Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete (katikati) akiwa na katibu mkuu wa chama hicho. Willson Mukama (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzannia Zanzibar, Aman Abeid Karume wakati wa ufunguzi wa kamati kuu ya chama hicho mjini Dododma jana
KAMATI Kuu ya CCM, (CC) jana ilikutana mjini Dodoma huku mpango mkakati wa kujivua gamba na uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga mkoani Tabora, zikiwa ni agenda moto katika kikao hicho kilichoketi chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo wa CC umefanyika kipindi ambacho chama hicho tawala, kimepigwa na mawimbi mazito ya kisiasa kutokana na mpango huo wa kujivua gamba, ambao unaungwa mkono na baadhi ya makada wa chama hicho huku wengine wakipinga jinsi unavyotekelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya ndani, kikao cha jana ambacho kilitanguliwa na Kamati ya Maadili iliyokutana juzi, pamoja na ajenda nyingine kilijikita zaidi katika mpango mkakati huo wa kujivua gamba.
Hata hivyo hadi jana jioni Katibu wa Itikadi na Uenezi mwenye dhamana ya kueleza umma ajenda sahihi zilizojadiliwa alikwepa jukumu hilo huku akidai kutofahamu chochote ambapo alirudia kauli aliyoitoa juzi kwamba, "ajenda hazijapangwa."
Lakini kauli hiyo ya Nape ambayo haikuwa na nguvu za kimantiki kwa kuwa kikao kilishaanza na kisingeweza kuendelea bila ajenda kuwapo.
Kadhalika kauli hiyo ya Nape ilitofautiana na vyanzo vingine ndani ya kikao hicho ambavyo vilifafanua zaidi kwamba katika sehemu ya kwanza ya kikao hicho “kuliibuka mvutano mkali” kuhusu utekelezaji wa mpango huo wa kujivua gamba ambao wapo waliotaka utejelezwe lakini wengine wakipinga.
Blog hii ilidokezwa zaidi kwamba, kundi linalopinga linaona utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya kuendeleza mpasuko ndani ya chama kwani wanaotakiwa kuchukuliwa hatua nao wana wafuasi wao.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa hizo, wajumbe waliounga mkono utekelezaji wa mpango huo walijenga hoja kwamba ni hatua muhimu kwa chama kujisafisha ili kiweze kusonga mbele kwani hatua ya kurudi nyuma ingeweza kuwa na athari kubwa zaidi.
Chanzo hicho kilifafanua zaidi kwamba, hadi jana majira ya saa 10:00 jioni wakati wajumbe walipokwenda mapumziko, haikuwa imepatikana suluhu ya makubaliano ya pamoja kuhusu kujivua gamba ili yaweze kuwasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (Nec).
Nec ya CCM iliyoketi mwezi Apirili ndiyo ilitoa azimio la kuwataka watuhumiwa wote wa ufisadi ikiwemo Rada, wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT) wenye uhusiano na Kampuni ya Kagoda Agriculture na Richmond, wajiuzulu nyadhifa zao kabla ya utekelezaji wa mpango huo wa kujivua gamba.
Tayari aliyekuwa mbunge wa Igunga Rostam Aziz, alikwishafanya uamuzi wa kuachia nafasi zake zote na kwenda mbali zaidi hadi ubunge lakini mwenyewe, akipinga kwamba uamuzi huo ni sehemu ya kujivua gamba.
Mbali ya ajenda ya gamba, ajenda nyingine ilikuwa ni namna ya kuweka mikakati ya kushinda uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga liliachwa wazi na Rostam, ambalo linatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na wapinzani nao kujipanga kulitwaa.
Ajenda ya tatu kwa mujibu wa chanzo hicho, ni bajeti ya chama kwa mwaka
huo wa 2011/12 kama ilivyo bajeti kuu ya serikali kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi.
Kikao hicho kilianza mnamo takriban saa 6 mchana na kwenda hadi muda huo wa jioni na kuatarajiwa kwenda hadi usiku kutegemea mjadala wa ajenda ambavyo ungekwenda.
Hadi ilipofika mchana, Nape aliwaambia waandishi, “Kwa sasa sina cha kuwapa kwa kuwa kikao bado kinaendelea na hata kama mngenitaka niseme nini kilichozungumzwa siwezi kuwaambia,’’alisema Nape na kuongeza:
“Lakini naomba muamini kuwa kikao hiki ni lazima kiishe leo kwa muda wowote na katika kipindi hicho nitatoa taarifa kwenu kwa kuwa nimewaambia wajumbe wangu wawe wanaandaa taarifa hiyo hatua kwa hatua hivyo msitoke hapa kwa kuwa zege halilali."
Malecela kivutio
Katika hatua nyinginem, Mwanasiasa mkongwe, kada na Waziri Mkuu Mstaafu John Malecelea, jana alikuwa kivutio kwenye kikao hicho cha CC baada ya kuonekana akisamiliana na wajumbe wengi ambao walimtakia pole ya homa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Malecela kuonekana kwenye vikao tangu augue na kupelekwa nchini India ambako alifanyiwa upasuaji wa moyo mwezi uliopita. Taarifa za ugonjwa wa Malecela zilitangazwa bungeni na Spika Anne Makinda.
Jana, mkongwe huyo katika medani ya siasa, aliingia ukumbini akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete huku akionekana mwenye afya njema. Aliingia na kwenda moja kwa moja kukaa karibu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati.
Katika mkutano wa jana, Katibu Mkuu wa CCM Willson Mukama alisema kuwa wajumbe 33 walikuwa wamehudhuria katika kikao hicho idadi ambayo inakipa uhalali kikao hicho kufanyika.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa taarifa kuwa wajumbe waliotakiwa kuhudhuria humu ndani ni wajumbe 39, lakini hadi sasa jumla ya wajumbe 33 wamekwisha hudhuria na hivyo kikao hiki ni halali,’’alisema Mukama akimkaribisha Mwenyekiti kufungua Mkutano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Mukama kwa Vyombo vya habari, kikao hicho pamoja na mambo mengine kilitarajia kupokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya Halmashauri Kuu ya April mwaka huu.
Miongoni mwa wajumbe waliohudhuria jana ni pamoja na Mzee Alli Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Aman Abeid Karume, Rais wa sasa wa Zanzibar Dk Ally Mohamed Shein, Makamu wa Rais Dk Mohamed Ghalib Bilali pamoja na viongozi waandamizi ndani ya chama hicho, akiwemo Makamu mwenyekiti Pius Msekwa.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa hakuwemo kwenye chumba cha mkutano wakati wa ufunguzi na hata mchana hakuonekana katika eneo la makao makuu ya CCM Dodoma hali inayoashiria kwamba hakuhudhuria mkutano huo.Hata hivyo hakuna taarifa yoyote rasmi ambayo ilitolewa kuhusu kutokuwepo kwa mtangulizi huyo wa Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment