TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, June 6, 2011

MBOWE ATIKISA NCHI

Mbowe atikisa nchi
• Dk. Slaa asema huu ni mwisho wa uvumilivu
. Aitisha maandamano ya nchi zima
HATUA ya polisi kumshikilia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, imeibua simanzi na hasira miongoni mwa viongozi, wanachama, mashabiki wa CHADEMA na watetezi wa demokrasia ya vyama vingi.

Hali hiyo ilianza kujionyesha mapema jana asubuhi jijini Dar es Salaam na katika mikoa mingine nchini baada ya taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo kusambaa.

Tofauti na ilivyo ada, eneo zima linalozunguka Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam anakoshikiliwa kiongozi huyo lilikuwa limezingirwa na Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na zana za kijeshi.

Ili kuhakikisha kuwa hali inakuwa ni ya usalama, askari hao walikuwa wakirandaranda na kuwauliza watu waliokuwa wameanza kukusanyika katika eneo hilo shughuli walizokuwa wakifanya katika maeneo hayo.

Hata hivyo askari hao hawakuweza kuwazuia vijana walioanza kukusanyika eneo hilo na kuimba nyimbo za kulaani kukamatwa kwa kiongozi huyo kabla ya askari hao kutoa tangazo la kuwatawanya.

Katika eneo la Magomeni, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wapenzi wa CHADEMA waliokuwa wakiandamana kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi kulaani na kupinga kukamatwa kwa Mbowe.

Katika ofisi za makao makuu ya CHADEMA zilizoko Kinondoni, Katibu Mkuu wa chama hicho, Willibrod Slaa, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kulaani tukio la kukamatwa kwa Mbowe na lile la kushikiliwa kwa muda na polisi mjini Singida kwa Naibu Katibu Mkuu wao, Zitto Kabwe.

Akizungumza kwa hasira, Dk. Slaa aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho nchi nzima kujitokeza hadharani na kuchukua hatua za kupinga unyanyasaji na ukiukwaji wa demokrasia unaofanywa na jeshi la polisi na serikali ya CCM.

Katika tamko hilo, Dk. Slaa alisema viongozi wake hao waliokamatwa juzi, hawakukamatwa kwa mujibu wa sheria bali walikamatwa kwa mujibu wa maagizo ya kisiasa ya CCM, ambayo imeamua kutumia udikteta ili kujaribu kudhoofisha harakati za chama hicho za kuikomboa nchi.

Dk. Slaa ambaye kwa kawaida huzungumza taratibu na kwa upole, aliwataka wana CHADEMA kuacha kile alichokiita ukondoo na uvumilivu ambao wamekuwa wakiuonyesha siku zote.

Alisema tayari chama chake kimeshawasilisha malalamiko yote rasmi kwa Bunge la Uingereza (House of Commons) na vyama vya mabunge vya kimataifa kama “International Parliamentary Union” ili vichukue hatua za kidiplomasia za kukomesha unyanyasaji wanaofanyiwa wabunge wa upinzani Tanzania.

Pia alisema wameshawasilisha taarifa rasmi na yenye ushahidi wa kutosha kwa serikali ya Uingereza ya kuitaka ichukue hatua dhidi ya serikali ya Tanzania, kwani mabilioni ya pesa yaliyotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya mafunzo na programu nzima ya uboreshaji wa Jeshi la Polisi, yamefujwa huku polisi wakiwa bado hawajaelimika jinsi ya kuwatendea haki raia kwa mujibu wa sheria.

“Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) alinipigia simu akiniomba niwasihi wale vijana waondoke pale kituoni, na mimi nilimwambia sitawaambia waondoke. Sasa natangaza kuwa wafuasi wetu wote, nchi nzima sasa ni ruksa kuingia barabarani kupinga unyanyasaji huu. Viongozi waliokamatwa ni viongozi wa Watanzania.

“Asitokee mtu akatuambia tunakosa uzalendo, asitokee mtu akatuambia tunaharibu amani ya nchi. Wanaoharibu amani ya nchi ni Kikwete, CCM, na Jeshi la Polisi. Uvumilivu wetu umefika mwisho, ukondoo wetu umefika mwisho,” alisema Dk. Slaa na kushangiliwa na wafuasi kadhaa waliokuwa wakisikiliza tamko hilo.

Dk. Slaa alitumia muda mwingi kueleza jinsi Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mkoani Arusha, alivyokiuka vipengele kadhaa vya sheria kwa sababu za kisiasa, ili kujaribu kumdhalilisha na kumnyamazisha Mbowe na wabunge wa chama hicho, hasa katika kipindi hiki wanapokwenda kuipa changamoto kubwa serikali katika mkutano wa Bunge la Bajeti.

Alisisitiza kuwa, haikuwa halali kwa hakimu huyo kuamuru Mbowe akamatwe, kwani tayari alishatoa ruksa rasmi ya kimahakama ambayo iliwapa uhuru wa kuhudhuria shughuli za Bunge, wabunge wote wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi hiyo iliyotokana na maandamano yaliyofanyika Arusha Januari 5 mwaka huu.

Katika tamko lake hilo, Dk. Slaa alieleza mambo makuu manne kuthibitisha jinsi hakimu huyo anavyoiendesha kesi hiyo kisiasa badala ya kufuata sheria.

Kwanza alisema hakimu huyo alishatoa ruksa rasmi ya kuwaruhusu Mbowe na wabunge wenzake kuendelea na shughuli za bunge, lakini kwa makusudi uamuzi wa ruksa hiyo haukurekodiwa kimaandishi katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo kama ilivyo kawaida.

Hawakufanya hivyo ili kujijengea uhalali wa kuja kumkamata Mbowe kama walivyofanya.

Pili, alisema hakimu huyo hadi Ijumaa iliyopita wakati anatoa amri hiyo, alikuwa bado hajatoa hati ya kuitwa kwa mdhamini wa Mbowe ili ajieleze kwanini yeye na mshtakiwa wake hawajaonekana mahakamani kama taratibu za uendeshaji wa kesi zinavyotaka.

Badala yake, alisema kuwa hakimu huyo alikimbilia kutoa amri ya kutaka Mbowe akamatwe ili kutimiza kile alichoagizwa na serikali ya CCM.

“Na mdhamini wa Mbowe hakuweza kufika mahakamani kwa sababu ni mgonjwa, sasa anakimbilia kutoa amri ya kutaka watu wakamatwe bila kutoa haki ya mdhamini kujieleza….hii si sheria, ni siasa,” alisema Dk.Slaa.

Tatu, alisema wakati hakimu huyo anaamuru Mbowe akamatwe wakili wake hakuwepo mahakamani kwa sababu alikuwa akihudhuria kesi nyingine mbele ya Jaji kutokana ratiba za kesi kugongana.

Alisema kwa sababu wakili wa mshitakiwa Mbowe alikuwa akihudhuria kesi nyingine, kesi hiyo ilipaswa kuahirishwa siku hiyo kama taratibu za kisheria zinavyotaka, lakini kwa sababu ya kutaka kuifurahisha serikali ya CCM iliyomtuma, hakimu huyo hakufanya hivyo.

Badala yake aliiendesha kesi hiyo bila wakili kuwepo na akatoa hati ya Mbowe kukamatwa.

“Kwanza kesi yetu huanza saa 3:00 asubuhi, lakini katika hali isiyo ya kawaida siku hiyo alianza kesi hiyo mapema, saa 2:30 huku akijua fika kuwa wakili wa Mbowe hayupo. Sasa mdhamini wa mshtakiwa hakuwepo na hakuwa amepewa hati ya kuitwa kujieleza, na wakili wake pia hakuwepo alikuwa mbele ya Jaji akihudhuria kesi nyingine.

“Kwa taratibu za kimahakama, alipaswa kuiahirisha kesi hiyo, lakini yeye ili aifurahishe serikali iliyomtuma, aliiendeleza na kuamuru Mbowe akamatwe,” alisema Dk. Slaa.

Nne, Dk. Slaa alisema hata yeye na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, walipokwenda wenyewe mahakamani hapo wiki iliyopita, bado hakimu huyo alionekana kuwasikiliza wanasheria wa serikali waliotaka kesi hiyo isiendelee mpaka wakamatwe na polisi, wakati kwa taratibu za kisheria hati ya kumkamata mshitakiwa huisha mara tu mshitakiwa huyo anapokuwa ndani ya mahakama.

“Lengo lao lilikuwa lazima watukamate hata ndani ya mahakama, ili mradi tu watekeleze mkakati wao wa kutaka kutukandamiza na kutudhalilisha, sisi tulikataa….tulisema polisi hamjui sheria. Baada ya kubishana nao kwa hoja za kisheria ndio wakatuacha, vinginevyo hakimu yule alikuwa tayari tukamatwe mbele yake wakati ‘arrest warrant’ inakwisha mara baada ya mshtakiwa kufika mwenyewe mahakamani,” alifafanua Dk. Slaa.

Alisisitiza kwa namna yoyote Mbowe kwa nafasi yake kama mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) hakupaswa kukamatwa wakati huu ambao anatekeleza majukumu mengi ya kibunge yanayohusiana na bajeti.

Alisema mbali na ruksa iliyokuwa imetolewa na ambayo kwa makusudi haikurekodiwa, pia hakimu alipaswa kujua kuwa kiongozi huyo alikuwa akihudhuria vikao vya kamati mbalimbali za Bunge, vikiwemo vile vya kamati za chama chake (party caucus) ambavyo vinatambuliwa na kanuni ya 110 ya Bunge.

Akizidi kuonyesha jinsi kamata kamata hiyo ya wabunge na viongozi wa upinzani ilivyo ya kisiasa badala ya kuwa ya kisheria, Dk. Slaa alisema Zitto alikamatwa juzi akiwa Singida kwa hoja kuwa alifanya kosa kuhutubia mkutano hadi saa 12:20 badala ya kumaliza saa 12:00 jioni.

Alisema huo pia ulikuwa ni uonevu wa dhahiri kwani sheria inasema wazi kuwa kwa wakati huu ambao si wa uchaguzi, mikutano ya kisiasa ruksa kufika hadi saa 12:30, kwa hiyo alifafanua kuwa Zitto hakukiuka sheria yoyote kuhutubia hadi saa 12:20.

Alisema kukamatwa kwa Mbowe na Zitto kutasababisha kikao cha kamati ya uongozi ya bunge kilichopangwa kukaa leo ili kupanga ratiba ya bunge la bajeti kisifanyike kama inavyotakiwa, kwani ni lazima mmoja wao kati ya viongozi hao wahudhurie kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

“Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni ni mjumbe wa lazima katika kikao cha kamati ya uongozi ya Bunge, asipohudhuria ni lazima ateue mwakilishi wa kuhudhuria kama kanuni zinavyotaka, sasa tutamwambia Zitto asiende, kwa sababu anayepaswa kumteua kumwakilisha yupo ndani,” alisema Dk. Slaa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), John Heche akizungumza na wanafunzi wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu, Augustine Mwanza, pamoja na mambo mengine, alitoa onyo kwa Rais Kikwete kuwa atakuwa rais wa kwanza kuandika historia mbaya kabisa ya kusababisha machafuko katika nchi hii iwapo hataacha kulitumia Jeshi la Polisi vibaya kukandamiza wapinzani.

“Tutaendelea kuheshimu sheria za nchi na kulinda amani ya nchi hii, lakini kamwe hatutalinda uonevu, dhuluma wala unyanyasaji unaoanza kufanywa kwa kasi na Jeshi la Polisi, kwa kuwakamata wabunge na viongozi wetu wa kitaifa bila sababu za msingi. Hatuko tayari kuvumilia udikteta wa serikali ya CCM inayotaka kuigeuza nchi yetu kuwa dola ya kipolisi. Tutapigania haki bila kuogopa risasi, mabomu na virungu vya polisi.

“Tunalionya Jeshi la Polisi na CCM, Tunamuonya Rais Kikwete, tunamtaka achunge mwenendo wa serikali yake na vyombo vyake vya usalama, vinginevyo atakuwa Rais wa kwanza kuandika historia mbaya ya kusababisha machafuko katika nchi hii. BAVICHA tunaendelea kufuatilia na tuko tayari kuchukua hatua. Busara na uwezo wetu wa kulinda amani na kupigania haki, si vya kutiliwa shaka,” alisema Heche.

Wakati Heche akitoa kauli hiyo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alifika Kituo Kikuu cha Polisi na kukutana na Mbowe alilaani kitendo hicho cha polisi.

Mbali ya hilo, Profesa Lipumba alimtaka Spika wa Bunge kutoa tamko la kupinga kamatakamata hiyo ya wabunge wa upinzani ambayo imemgusa pia mbunge mmoja wa CUF.

Mbali ya Lipumba viongozi wengine wa kisiasa waliofika kituoni hapo kuonana na Mbowe ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Profesa Abdallah Safari.

Viongozi wa CHADEMA mikoani watoa tamko

Viongozi wa CHADEMA wa mikoa mbalimbali jana pia walitoa matamko ya kulaani na kupinga kukamatwa kwa Mbowe.

Mkoani Mara, Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa CHADEMA, Mwita Mwikwabe Waitara akisoma maazimio tisa ya mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho kwa waandishi wa habari mjini Musoma jana alisema, kitendo cha polisi kumkamata Mbowe wakati wakielewa ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni hakivumiliki.

Alisema, endapo serikali na jeshi la polisi haitamwachia Mbowe mara moja, wana-CHADEMA wa mkoani Mara wataungana na mikoa mingine nchini kutumia nguvu ya umma ili kiongozi huyo aachiwe huru.

Waitara alisema kukamatwa kwa Mbowe ni kinyume cha sheria ya mwaka 1992 inayotoa kinga kwa wabunge kudhalilishwa hadharani na kusisitiza kwamba serikali inapaswa kuomba radhi kwa kitendo hicho, tena kinachofanywa kwa wabunge wa upande mmoja tu wa upinzani.

Mkoani Dodoma, viongozi wa chama hicho nao walitoa tamko hiyo jana wakitaka Mbowe aachiwe kwani vikao vya bajeti vinaanza kesho.

Tamko hilo lililosomwa na Katibu wa CHADEMA mkoa wa Dodoma, Steven Masawe, pamoja na kuungwa mkono na umoja wa vyuo vikuu mkoani hapa.

Kwa pamoja wameazimia kufanya maadamano ili kusitisha shughuli za Bunge kwa madai kuwa kama Mbowe hataachiwa, bunge halitakuwa na uwakilishi mzuri wa kutetea maslahi ya Watanzania.

“Inasikitisha kuona serikali ikiiacha kukamata mafisadi wanaolisababishia hasara kubwa taifa, na badala yake inakamata viongozi wema kama mwenyekiti wetu bila sababu zozote za msingi,” alisema Kalogi.

No comments: