TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, August 19, 2011

Tegete, Nsajigwa wavamia gari la Mwananchi na Kufanya Fujo

Nahodha wa timu ya Tanzania,Taifa Stars na Yanga Shadrack Nsajigwa pamoja na mshambuliaji Jerry Tegete(aliyevaa jezi ya njano) wakifanya vurugu ndani ya Gari la Waandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi muda mfupi baada ya mechi kumalizika.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wachezaji wa Yanga, Jerryson Tegete, nahodha Shadrack Nsajigwa na Nadir Haroub baada ya kumalizika kwa mechi ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Simba iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam walivamia gari la Waandishi wa habari wa Mwananchi lililokuwa katika foleni ya kutoka uwanjani humo na kuanza kufanya fujo.

Tegete alifanya vurugu hizo baada ya kuambiwa na mtu asiyekuwa mwandishi wa gazeti la Mwananchi kwamba wamefungwa 2-0, lakini kwa sababu mtu huyo alikuwa ndani ya gari la Mwananchi, mshambuliaji huyoalishuka kutoka kwenye basi la Yanga na kupiga kwa nguvu kioo cha nyuma cha basi la Mwananchi kabla ya kufungua mlango wa gari na kuingia ndani ya gari la Mwananchi.


Mshambuliaji huyo alikuwa akifuatana na nahodha wake Shadrack Nsajigwa aliyekuwa akimzuia, lakini Tegete alianza kufanya fujo kwa kumshambulia mtu huyo aliyekuwa ndani ya basi hilo pamoja na waandishi wa Mwananchi na waandishi wengine wa habari.

Mpiga picha wa gazeti hili, alipojaribu kumpiga picha Tegete wakati akifanya fujo Nsajigwa akataka kumnyang'anya kamera mpiga picha ili asipige tukio hilo, hali iliyosababisha kuhamasisha vurugu kwa mashabiki waliokuwapo kutaka kupora kamera, kompyuta na simu za waandishi zilizokuwapo kwenye gari.

Wakati Tegete na Nsajigwa wakifanya fujo hizo Haroub 'Canavaro', alitumia mwanya wa dereva wa Mwananchi aliyekuwa ameshuka kukagua gari kama limevunjwa kioo na yeye kukaa kwenye kiti cha dereva huku akijaribu kuwasha gari hilo, lakini jitihada zake Nadir ziligonga mwamba baada ya mwandishi Jackson Odoyo wa Mwananchi aliyekuwa kwenye kiti cha mbele kung'ang'ania funguo na kumkamata mikono mpaka dereva aliporejea na kuuchukua ufunguo huo.

Hata hivyo; katika fujo hizo mwandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo aliyekuwa ndani ya gari la Mwananchi, Julius Kihampa alipoteza simu yake ya kiganjani aina ya Nokia.

Katika hatua nyingine mashabiki wa Yanga Bombaa juzi usiku walimvunja mkono mwanachama wa Simba, Salum Cheusi aliyekuwa akisheherekea ushindi wa timu yake.

Cheusi alijikuta matatizoni baada ya songombingo kuibuka uwanjani kati ya wanachama wa Yanga na Simba waliokuwa wakilinda uwanja wa Taifa wakihofia kufanyiwa vitendo vya ushirikina.

Mbali na Cheusi mwanachama mwingine wa Simba anayefahamika kwa jina la Macho pia alijikuta akipewa kipigo kilichosababisha achanike mdomo kwa madai kuwa amekuwa akiihujumu Simba kwa kutoa taarifa za kila kinachoendelea ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Macho alisema, "Kuna wataalum waliletwa na mzee ...(jina limeifadhiwa) kutoka Zanzibar na walinzi walipewa shilingi 300,000 ili wawaruhusu kuingia uwanjani na fedha hizo mimi ndio nilipewa niwape,"alisema mwanachama huyo.

"Tulikuwa kundi la watu 30 sikupigwa na wanachama wa Simba nilipigwa na Yanga bomba wakiongozwa na Shamte Mkumba, nilipigwa nikiwa naongea na simu nikipokea maelekezo kutoka kwa mzee kuhusu wataalamu wetu.

"Ilikuwa ni saa saba usiku walimpiga Cheusi na kumvunja mkono hata kesho utamuona amevaa P.O.P, lakini masuala yote haya viongozi wameshayamaliza."

No comments: