RAIS Jakaya Kikwete amewatunuku nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili wanasiasa mbalimbali waliowahi kushika nyadhifa za Uwaziri Mkuu na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Muungano wa Tanzania, huku akiwatosa Edward Lowassa, John Malecela na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ambao nao, waliwahi kutumikia nafasi hizo.Vilevile, amemtunuku nishani hiyo spika wa zamani wa bunge, Pius Msekwa na wa sasa, Anne Makinda na kumtosa Samuel Sitta ambaye aliongoza Bunge la Tisa, kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Oktoba mwaka jana.
Katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam juzi, kama sehemu ya maadhimisho ya kilele cha kumbukumbu ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, Rais Kikwete alitunuku nishani za aina tatu kwa Watanzania 57 waliotoa michango mbalimbali ya kutukuka kwa maendeleo ya nchi katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wake.
Kikwete aliweka wazi kwamba, nishani hizo zimetolewa kwa Makamu Rais na Mawaziri Wakuu wastaafu walio hai ama waliokufa, walioondoka madarakani bila kashfa na hata baada ya kuondoka kwao madaraka, wameendelea kuwa na maadili mema na kuishi kwa heshima na maadili ya ofisi yao.
Katika kundi hilo, Rais Kikwete aliwatunuku watu 10 na kuwaacha Malecela, Lowassa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kujiuzulu mwaka 1984, kufuatia kile kilichoelezwa kuwa, machafuko ya hali ya hewa kisiasa Zanzibar.
Waliotunikiwa nishani hizo ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Aman Karume, Hayati Rashid Mfaume Kawawa, Hayati Edward Moringe Sokoine, Hayati Idrisa Abdul Wakili na Hayati Dk Omary Ali Juma.
Wengine ni Rais wa sasa wa Zanzibar ambaye aliwahi pia kuwa Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana , Dk Ali Mohamed Shein, na mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa Msuya, Joseph Warioba, Dk Salim Ahmed Salim na Fredereck Sumaye.
Malecela akosa
Malecela alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1990 hadi 1994, wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mbali na nyadhifa hizo za juu serikalini, mwanasiasa huyu pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM mwaka 1995 hadi 2007, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (1964-1966), Waziri wa Mambo ya Nje (1972-1973), Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki (1975-1976), Mkuu wa Mkoa wa Iringa (1980-1984) , pia amekuwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza.
Akiwa katika kilele cha siasa za Tanzania, Malecela alionekana kuwa mwanasiasa mwenye nguvu na kuaminiwa katika Serikali ya Awamu ya Pili, hatua iliyompa nafasi kubwa kwamba huenda angemrithi Rais Mwinyi baada ya kumaliza muda wake kikatiba mwaka 1995.
Hata hivyo, rekodi yake ilichafuliwa wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, baada ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutunga kitabu alichokiita ‘Uongozi wetu na hatma ya uongozi Tanzania’ kilichoainisha udhaifu kadhaa kisiasa wa kiongozi huyo na kumkosoa.
Kitabu hicho kilizima ghafla ndoto ya Malecela kuzidi kukwea milima ya kisiasa na kuwaacha njiapanda wachunguzi wa mambo ya kisiasa walioamini kuwa alikuwa kete muhimu ya Rais Mwinyi kurithi kiti chake, bila kujua mtu wa kurithi nafasi hiyo, kabla ya Rais Mkapa kuibuliwa na kuwa Rais ambaye hakutarajiwa na wengi.
Lowassa atoswa
Kwa upande wake Lowasa alikuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 2005 hadi Februari mwaka 2008, katika Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete .
Lowassa ambaye ni mshirika wa siku nyingi kisiasa wa Rais Kikwete, alijiuzulu kufuatia kashfa ya utoaji zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni tata ya Richmond Development LCC.
Hivi karibuni kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichofanyika mjini Dodoma, Lowassa alijaribu kujitetea dhidi ya kashfa hiyo lakini hata hivyo wachunguzi wa mambo wanasema bado hajawa safi mbele ya serikali inayoongozwa na swahiba wake Rais Kikwete.
