TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, June 14, 2011

Mbunge Azzan atishiwa kuwekewa madawa ya kulevya

Sakata la Mbunge wa Kinondoni Idd Mohammed Azzan, kushauri wajumbe wa sekretarieti ya mkoa wa Dar es Salaam ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutafakari jinsi ya kujivua gamba kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu wa 2010, limechukua sura mpya.

Mbunge huyo ambaye tayari amezuiwa kuwania nafasi yeyote ndani ya CCM kwa kipindi cha miezi 18, ameanza kuandamwa na kupokea vitisho, baada ya kuwasilisha rufaa yake kwenye Kamati Kuu (CC) ya CCM Taifa, kupinga adhabu hiyo.

Habari za uhakika zinasema kwamba katika rufaa hiyo, Mbunge huyo ‘amemwaga mboga’ kwa kueleza vituko vya aina mbalimbali vilivyofanywa na baadhi ya wadhamana wa CCM mkoa, pamoja na hila za kuengua watu walioshinda kura za maoni, lakini majina yao yakaenguliwa.

Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Kilumbe Ng’enda ambaye anatajwa kuwa kinara wa mkakati wa kummaliza Mbunge huyo kijana, amekanusha kuhusika kwa namna yeyote na suala hilo.

Pamoja na kukanusha hilo, Kilumbe anaelezwa kwamba alimsema hadharani Mbunge Azzan kuwa anahusika na biashara ya dawa za kulevya katika kikao cha UVCCM wilaya ya Kinondoni, na hivyo kuharibu hali ya hewa.

Mbali na kutaka kumwekea dawa za kulevya Mbunge Azzan pia amelalamikia hatua ya kupakaziwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa kada mmoja wa CCM aliyewahi kuwania Ubunge katika Jimbo la Temeke, ikielezwa kuwa na mkakati wa kumchafulia jina lake.

Inasemekana kuwa baadhi ya vigogo wanaopingana na Mbunge huyo wameungana na kuweka mkakati wa kutaka kumuwekea madawa ya kulevya kwenye gari yake, ili akamatwe na Jeshi la Polisi nchini.

Hata hivyo, habari zinasema kwamba tayari Mbunge huyo ametoa taarifa kwenye mamlaka za nchi kuhusiana na vitisho hivyo, huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Alhaj Suleiman Kova, akiahidi kulifuatilia kwa karibu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamishna Kova, alisema amepokea taarifa hizo za kutishiwa kwa Mbunge Azzan kwa masikitiko makubwa na hasa kutokana na nyadhifa za watu wanaotajwa kutaka kufanya jambo hilo.

“Unajua Polisi haina nafasi ya kuingilia mambo yanayotokea katika kumbi za siasa, kazi zetu ni kusimamia sheria na kulinda Usalama wa Raia na Mali zao,” alisema Kamishna Kova, huku akitoa onyo na kuahidi kuwaita watu wote waliotajwa kwa namna moja ama nyingine na suala la Wanasiasa wengine wanaotajwa katika sakata hilo ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (MNEC) wa Mkoa wa Dar es Salaam Ramadhan Madabida, Mwenyekiti wa UWT mkoa Zarina Madabida, Katibu Mwenezi Juma Simba na Abbas Tarimba.

Wanachama Tarimba ambaye ni Diwani wa Kata ya Hananasif Manispaa ya Kinondoni, Juma Simba, Ramadhan Madabida na mkewe Zarina (Mbunge wa Viti Maalum) hawakuweza kupatikana kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kufutia lawama zinazotupwa kwa upande wao.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mbunge Azzan alikiri kuwapo kwa njama hizo na kusema yeye amemuachia Mungu kufanya maamuzi ya mustakabali wake.

“Mimi nimeamua kumuachia Mungu suala hilo, maana siasa sasa zimegeuka na kuwa vita, hivyo ninaona hatari ya kusema ukweli ndani ya chama changu,” alisema Mbunge Azzan.

No comments: