shida kwa sababu kule hawana viongozi na wanaharakati tu.”

Nape: Mwache Guninita aseme
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM , Nape Nnauye, alipoulizwa jana kuhusu kauli ya Guninita kwamba hali ndani ya chama si shwari alisema, angependa kuona kauli hiyo kwanza kabla ya kujibu kitu chochote.

Balozi Lusinde atoa angalizo
Mmoja wa makada maarufu wa CCM tangu enzi za TANU na mmoja wa mawaziri wa kwanza wa Baraza chini ya Serikali ya Tanganyika huru, Balozi Mstaafu Job Lusinde, alisifu uamuzi wa Rostam kujiuzulu nyadhifa zake, akisema ni wa kishujaa. Lakini, akawataka makada wengine wanaonyoshewa vidole kwa tuhuma mbalimbali, waige mfano wake badala ya kusubiri kufukuzwa.

Balozi Lusinde ambaye ni mmoja wa watu wanaoheshimika nchini, alisema “Hakuna kidonda katika kufanya maamuzi ya kujing’atua kwa hiyari kwani hatua hiyo itamaliza haraka kelele za wananchi.’’

Lusinde alirudia kauli yake kuwa chama ni lazima kiondoe woga na kigugumizi kilichopo ili kuwafukuza mara moja watu ambao wanaamini ni mzigo, ndani ya chama hicho kuliko kuendelea kutumia majukwaa kutangaza mambo hayo wakati wanazo nafasi za kufanya hivyo kwenye vikao.

“Napenda kueleza jambo moja kuwa kama chama kina ushahidi na hao wanaowatuhumu, basi kiwafukuze mara moja kuliko kuendelea kupiga maneno yasiyo na utekelezaji ndani yake na kama hawana ushahidi basi waache kuwapigia kelele wenzao bali hao wanaopigiwa kelele watajipima wenyewe,’’ alifafanua.

Kuhusu mpasuko ndani ya chama endapo kitachukua maamuzi magumu, alisema, “ Mpasuko ni bora kuliko chama kufa kwa ajili ya kuwang’ang’ania watu wachache ambao ni ‘funza’, katika safari lazima wengine watoswe.”

Kwa maoni ya mwanadiplomasia huyo, ingefaa watu wote ndani ya CCM wanaotuhumiwa wasisubiri kutimuliwa hata kama hawana hatia, lakini kwa kuwa watu walishazungumza mambo mengi juu yao, basi lazima wakae pembeni kwanza ili chama kiweze kujijenga.

Akemea viongozi wa CCM
Hata hivyo, Balozi Lusinde aliwanyooshea vidole viongozi wa CCM kuzunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kuwaita wenzao kuwa ni mafisadi hata baada ya vikao kuamua misimamo mingine.

Alifafanua kwamba, kitendo cha viongozi ndani ya chama kuendelea kuwaanika wenzao katika majukwaa kuwa ni mafisadi kinaongeza na kuchochea chuki ndani ya chama hicho kikongwe na akakemea tabia hiyo kuwa inapaswa kuachwa mara moja.

“Hawa viongozi nao wana jambo ambalo silipendi kabisa, hivi walishaelezana kwenye vikao ya nini tena kuzungumza kwenye majukwaa kuhusu wenzao hao wanaowatuhumu, si afadhali kuwafukuza kuliko kuwasema kila siku hii ni kuongeza vidonda.’’

Mtazamo wa CCM kwa siku zijazo
Lusinde alisema chama kilivyo kwa sasa kinapaswa kupata viongozi waadilifu ambao wanaweza kukisogeza kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine na kwamba bila ya kupatikana viongozi wa aina hiyo chama kitazama
Alipingana na kauli kuwa ndani ya chama hicho kuna watu watatu ambao wanakivuruga na badala yake akasema wapo watu wengi kuanzia ngazi ya chini na akataka uwajibikaji na kujivua gamba uanzie chini.

Hata hivyo, alisema kuondoka kwa wanachama ndani ya chama hakuna maana chama kitakufa, bali kinajiimarisha zaidi kwa kuwa watu wengine wataanza kuogopa.Balozi Lusinde alitoa mfano wa kipindi cha awamu ya kwanza na kusema kulikuwa na uwajibishwaji ambapo watu kama akina Oscar Kambona na wengineo waliwajibishwa na kupoteza umaarufu wao.

Kauli ya John Chiligati
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Tanzania Bara), John Chiligati alipoulizwa juu ya shutuma alizotupiwa na Rostam, alisema amezisikia, lakini hana jambo la kusema.
“Nimesikia hiyo kauli (shutuma za Rostam), lakini kwa sasa sina cha kusema,” alisema Chiligati.
Lakini mwandishi alipotaka kujua kama shutuma hizo zinao ukweli wowote, alisisitiza “No comment” (sina cha kusema).
Chiligati alipotakiwa kuzungumzia hali ndani ya chama hicho ambayo kwa sasa inaokana ni tete, alieleza pia kuwa, hayuko tayari kuzungumzia suala hilo.
“Muulize msemaji wa chama (Nape Nnauye), ndiye ataweza kuzungumzia hilo,” alisema Chiligati.

Kombora la Sitta
Katika kuonyesha hali si shwari, kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta juzi mjini Mbeya ya kutaka watu waliosababisha taifa kufikia hatua ya tatizo la nishati wawajibishwe kisheria inazidi kuongeza joto hilo.

Wadadisi wa mambo ya kisiasa ndani ya CCM wanaonyesha kauli hiyo moja kwa moja inawalenga Rostam katika sakata la Richmond na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambao hata tuhuma zinazowataka wajivue gamba zinatokana na kampuni hiyo ya iliyoifulia Tanzania umeme wa dharura.Juzi, Sitta akiwa Mbeya alisema Serikali inapaswa kuwaomba radhi Watanzania kutokana na tatizo la mgawo wa umeme, lakini akitia ngumu akisema, isiishie kuomba radhi bali waliohusika kulifikisha taifa lililpo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kauli hiyo ya Sitta mmoja wa mawaziri wenye nguvu kubwa ya umma, alisema Tanzania siyo nchi inayopaswa kuwa na mgawo wa umeme, bali inapaswa kuzalisha na kuuza umeme nje, lakini imefikia mahali hapo kutokana na mikataba ya kifisadi.

Sitta, pia aliwahi kunukuliwa akisema Kampuni ya Richmond ilikuwa ni kampuni ya genge la watu watatu ambao waliamua kwa makusudi kulihujumu taifa.Tayari pia, wiki moja kabla ya kujiuzulu kwa Rostam, Sitta pia alimrushia kombora Lowassa katika dhana ya kutaka maamuzi akisema, hayawezi kufanyika katika mipango ya kupata asilimia 10 au kuingia mikataba ya kitoto.

No comments: