TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, June 5, 2011

ZITTO NA MBOWE WATIWA MBARONI


MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi baada ya kujisalimisha katika kutuo Kikuu cha jijini Dar es Salaam.Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, jana alikamatwa na polisi mjini Singida kwa kosa la kuzidisha muda wa kuhutubia mkutano wa hadhara.Habari zilizopatikana kutoka Singida na kuthibitishwa na Zitto mwenyewe, zinaeleza kuwa polisi walimkamata jana jioni kwa madai kuwa alihutubia mkutano wa hadhara mpaka zaidi ya saa 12:00. Muda wa mwisho kisheria kuhutubia mkutano wa hadhara ni saa 12:00 jioni."Mpaka sasa bado nipo polisi wanaendelea kunihoji," alisema Zitto kwa kifupi.

Hadi tunakwenda mitamboni, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alikuwa bado ameshikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini Singida.Kukamatwa kwa Mbowe kunafuatia amri ya mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuamuru akamatwe popote alipo na kufikishwa mahakamani kwa kutotii amri ya kufika mahakamani katika kesi yake.

Juni 2 mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa, alikubaliana na hoja ya wakili upande wa Serikali kuitaka mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Mbowe kwa sababu ya kutotii amri ya kufika kortini au kumtuma mdhamini wake.Alisema sababu iliyotolewa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo ni mbunge na yupo kwenye vikao vya Kamati za Bunge haina uzito kwa kuwa hiyo ni moja ya shughuli zake kama ilivyo shughuli nyingine kwa watumishi wa Serikali.

Hakimu Magesa akitoa agizo hilo alisema kuwa inachokumbuka ni kwamba mahakama hiyo ilipokea maelezo ya kuwa washtakiwa hawatahudhuria mahakamani hapo Mei 27, mwaka huu na kwa sababu ya kuwapo vikao vya kamati za Bunge iliagiza wafike wadhamini wao kesi inapotajwa. Ndiyo maana Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alimpeleka mdhamini.Katika kesi hiyo iliyopangwa kuendelea kusikilizwa kesho, Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali Januari 5, mwaka huu jijini Arusha.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando alithibitisha jana kukamatwa kwa Mbowe saa 9:00 alasiri kutokana na amri ya mahakama."Ni kweli amekamatwa saa moja iliyopita kwa sababu ni amri ya mahakama na chama hakiwezi kumwombea dhamana itabidi apelekwe Arusha," alisema Marando.

Pamoja na Marando kuthibitisha kukamatwa kwa Mbowe, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema halina taarifa zozote za kukamatwa kwa mwenyekiti huyo.Jeshi hilo limesema halina taarifa zozote juu ya mwenyekiti huyo kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. Mei 27, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wake, Mbowe.

Pamoja na viongozi hao, mahakama hiyo pia iliamuru wabunge wawili wa chama hicho, Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wakamatwe na kufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kuhudhuria mara kadhaa . Lakini, viongozi hao waliwasiliana na mahakama hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.
Awali asubuhi, akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda Shilogile alisema kuwa hana taarifa zozote za Mbowe kukamatwa au kujisalimisha katika kituo hicho.

“Sina taarifa zozote kuhusiana na kukamatwa kwa Mwenyekiti cha Chadema. Taarifa hizi ndiyo nazisikia kwenu waandishi wa habari. Mimi wala uongozi wangu hauna taarifa hizo,”alisema Shilogile na kuongeza;
“Angekuwa amekamatwa au amekuja kujisalimisha mkoa wangu ndiyo ungekuwa wa kwanza kupata taarifa hizo, labda mtafute Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kama ana taarifa hiyo anaweza kukwambia.”Kova alipotafutwa kwa njia ya simu alisema yuko Zanzibar na kwamba hana taarifa zozote za kukamatwa kwa Mbowe.

Marando, Tundu Lissu
Mapema asubuhi Marando na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu walionekana wakiingia katika Ofisi ya Mpelelezi wa Mkoa wa Ilala (RCO), Diwan Nyanda.Alipoulizwa ujio wake katika ofisi hizo, Marando alisema kuwa alikwenda katika ofisi hizo kwa shughuli zake binafsi na kwamba hana taarifa za kukamatwa kwa Mbowe.

Akizungumza na Mwananchi Alhamisi wiki hii baada kutolewa amri ya kukamatwa kwake, Mbowe alisema anatarajia kutoa tamko kuhusu suala hilo Ijumaa jijini Dar es Salaam.“Nitatoa tamko kesho, lakini nasikitishwa na tafsiri hii ya Mahakama kwamba mimi nimekaidi amri ya kufika katika vikao vya mahakama...,” alisema Mbowe

Mnyika
Katika hatua nyingine Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) amesema chama hicho kitaandika barua rasmi katika Ofisi za Bunge kueleza jinsi wabunge wa vyama vya upinzani wanavyokamatwa bila kufuata kanuni na taratibu, wakati wana kinga ya kibunge inayowazuia kukamatwa bila kibali.

Alisema mpaka sasa wabunge wa upinzani ambao wamewahi kukamatwa bila kuombwa kwa kibali chochote kutoka kwa Spika wa Bunge ni pamoja na Godbless Lema (Arusha Mjini), Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini), Joseph Selasini (Rombo), Meshack Opulukwa (Meatu)

Wengine ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalumu-Chadema) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF) ambaye mpaka sasa yuko mahabusu mkoani Tabora huku kesi yake inatarajiwa kutajwa Juni 6 mwaka huu.

No comments: