TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, June 14, 2011

Lazima utamaduni wa posho upigwe vita


Kwa yeyote anayeijua Tanzania kwa maana ya hali ya maisha ya wananchi wake, ni jambo la hatari kikundi kidogo cha watu waliokalia ofisi za umma kujipangia utaratibu wa kujinufaisha kwa jasho la walipa kodi kwa kisingizio cha sheria ambayo waliitunga wenyewe kwa kujipendelea.

Ni aibu zaidi kusikia kwamba wabunge wengi na hata mawaziri wanakejeli juhudi za wabunge wachache za kutaka kujenga jamii inayoogopa kodi za wananchi na wakati wote kuzielekeza katika kuleta maendeleo ya taifa.

Tunasema maneno haya baada ya kukaa na kutafakari mwelekeo wa sasa wa hoja ya baadhi ya wabunge ya kutaka kuondolewa kwa posho za vikao na badala yake wabunge wafanye kazi kwa kuwa wanalipwa mishahara. Tunasema na kusisitiza kuwa ujira wa vikao ambavyo ni kazi halali za ubunge ni mshahara na si posho!

Hoja hii ambayo inaelekea kuungwa mkono na kambi ya upinzani tu, inajengwa kwenye ukweli kwamba mabilioni ya shilingi zikiwa ni kodi za wananchi kila mwaka wa fedha yanatengwa kwa ajili ya posho tu, mwaka wa fedha unaokuja yaani 2011/12 serikali imeomba Bunge lipitishe Sh. bilioni 987 kwa ajili ya posho mbalimbali za watumishi wa serikali wakiwamo wabunge. Hii ni hatari.

Kufichuliwa kwa kiwango hiki cha fedha wakati Waziri wa Fedha akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/12 akiwa ameahidi kwamba posho ambazo hazina tija zitaondolewa kauli iliyoonekana kama mwanzo wa mageuzi ya kweli, ni kielelezo cha kukosekana kwa tafsiri ya maneno kuwa vitendo halisi kwa kiongozi kama huyo.

Yaani wakati serikali inataka wananchi waisadiki kuwa imeamua kupunguza posho, au tuseme matumizi ya ovyo, ndani ya vitabu vya mgawo wa fedha serikali inafanya kinyume chake. Hali hii kila tukiitazama na kuitafakari tunashindwa kujua nini maana yake, anadanganywa nani na kwa faida ya nani.

Ni kweli Tanzania ni nchi maskini, kwani kipato cha mwaka cha mwananchi wa kawaida ni kama Sh. 770,463 hivi, yaani wastani wa kama Sh. 2,140 kwa siku, kiasi hiki cha fedha kwa maelezo yoyote ni kidogo sana kwa mwananchi kumudu mahitaji yake muhimu. Ni kidogo sana.

Lakini wakati wananchi walio wengi wakiishi katika umaskini wa kutupa, wapo watu waliaomua kusaka nafasi za uongozi katika nchi hii si kwa nia ya kusaidiana na wananchi kutokomeza umaskini ulioelemea taifa hili, ila kujitenga nao kwa kutengeneza taratibu mbaya na kandamizi za kujilipa mafao manono kama hizi zinazoitwa posho za vikao za wabunge.

Kwa maelezo yoyote yale, posho hizi si halali hasa zinapolipwa na taifa maskini kama Tanzania ambalo haliwezi hata kujitegemea kwa kuwa na bajeti yake walau kwa mwaka mmoja tu bila kutembeza bakuli kwa wafadhili. Hii ni aibu ya mchana kweupe.

Inawezekana walioweka utaratibu huo walipotoka, walipotea njia kwa kuwa ama walifunikwa na tamaa ya ubinafsi ya kujinufaisha wao, lakini wakati huu ambao sasa wananchi wamefunguka zaidi macho na kupitia kwa baadhi ya wawakilishi wao wanahoji mantiki hasa ya wabunge kujilipa posho ya vikao vya bunge wakati wanalipwa mshahara na pia posho ya kuwa nje ya vituo vyao vya kazi, inakuwa vigumu kujua kwa nini sasa hivi hawaoni ni wakati wa kuachana na utaratibu huo wa kujinufaisha kwa upendeleo wa wazi.

Hali kama hii pia inatokea ndani ya serikali, kuna taarifa za kutisha sana kwamba siku hizi hata kazi ambazo ni wajibu wa watumishi wa umma hazifanyiki mpaka kuwepo na uwezesho, yaani ofisa wa serikali kukaa kwenye kikao cha kazi ambayo ni wajibu wake, anadai kuwezeshwa.

Utaratibu huu hakika ndiyo donda ndugu kubwa kuliko yote linalodhoofisha uwezo wa serikali kutimiza wajibu wake kwa kuwa hata fedha kidogo inayopatikana kutokana na kodi za wananchi inaishia kuliwa kama posho zisizo na tija.

Wabunge ni lazima wajue kwamba wanapaswa kuwa mfano mzuri katika matumizi ya fedha za walipa kodi, si jambo la busara kung’ang’ania kulipwa posho mara mbili wakati taifa hili likiwa limegubikwa na umaskini mkubwa unaohitaji kila senti moja inayopatikana kutokana na kodi za wananchi kuelekezwa kwenye maeneo ambayo baada ya muda umaskini huo uonekane ukipungua siku baada ya siku.

Ni lazima sasa taifa hili likatae utamaduni wa posho. Hakika posho ni adui namba moja wa kutatua kero za wananchi, kama ugonjwa huu usipotibiwa hakika maendeleo ya taifa hili yataendelea kuwa ndoto.

No comments: