TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE
Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com
Friday, August 19, 2011
NGELEJA AWATANIA WATANZANIA, AIINGIZA NCHI KATIKA MGAO MKALI WA UMEME.
MKOA WA MWANZA WIKI SASA HAUNA UMEME
WIKI moja baada ya kupitishwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyojaa mikakati ya dharura ya kukabiliana na tatizo la mgawo wa umeme, maeneo mengi nchini yamejikuta yakikabiliwa na tatizo hilo.
Waziri wa Nishati na madini, William Ngeleja, Jumamosi wiki iliyopita aliwasilisha bungeni mpango wa dharura wa kupata umeme kuanzia mwezi huu hadi Desemba mwakani unaotarajia kugharimu jumla ya Sh1.2trilioni, hivyo kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti yake ya mwaka 2011/12.
Hata hivyo, taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini zinaonyesha kuwakuna mgawo mkubwa wa umeme na jana Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za hali hiyo, lakini hadi jioni maelezo hayo hayakutolewa.
Agizo la Makinda lililitokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, aliyetaka Bunge kuahirisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ili kujadili jambo la dharura la kukatika umeme sehemu nyingi nchini.
Wenje alisema kwa mujibu wa taarifa alizopata, jiji la Mwanza halikuwa na umeme siku nne mfululizo hadi jana na maeneo mengine ya Kigoma, Arusha, Dar es Salaam na Mbeya hali ilikuwa hivyohivyo.
“Mheshimiwa Spika, natumia Kanuni ya 47(1), inayosema baada ya muda wa maswali kwisha, mbunge yeyote anaweza kutoa hoja kuwa shughuli za Bunge kama zilivyoonyeshwa kwenye orodha ya shughuli, ziahirishwe ili Bunge lijadili jambo halisi la dharura na la muhimu kwa umma,” alisema Wenje na kuongeza:
“Kifungu kidogo cha pili kinasema hoja ya namna hiyo itakuwa na ni maalum na inaweza kutolewa wakati wowote hata kama majadiliano yatakuwa yanaendelea”.
Wenje alihoji sababu zilizofanya nchi kuwa gizani, akisisitiza kwamba, hali hiyo inachangia kukwama kwa shughuli za kiuchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla.
“Hali ni mbaya, Mwanza hakuna umeme na mji mzima, sasa nasikia hata maji hakuna kwa sababu mashine za kusukuma maji zinategemea umeme, shughuli za watu zimesimama, watu wanalala njaa maana hata mashine za kusaga nafaka zimesimama. hii ni dharura, naomba kutoa hoja,” alisema Wenje, huku hoja yake ikiungwa mkono na wabunge wengi.
Mbunge huyo alisema uhaba wa umeme unatia shaka kwani katika muda wa wiki mbili ambazo Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa ikisubiri kupitishwa kwa bajeti yake bungeni (baada ya kukwama awali), hakukuwa na tatizo hilo.
Kauli ya Spika
Baada ya Wenje kutoa hoja hiyo, Spika Makinda alisimama na kuitaka Serikali kuwasilisha maelezo bungeni hivyo kuruhusu mjadala wa Maliasili na Utalii kuendelea.
“Kanuni hiyohiyo uliyoitumia, kipengele cha nne kinasema hivi, …. iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura, halisi na lina maslahi kwa umma, basi ataruhusu hoja hiyo itolewe,” alisema Makinda na kuongeza: “Sasa kwa sababu hii naiagiza Serikali ilete maelezo yake hapa bungeni”.
Wakati Spika akiahirisha Bunge baada ya kikao cha jana asubuhi, alisema maelezo kuhusu dharura ya umeme kutoka Serikalini yangetolewa katika kikao cha jioni, kabla ya Waziri wa Maliasi na Utalii, Ezekiel Maige kuhitimisha hoja yake.
Hata hivyo, maelezo hayo hayakutolewa na hakukuwa na taarifa zozote kuhusu sababu za kutotolewa kwa maelezo hayo jana.Habari ambazo Mwananchi lilizipata zinasema kuwa kurejea kwa mgawo mkali wa umeme, kunatokana na msukumo mdogo wa gesi kutoka katika kisiwa cha Songosongo, wilayani Kilwa na uhaba wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL.
“Hapa kuna matatizo mawili, kwanza tunaambiwa kwamba, msukumo wa gesi kutoka Songosongo ni mdogo hivyo mitambo ya gesi haifanyi kazi vizuri. Pili, tumepewa taarifa kwamba, IPTL kuna tatizo la mafuta, hivyo mitambo inayozalisha umeme ni nusu tu,” kilisema chanzo chetu ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Lukuvi atamba
Lakini jana jioni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi alisema Serikali ilikuwa tayari na ipo tayari kutoa maelezo hayo muda wowote ikipewa nafasi.
Waziri Lukuvi alisema jana jioni kuwa Serikali ilikuwa tayari kufanya hivyo, lakini muda haukuwepo kutokana na kuendelea kwa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambao ulikuwa ukihitimishwa.
Mpango wa dharura
Katika mpango wa dharura ambao Bunge liliupitisha mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Ngeleja alisema kuna mpango wa kuanzia sasa hadi Desemba mwaka huu ambao Serikali itatumia Sh408 bilioni kuufanikisha. Alisema Serikali itakopa fedha hizo kwenye benki za hapa nchini.
Waziri Ngeleja alisema mbali na mpango huo, mpango mwingine wa hadi Desemba unatarajiwa kutumia takriban Sh800 bilioni hivyo kuufanya mpango mzima kwa kukabiliana na mgawo wa umeme kufikia Sh1.2trilioni.
Alisema, hadi wiki jana IPTL ilikuwa ikizalisha kwa uwezo wake wote wa megawati za umeme 100 na kwamba ndiyo ilikuwa imepunguza athari za mgawo wa awali.Hata hivyo, waziri Ngeleja aambaye jana jioni hakuwepo bungeni, alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokewa.Alipotafutwa Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud, simu yake pia ilikuwa ikiita bila majibu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment