TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, June 14, 2011

Bunge lachafuka • Kafulila adai kuwakamata wabunge wakiomba rushwa

MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amewalipua wabunge wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba aliwakamata wakiomba rushwa kwenye halmashauri moja nchini iliyokuwa na hati chafu.

Kafulila aliwataja wabunge hao ambao ni wajumbe kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, (LAAC), kuwa ni Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki) na Omar Badwel (Bahi).

Mbunge huyo aliwataja wenzake hao jana bungeni wakati akichangia hoja ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.

Kafulila, hakuweza kuendelea kuyataja majina mengi zaidi ya wabunge aliowakamata kutokana na muda wake wa kuchangia hoja hiyo kumalizika baada ya kengele kulia.

“Mheshimiwa mwenyekiti kuna udhaifu mkubwa wa kimfumo katika kusimamia mipango ya maendeleo ndio maana mpango huo unaweza kufeli,”
“Wapo mawaziri na wabunge wanaokula rushwa. Mimi mwenyewe niliwakamata wabunge wakiomba rushwa usiku wa manane na wabunge hao wamo humu ndani,” alisema Kafulila.

Alisema tayari ameshachukua hatua kadhaa dhidi ya watuhumiwa hao ikiwemo kupeleka tuhuma zao kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU), pamoja na kumwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makina.

Kauli hiyo iliwafanya wabunge karibu wote ukumbini kunyamaza kimya na kumsikiliza kwa makini, hata hivyo hakuweza kuendelea kuyataja majina mengine mbali ya Zambi na Badwel baada ya Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachaweni, kumtaka akae chini kutokana na muda wake kumalizika.

Hata hivyo Kafulila alimtaja mbunge mwingine ambaye jina lake halikuweza kusikika vizuri kutokana na sauti yake kuingiliana na ya Simbachawene na baadhi ya wabunge walioanza kutoa maneno bila mpangilio kumtaka awataje kwa majina.

Wakati Kafulila, akilazimika kukaa na kukatiza hoja yake, Mwenyekiti wa Bunge alimwita mchangiaji mwingine aendelee, lakini baadhi ya wabunge walionekana wakinong’ona kujadili tuhuma hizo.

Baadhi ya wabunge walianza kumpelekea Kafulila, ‘vimemo’ ambavyo havikujulikana mara moja vilikuwa na ujumbe gani.

Wakati mchangiaji mwingine akiendelea, Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliomba mwongozo wa kiti cha Spika kutaka mbunge aliyeibua hoja hiyo nzito apewe nafasi ya kufafanua na hata kutoa ushahidi wa madai yake.

Simbachawene aliahidi kutoa mwongozo wa madai hayo kabla ya kuahirisha kikao cha jana jioni.

Akizungumzia madai hayo, Naibu Spika, Job Ndugai (CCM), alisema kuwa madai hayo aliwahi kuyasikia kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge ambapo Mwenyekiti wa Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema, aliwahi kutoa taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Ndugai, Mrema aliwasilisha madai ya Kafulila na kwamba mbunge huyo wa Kigoma Kusini, alikuwa anakusudia kupeleka taarifa hiyo kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

“Pia Kamati ya Uongozi ya Bunge tulijulishwa kwamba Kafulila atalipeleka suala hili TAKUKURU na kumwandikia Spika wa Bunge, Anne Makinda, barua rasmi kuhusiana na madai hayo. Zaidi ya hapo sina taarifa zaidi,” alisema Ndugai.

Kwa upande wake, Zambi ambaye alieleza kukerwa na tuhuma hizo, alisema kuwa kwa vile jambo hilo limetokea bungeni, kuna taratibu zake za kulijibu si kulizungumzia barabarani.

“Najua kiti cha Spika kitamtaka atoe ushahidi, akishafanya hivi, basi nitajua nini cha kufanya ila ni madai yasiyo na msingi na yenye lengo la kujitafutia umaarufu,” alisema Zambi.

Naye Badwel, alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi, alisema kuwa madai hayo ni uzushi wenye lengo la kujitafutia umaarufu.

No comments: