SEMA HAKUZALIWA KWA AJILI YA TUZO, LOWASSA HANA TAARIFA, SITTA KIMYA
WAZIRI Mkuu Mstaafu, John Malecela amesema Ikulu ndiyo inayojua sababu za yeye kutostahili kupata nishani na kwamba hakuzaliwa kwa ajili ya kupata tuzo hiyo.Kauli hiyo Malecela ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, imekuja siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwatunuku nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili, wanasiasa mbalimbali waliowahi kushika nyadhifa za Uwaziri Mkuu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Muungano wa Tanzania, huku yeye, na viongozi wengine kadhaa wakikosa.
Viongozi wengine waliokosa ni nishani hizo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa na Spika Mstaafu wa Bunge la tisa, Samuel Sitta. Hata hivyo, baada ya viongozi hao kuachwa katika orodha ya waliotunukiwa nishani hizo kumekuwa na maswali kuhusu vigezo vilivyotumika kuwaengua ingawa tayari Rais Kikwete alivitangaza, ikiwamo uadilifu katika kulitumikia taifa wakati wa kazi na baada ya kustaafu.
Akizungumzia sababu za yeye kukosa nishani hiyo jana, Malecela ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa Rais kati ya mwaka 1990 hadi 1994 wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema wanaojua sababu ni Ikulu kwa kuwa wao ndiyo waliokuwa na orodha hiyo.
Malecela alienda mbali zaidi akisema yeye hakuzaliwa ili apate nishani, hivyo ni muhimu vyombo vya habari vikaacha kukuza mambo ambayo hayana msingi.
Alisema:, "Mnataka kujua nini? Sikuzaliwa ili nipate nishani..., kaulizeni Ikulu na muache kukuza haya mambo, ninawasihi sana mbadilike na muandike mambo muhimu".
Alisema kwa kuwa yeye siyo mwenye orodha ya waliokuwa wanatakiwa kupata nishani hivyo, hawezi kujua nani alitakiwa apate na nani alitakiwa kukosa, hivyo Ikulu ndiyo wanaojua.
"Please don't make it an issue(tafadhali msifanye ni kitu cha muhimu), sikuzaliwa ili nipate nishani, acheni suala hilo ni uchonganishi, acheni,"alisema Malecela.
Alisema nishani zimekuwa zikitolewa nyingi katika sherehe mbalimbali zilizopita na hata hizi za juzi sio kitu cha ajabu na kwamba habari iliyoandikwa kwenye vyombo vya habari jana kuhusu yeye kukosa nishani ni kukuza mambo.
"Msitake kukuza mambo serikali imefanya mengi, mbona wakati wa kutoa degree(shahada) huwa kuna wengine wanakosa na wengine wanapata si sawa, please acheni hilo suala,"alisema Malecela.
Mbali na nyadhifa hizo za juu serikalini, mwanasiasa huyu pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM mwaka 1995 hadi 2007, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (1964-1966), Waziri wa Mambo ya Nje (1972-1973), Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki (1975-1976), Mkuu wa Mkoa wa Iringa (1980-1984) , pia amekuwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa huenda amekosa nishani hiyo kutokana na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutunga kitabu mwaka 1995 alichoikiita ‘Uongozi wetu na hatma ya uongozi Tanzania’ kilichoainisha udhaifu kadhaa kisiasa wa kiongozi huyo.
Lowassa
Kwa upande wake Waziri Mkuu aliyejiuzulu Lowassa, akizungumzia kukosa nishani hiyo, alisema hakuwa na taarifa yoyote ya kilichotokea kwa kuwa yuko kijijini kwao Monduli.
"Tumekosa mimi na nani? Niko kijijini na sijasoma gazeti mpaka nilipate ndiyo nijue andika hivyo,"alisema Lowassa kwa kifupi baada ya kuulizwa kwa njia ya simu.
Lowasa alikuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 2005 hadi Februari mwaka 2008, katika Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete, alijiuzulu kufuatia kashfa ya utoaji zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni tata ya Richmond Development LCC.
Sitta asema aachwe
Alipoulizwa Spika wa Bunge la Tisa, Sitta kuhusu kutopata nishani hiyo, alisema kwa sasa asingependa kulizungumzia suala hilo na kusisitiza, "hilo liache kwanza, sitaki kulizungumzia".
JK na nishani
Mbali ya kuwaacha viongozi hao wakuu wastaafu katika serikali, pia katika mhimili mwingine wa dola wa kutunga sheria (Bunge) Rais aliwatunuku nishani hiyo spika wa zamani, Pius Msekwa na wa sasa, Anne Makinda, lakini akamnyima Samuel Sitta ambaye aliongoza Bunge la Tisa, kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Oktoba mwaka jana.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam, kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika , Rais Kikwete alitunuku nishani za aina tatu kwa Watanzania 57 waliotoa michango mbalimbali ya kutukuka kwa maendeleo ya nchi katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wake, huku pia akimwacha aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi.
Nishani hizo ni ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwenge wa Uhuru Daraja la kwanza na Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili.
Kikwete aliweka wazi kwamba, nishani hizo zimetolewa kwa Makamu Rais na mawaziri wakuu wastaafu walio hai ama waliokufa, walioondoka madarakani bila kashfa na hata baada ya kuondoka kwao madarakani, wameendelea kuwa na maadili mema na kuishi kwa heshima na maadili ya ofisi yao.
Viongozi wengine waliotunikiwa nishani hizo ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Aman Karume, Hayati Rashid Mfaume Kawawa, Hayati Edward Moringe Sokoine, Hayati Idrisa Abdul Wakili na Hayati Dk Omary Ali Juma.
Wengine ni Rais wa sasa wa Zanzibar ambaye aliwahi pia kuwa Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana , Dk Ali Mohamed Shein, na mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, Dk Salim Ahmed Salim na Fredereck Sumaye.
Nishani ya juu kabisa iliyotolewa na Rais Kikwete ni ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo walitunukiwa maraisi wa awamu zote tatu zilizopita, Hayati Mwalimu Nyerere ambayo ilipokelewa na Mama Maria Nyerere kwa niaba yake, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
No comments:
Post a Comment