TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, June 6, 2011

JK AWAPASHA VIONGOZI WA DINI. Asema wapo wanaouza dawa za kulevya

RAIS Jakaya Kikwete, amewaonya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini kuacha tabia ya kushiriki biashara ya kuuza dawa za kulevya na badala yake washirikiane na viongozi wa serikali kuidhibiti biashara hiyo haramu.

Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga wakati wa ibada maalumu ya kupewa daraja la uaskofu na kusimikwa kwa askofu wa jimbo hilo, Mhashamu John Ndimbo, katika kanisa la kiaskofu la Mtakatifu Killian iliyohudhuriwa pia na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa.

Alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakishiriki kufanya biashara hiyo ya dawa za kulevya kwa kuwatumia vijana ambao huwafanyia mipango ya kuwatafutia hati za kusafiria (Passport) kwenda nchi za nje.

Badala yake Rais Kikwete amewataka viongozi hao nchini kuikemea biashara hiyo na kujenga uhusiano mzuri na vyombo vya dola katika kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa kwa kuwafichua wahusika wanaoifanya ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Inasikitisha sana na kutisha, biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili kwani baadhi yenu tumewakamata.

“Kwa kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususan vijana waweze kuepuka na matumizi ya dawa hizi,” alisema Rais Kikwete.

Ameyaomba pia madhehebu ya dini nchini kuweka mipango endelevu ya maendeleo ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika mipango yao ya kimaendeleo ili kuisaidia jamii katika ushindani wa soko la ajira.

Alieleza kuwa kutokana na wananchi wengi kukabiliwa na tatizo kubwa la ajira ni vyema sasa serikali kwa kushirikiana na madhehebu ya dini kujikita zaidi katika kujenga vyuo vya ufundi ambavyo vitasaidia kupunguza kero iliyopo ya ukosefu wa ajira hususan vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari.

“Kufanikiwa kwa viongozi wa dini katika shughuli za kimaendeleo ni faraja kwa serikali iliyo madarakani na Watanzania wote kwa ujumla,” alisema Rais Kikwete.

Awali Rais wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki, Tanzania, Askofu Yuda Thadei Ruwa’ichi, aliiomba serikali kuwa makini wakati wa kuandaa bajeti ya nchi ambayo inatarajiwa kupitishwa bungeni hivi karibuni.

Alisema bajeti hiyo ni vyema izingatie maendeleo ya Watanzania ambao wengi wao ni maskini.

Aliishauri pia serikali kudumisha amani na utulivu nchini kwa kuhakikisha wakati wote vitendo vya vurugu havipewi nafasi kamwe na kwamba kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na serikali na Watanzania wote bila ubaguzi wa rangi, dini au ukabila.

Naye Askofu Ndimbo baada ya kusimikwa alitoa shukurani zake kwa Rais Kikwete na waumini wa jimbo hilo na kuahidi kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Askofu huyo alisema kuwa kazi yake kubwa ni ya kuwachunga kondoo wa Mungu (waumini) pamoja na kuwahamasisha kujikita katika kilimo cha kisasa ambacho kitawasaidia kupunguza ukali wa maisha.

No comments: