Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza moja ya vikao vya kamati kuu ya CCM.
CC kuketi leo, vigogo matumbo joto
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo inaketi katika kikao chake cha kawaida huku wajumbe na makada wa chama hicho wakijawa na hofu ya kuadhibiwa kwa sababu mbalimbali huku ajenda za kikao hicho zikifanywa siri.
Blog hii ya hekima imedokezwa hofu hiyo inatokana na kuwapo kwa taarifa kuwa Kamati ya Maadili na Usalama iliyoketi jana, ilitoa pendekezo la kuwakanya na kuwashughulikia wanachama wote waliokaidi amri ya kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya kushambuliana hadharani.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Maadili na Usalama, amebainisha kuwa Kamati Kuu (CC), itajadili kauli za viongozi wa juu wa chama hicho kuhusu dhana ya kujivua gamba ambayo inadaiwa imekuwa ikipotoshwa kwa lengo la kuwakandamiza baadhi ya wanasiasa kwa malengo fulani.
Hata hivyo blog hii ilidokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wanataka viongozi wote waliopotosha dhana ya kujivua gamba wawajibishwe kulingana na taratibu za chama ili kurejesha umoja, amani na mshikamano ambao hivi sasa umedorora.
Habari zinasema miongoni mwa wanasiasa wanaokabiliwa na shinikizo hilo la kuhojiwa kutokana na kauli zao ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamisi, Mgeja na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.
Hivi karibuni Sitta, akiwa mkoani Mbeya alisema mgawo wa umeme uliopo hivi sasa hapa nchini unasababishwa na serikali, hivyo akasema serikali ilikuwa ikipaswa kuwaomba radhi wananchi kwa kosa hilo, huku akiwataka Watanzania kuwahoji viongozi wao.
Matamshi hayo yalipingwa vikali na Mgeja na Guninita ambao walisema kiongozi huyo ana ajenda ya kuibomoa CCM na kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, amfukuze kwenye baraza la mawaziri.
Wenyeviti hao walisema Sitta anaingia katika vikao vya baraza la mawaziri hivyo hapaswi kumshambulia waziri mwenzake, bali alitakiwa kutoa ushauri wa kuboresha upatikanaji wa umeme katika vikao husika.
kikao hicho cha CC pia kitaweka mikakati ya kuhakikisha Jimbo la Igunga linabakia mikononi mwa chama hicho baada ya kada wake, Rostam Aziz, kujiuzulu kwa kile alichodai ni kuchoshwa na siasa uchwara zinazofanywa dhidi yake.
Rostam aliwatuhumu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, Naibu Katibu Mkuu, John Chiligati na viongozi wengine kwa kumtaja yeye kuwa ni miongoni mwa magamba yanayopaswa kuvuliwa ndani ya chama hicho.
Habari zinaeleza kwamba, kujiuzulu kwa Rostam kunaweza kukawa ajenda ya kwanza na muhimu katika kikao hicho ambacho kinaweza kikalazimika kujadili mbinu zitakazokiwezesha chama hicho kuendelea kuongoza Jimbo la Igunga.
Vyanzo kadhaa vya kuaminika kutoka ndani ya chama hicho tawala, vimekuwa vikieleza kuwa kuanguka kwa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Igunga kunaweza kukatajwa kuwa ni kielelezo cha kwanza cha kushindwa kwa dhana ya kujivua gamba iliyoasisiwa na Rais Kikwete mwenyewe na kupigiwa chapuo kubwa na viongozi wa sekretarieti ya chama hicho wakiongozwa na Nape.
Blog hii iliwasiliana na Nape kuhusu ajenda za kikao hicho cha CC, kitakachofanyika leo, ambapo alisema ni siri.
Nape alisema kuwa hawakupenda kuziweka wazi ajenda za kikao hicho kwa sababu maalumu lakini amekuwa akishangazwa na maneno ya mitaani yanayozitaja ajenda zitakazojadiliwa.
“Ndugu yangu sisi hatujatoa taarifa kuhusu ajenda tutakazozijadili leo lakini kila kukicha nimekuwa nikisoma habari na kusikia mitaani kuhusu tunachodajili leo, sijui wenzangu wamezipata wapi?” alihoji.
Alisema hawakuona sababu ya kuzitaja ajenda za kikao hicho kama wanavyofanya kwa sababu wangependa kuwapo na usiri wa kile watakachokijadili.
No comments:
Post a Comment