|
|
Waandishi wetu SAKATA la posho za wabunge limezidi kuingia katika sura mpya, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kukwepa mdahalo uliohusu mada hiyo, huku Katibu wake, Dk Thomas Kashilillah, akitua mzigo kwa kutotaka ahusishwe tena kwenye mjadala huo.Wakati viongozi hao wa juu wa Bunge wakikwepa kuzungumzia suala hilo, wasomi, wanaharakati na viongozi wa dini kutoka kona mbalimbali za nchi, wamekuja juu wakipinga nyongeza hiyo. Makinda akacha mdahalo Jana, Makinda alikwepa kipindi cha luninga cha Channel Ten cha Asubuhi Njema ambacho mada yake ilikuwa kuzungumzia nyongeza ya posho za wabunge akisema "iwapo mjadala wenu ni kuhusu posho, sitashiriki kipindi hicho." Mtangazaji wa kipindi hicho, David Ramadhan alisema awali, aliwasiliana na Spika Makinda kwamba angekuwa mgeni katika kipindi hicho, lakini dakika za mwisho, aligeuka na kusema asingeweza kushiriki mjadala huo iwapo mada ni nyongeza ya posho za wabunge. “Jamani ilikuwa tuwe na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda ambaye hata hivyo amesema hataweza kushiriki kipindi iwapo mjadala wenyewe ni huo unaohusiana na ongezeko la posho za wabunge,”alisema mtangazaji huyo akiwajulisha watazamaji. Kutokana na hali hiyo, Ramadhani aliwasiliana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ili atoe ufafanuzi kuhusu msimamo wa CCM juu ya nyongeza hiyo ya posho. Nape alikazia msimamo wa chama hicho kuwa wanapinga ongezeko hilo kwa nguvu zote. Jitihada za gazeti hili kumpata Spika Makinda jana ili azungumzia msimamo wake huo wa kukimbia mjadala wa posho hazikuzaa matunda kutokana na simu yake ya mkononi mara kadhaa kuita bila kupokelewa na wakati mwingine, inakatwa.Taarifa zilizopatikana baadaye ofisini kwake zilieleza kuwa muda mwingi jana, Spika Makinda alikuwa na kikao. Dk Kashililah Kwa upande wake, Dk Kashililah jana aliamua kutua mzigo baada ya kukataa kuhusishwa tena na mjadala wa posho za wabunge unaoendelea nchini. Dk Kashililah aliliambia gazeti hili kuwa kauli ya CCM kutaka nyongeza ya posho iondolewa kwa sababu maisha magumu, haimuhusu na yeye hana jipya kwenye mjadala huo. “Hayo ya CCM hayanihusu… Unanionea tu ndugu yangu,” alisema Dk Kashililah alipotakiwa kutoa msimamo wake kuhusu ushauri wa CCM uliotolewa juzi na Nape. Kuhusu mgongano wa kauli yake na ile ya Spika Makinda kuhusu posho za wabunge, Dk Kashililah alisema" “Wewe ndio unasema (tulitofautiana).” Wasomi, viongozi dini, wanaharakati Wakati huo huo wasomi nchini wamesema suala la ongezeko la posho hizo kwa wabunge halijazingatia haki na usawa katika jamii hali itakayoweza kusababisha madhara makubwa katika ustawi wa uchumi na maendeleo ya jamii. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema wabunge waliopitisha kupanda kwa malipo ya posho zao katika vikao vyao, hawana machungu na maendeleo ya taifa, kwani wanachukua pesa nyingi kuliko wafanyakazi wa idara nyingine. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, (UDSM) Dk Benson Bana, alisema wabunge wote wanaotaka pesa zipande, hawana budi kuachia madaraka kwani wanalinyonya taifa. Alisema wabunge wanatakiwa kufahamu kwamba Serikali ni masikini hivyo wanavyopitisha suala la kupata posho kubwa ni sawa na kuitia nchi umasikini. “Hawa jamaa mimi siwaelewi kabisa unajua kitendo cha kupandishiwa posho kutoka Sh70,000 mpaka Sh200,000 ni sawa na kulitia umaskini taifa letu,”alisema Bana. Dk Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema sababu iliyotolewa kwamba posho hizo zimepanda kutokana na hali ngumu ya maisha, haina mashiko kwani ugumu wa maisha hauko mkoani Dodoma pekee. “Kitendo cha kujiongezea posho kwa wabunge hao kimekuja baada ya kikundi cha watu wachache ambao ni watunga sera na sheria kukaa na kujadili namna ya kujipatia ahueni ya maisha na kuamua kujipandishia hizo posho bila kuangalia mwananchi wa kawaida ambaye ni mlipa kodi atakuwa anaishi katika hali gani,”alisema Dk Ngowi. Profesa Robert Mabele wa Chuo Kikuu cha Dar e s Salaam, alisema kupanda kwa posho hizo kunamkandamiza mwananchi wa kawaida akiwamo mwalimu. Alisema Bunge linatakiwa kuhakikisha kwamba mapato ya Mtanzania yanatakiwa kuwa na uwiano sawa na haya mabadikilo yanatakiwa kufanyika kwa watu wote sio kwa wabunge tu.Mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashiru Ally alisema kupanda kwa posho za wabunge ni kukomaza utabaka kati ya walionacho na wasio nacho. Laltaika, alisema ongezeko hilo ni kubwa, lakini sababu za kupanda gharama za maisha linawagusa watanzania wote na sio wabunge peke yao huku akisistiza kuwa kitendo hicho ni ubadhirifu mkubwa serikalini usiovumilika. | ALIALIKWA CHANNEL TEN, AWAAMBIA KAMA NI KUHUSU POSHO 'SIJI', WENGI WAPONDA, CAG KUFANYA UCHUNGUZI
No comments:
Post a Comment