Lowassa alisema hakuhusika moja kwa moja katika hilo lakini alilazimika kujiuzulu kwa sababu waliozembea na maofisa walioko chini yake.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa dhamira yake ilikuwa kuvunja mkataba wa Richmond jambo alilomjulisha pia mkubwa wake(Rais Kikwete) kwa simu akiwa nje ya nchi, lakini Rais alimwambia asubiri kwanza kwani alipata ushauri kutoka kwa makatibu wakuu kuhusu jambo hilo.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa gazetini kwa kile walichoeleza nafasi zao nyeti ndani ya serikali, walisema utetezi wa Lowassa bado haujakidhi kumfanya awe safi, ndio maana hakuweza kutunukiwa tuzo hiyo.
Walitoa mfano kwamba kwenye sherehe hizo, Rais Kikwete alimtunuku Nishani ya Juu ya Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ingawa naye aliwahi kujiuzulu kutokana na kashfa ya mauaji ya vikongwe mkoani Shinyanga wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Mwalimu Nyerere. Kwa uwajibikaji huo, Rais Kikwete aliutaja kuwa ni moja ya mambo ambayo yalionyesha kuwa Mwinyi ni mwadilifu.
Wachunguzi wa mambo haya siasa wanadai kitendo cha Mzee Mwinyi kujiuzulu na leo anatunukiwa nishani hiyo ni changamoto muhimu kwa Lowassa kutambua kuwa pamoja na maelezo yake ndani ya NEC, bado usafi kwa kashfa zinazomwandama unatia shaka, kwani yeye alijiuzulu baada ya Bunge kuunda tume iliyochunguza na kutoa mapendelezo ya ‘kupima’ lakini Mzee Mwinyi alipima mwenyewe uzito wa tukio na kuamua kuachia ngazi.
Mzee Aboud Jumbe Mwinyi
Mzee Jumbe ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais katika kipindi cha mwaka 1972 hadi 1984 naye ni mmoja wa watu ambao hawakutunukiwa nishani hiyo mbali na kutumikia nafasi hizo kutokana na dosari zilizojitokeza wakati wa utumishi wake.
Aboud Jumbe lijiuzulu mwaka 1984 kutokana na kile kilichoelezwa, machafuko ya hali ya kisiasa visiwani Zanzibar yakihusisha chokochoko zilizokuwa na viashirio vya kuvunja Muungano.
Samuel Sitta
Kwenye sherehe hizo pamoja na kutunuku Msekwa na Makinda wengi wamejiuliza sababu za kutoswa kwa ‘Spika wa Bunge la Kasi na Viwango’, Samuel Sitta.
Baadhi ya wanasiasa wazoefu waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa wameshangazwa na kitendo cha maspika hao kutunukiwa nishani na Sitta ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuachwa.
Mmoja wa wanasiasa hao kutoka CCM ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema huenda Sitta hakupewa zawadi kutokana na chama hicho tawala kumtuhumu kuwa anaongoza makundi ya upinzani ndani ya chama, jambo ambalo mara kadhaa mwanasiasa huyo amekuwa akilikanusha.
Alisema huenda kutokana na msimamo wake imara usioyumba wa kupambana na vitendo vya ufisadi bila woga ndilo jambo ambalo linalokera wenzake ndani ya chama hicho nakutafsiri kwamba ni kukigawa chama .
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alisema hajui vigezo vilivyotumika kutoa nishani hizo lakini yeye anaamini Sitta aliweza kulifanya Bunge kuendesha mambo kiuwazi kiasi cha kuwafanya wananchi wengi kuwa na imani nalo.
“Alisema tangu awali Bunge lake litakuwa la ‘standard and speed’ (kasi na viwango ) na liliweza kuonyesha hilo… lakini mimi Napata kigugumizi cha kusema sababu sijui vigezo vilivyotumika,” alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na alihudhuria sherehe hizo.
Alisema ingawa yeye alichelewa kufika kwenye sherehe hizo, alishangazwa kusikia kuwa Makinda amepata tuzo hiyo wakati kipindi chake cha uspika hakijamalizika.
Spika mwingine ambaye hakutajwa kwenye orodha hiyo ni Yule aliyekuwa wa kwanza baada ya Tanzania kupata uhuru, Chifu Adam Sapi Mkwawa (1964-1973 na 1975-94) na Erasto Mang'enya (1973-75).
Nishani ya juu kabisa iliyotolewa ni ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo walitunukiwa maraisi wa awamu zote tatu zilizopita, Hayati Mwalimu Nyerere ambayo ilipokelewa na Mama Maria Nyerere kwa niaba yake, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
No comments:
Post a Comment