JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
KUSITISHA BIASHARA YA WANYAMAPORI HAI
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa kutokana na Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 435 la tarehe 09 Desemba 2011 wafanyabiashara wenye vibali halali vya kumiliki na kusafirisha wanyamapori ambavyo hadi tarehe 18 Agosti, 2011 vilikuwa havijamaliza muda wake kisheria wanatakiwa kusafirisha wanyama hao ndani ya kipindi cha miezi mitatu (siku 90) tangu tarehe 9 Desemba 2011.
Tangazo hili la Serikali limetolewa kwa kutambua kuwa wakati amri ya kusitisha biashara ya wanyamapori hai ilipotolewa tarehe 18 Julai 2011, kuna baadhi ya kampuni ambazo tayari zilikuwa na wanyamapori katika mazizi yao waliokuwa wamekamatwa kwa mujibu wa sheria.
Muda uliotolewa kwa wafanyabiashara ni kwa mujibu wa Kanuni za Ukamataji wa Wanyamapori za mwaka 2010 zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 244 la tarehe 02 Julai, 2010. Kanuni ya 12(4) na (5) ya Kanuni hizo inaelekeza kuwa wanyamapori waliokamatwa kwa ajili ya usafirishaji nje ya nchi kibiashara wanatakiwa wawe wamesafirishwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu kukamatwa.
Vilevile, kutokana na Tangazo hilo (Na. 435 la tarehe 09 Desemba 2011) Wizara imezuia Ukamataji, Uingizaji na Usafirishaji wa Wanyamapori hai isipokuwa wadudu tu (Class 21). Hii inatokana pia na Amri ya kuzuia ukamataji ijulikanayo kama The Wildlife Conservation (Capture of Animals) (Prohibition) Order, 2011.
Mwisho, Wizara inapenda kuufahamisha Umma kuwa matumizi mengine ya wanyamapori hai pamoja na mazao yake kwa shughuli zisizo za kibiashara na zenye manufaa kwa Taifa, kama vile utafiti, yanaruhusiwa.
George Matiko
MSEMAJI WA WIZARA
14 Desemba 2011
No comments:
Post a Comment