HOTUBA YA MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB), MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA MAMBO YA NDANI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012.
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya umma wa Watanzania, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo hapa leo, kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi rasmi ya Upinzani, kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa mujibu wa kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, natoa pia shukurani zangu za dhati kwa familia yangu, Mke wangu Neema Lema, watoto wangu, Allbless Lema na Brilliant Lema, na wazazi wangu wote, Mzee Elibariki Jonathan Lema na Mama .
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Arusha Mjini kwa imani yao kwangu. Licha ya vitisho, vipigo na mabomu ya machozi yaliyotawala kampeni na hata siku ya kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo, wananchi wa Arusha waliendeleza msimamo wao wa kutetea haki kwa kulinda kura zao kwa ujasiri wa hali ya juu. Kwa ujasiri wao, kwa uvumilivu wao, na kwa kujitolea kwao, wananchi hawa wameendelea kutukumbusha kuwa: “Ni heri ya vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu.”
Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, Naibu wake Mhe. Kabwe Zuberi Zitto, na Mnadhimu Mkuu Mhe. Tundu Antiphas Mughwai Lissu, kwa kutambua uwezo wangu na kunipa dhamana ya kuwa Waziri Kivuli wa Wizara hii nyeti ya Mambo ya Ndani
.Mheshimiwa Spika, nawashukuru wanachama, viongozi wa ngazi mbali mbali na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) popote pale walipo ndani na nje ya Tanzania kwa kutuunga mkono wakati wote wa harakati za kudai haki katika siku ngumu na za hatari zilizofuatia uchaguzi batili wa Meya wa Jiji la Arusha. Msimamo wao umeendelea kututia nguvu na ujasiri hata katika kipindi hiki ambacho kuna dalili za baadhi yetu kutetereka katika mapambano yetu ya kudai haki.
Mheshimiwa Spika, Mwanafalsafa maarufu wa Kiyahudi Elie Wiesel alisema, “there may be times when we are powerless to prevent injustice, but there must never be a time when we fail to protest.” Kwa Kiswahili, “kuna nyakati tunaweza kuwa wadhaifu katika kuzuia uovu na dhuluma, lakini kamwe isijetokea wakati ambapo tutashindwa kupinga uovu na dhuluma.” Pengine tulikuwa dhaifu kudhibiti hujuma na dhuluma tulizofanyiwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita, lakini kamwe hatutakuwa tayari kuhujumiwa katika uchaguzi wowote ujao, ukiwemo wa Jimbo la Igunga.
HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika, dira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kutoa huduma bora katika kudumisha amani, utulivu na umoja nchini. Katika kutekeleza dira hiyo, Wizara imeweka dhima ya kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi wanaotuhumiwa kwa uhalifu na kuwarekebisha wafungwa, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini wa raia na wageni, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji na kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini.
Mheshimiwa Spika, licha ya maneno mazuri ya dira na dhima hiyo, hali ya usalama wa raia na mali zao katika nchi yetu ni mbaya. Vile vile, mfumo mzima wa kimagereza umekuwa wa kutesa na kudhalilisha zaidi wafungwa na watuhumiwa wa uhalifu kuliko kuwahifadhi na kuwarekebisha; Mfumo wa uhamiaji umekuwa dhaifu kuruhusu wageni haramu badala ya kuwadhibiti; Na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kimekuwa cha kushuhudia matukio ya moto badala ya kuyazuia na kuyadhibiti!
Mheshimiwa Spika,Mpigania haki za watu weusi wa nchini Marekani, Hayati Dr. Martin Luther King, Jr. aliwahi kusema kwamba “peace is not the absence of war but merely the presence of Justice”, yaani “amani si hali ya kutokuwepo vita, bali ni uwepo wa haki”. Kwa kipimo hiki cha amani, nchi yetu haina amani kama viongozi wa serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanavyodai kila mara. Hii ni kwa sababu, licha ya ukweli kwamba Tanzania hakuna vita, pia ni dhahiri Tanzania sio nchi ya haki. Nathibitisha;
MAUAJI YA RAIA WASIO NA HATIA
Mheshimiwa Spika, wakati viongozi wa serikali yetu na wapambe wao wakidai majukwaani, na kwa sauti kubwa, kwamba Tanzania ni nchi ya amani na utulivu, serikali hiyo hiyo kwa kutumia Jeshi lake la Polisi na vyombo vingine vya usalama imekuwa mstari wa mbele kuua raia wasiokuwa na hatia wanapodai haki zao.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii inayohubiri amani kila kukicha, kwa kutumia vyombo vyake vya mabavu, imekuwa inakamata wananchi wasiokuwa na hatia na kuwabambikizia kesi za uwongo pale wanaposhindwa kutoa rushwa katika vituo vya polisi na mahakamani. Watawala hawa, wanaopenda kujidai kwamba mamlaka yao imetoka kwa Mungu na kwa hiyo iheshimiwe, wamekuwa wanatesa wananchi wetu katika vituo vya polisi na magerezani kinyume na sheria za Tanzania na hata za kimataifa.
Mheshimiwa Spika, licha ya maovu yote haya wanayotendewa, Watanzania hawajachukua silaha kujitetea. Hata hivyo, ‘utulivu’ huu hauwezi kuitwa amani, maana amani si uwepo wa ukatili bali ni uwepo wa haki kama tafsiri sahihi ya Dr. Martin Luther King, Jr ilivyosema
Mheshimiwa Spika, Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), imeeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2010 peke yake, watu 52 walikufa wakiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama. Kati ya wote waliouawa, watu 10 waliuawa na Jeshi la Polisi katika maeneo ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Nyamongo wilayani Tarime peke yake.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2011, tayari Watanzania 21 wameuawa kwa kupigwa risasi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na wengine wengi kuumizwa. Kati ya hao, watu 9 wameripotiwa kuuawa na Jeshi la Polisi katika maeneo yanayozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara peke yake. Vile vile, watu watatu waliuawa katika Jiji la Arusha wakati polisi walipovamia maandamano ya amani kupinga uchaguzi batili wa meya wa Jiji hilo.
Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha zaidi, wilayani Tarime Watanzania walishuhudia Jeshi la Polisi likitumia giza la usiku kuiba maiti za marehemu lililowaua na baadae kuwatelekeza barabarani na kukimbia. Sasa tunadhihakiwa na watu wengine duniani kwa kuwa na Jeshi la Polisi linaloiba maiti badala ya kulinda uhai wa raia na mali zao!
Mheshimiwa Spika, mbali na ripoti kuhusu ukiukwaji mkubwa Haki za Binadamu, zilizotolewa na taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kiserikali kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Tanzania (CHRAGG) pia zimethibitisha jinsi vyombo vya dola vya nchi hii vilivyo katili. Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka 2002/03 iliyochapishwa mwezi Mei 2005, ilisema kwamba malalamiko mengi iliyoyapokea yalihusu polisi kubambikizia raia kesi, mahabusu kutopelekwa mahakamani kama taratibu zinavyotaka, watuhumiwa kupigwa na kuteswa wakati wa kuhojiwa na upelelezi hasa wa kesi za mauaji kuchukua muda mrefu
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatoa haki ya kuishi kwa kila mtu na inaitaka Serikali kumpatia kila mtu hifadhi ya maisha yake. Vile vile, vifungu vya 195 na 196 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania vinakataza vitendo vya mauaji vilivyo kinyume na sheria. Kwa mujibu wa ibara ya 30(2)(c) ya Katiba, mauaji yanaweza kuwa halali endapo yamefanywa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa kwa ajili ya “... kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la ... jinai.”
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, mauaji yanayofanyika ili kutekeleza adhabu ya kifo inayokuwa imetolewa na mahakama kwa kosa la mauaji chini ya kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu ni mauaji halali kwa mujibu wa sheria zetu. Kinyume kabisa cha sheria hiyo, mauaji yote ambayo yamekuwa yakifanywa na Jeshi la Polisi hayajawahi kutokana na adhabu yoyote ya kifo iliyotolewa na mahakama za Tanzania na kwa hiyo ni mauaji haramu.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania, kifo chochote ambacho kimetokea katika mazingira ya mashaka kinatakiwa kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria hiyo. Hatua ya kwanza ya uchunguzi wa kifo cha aina hiyo, kwa mujibu wa sheria hiyo, ni uchunguzi wa kidaktari (autopsy) ili kubainisha sababu halisi ya kifo hicho. Aidha, hatua ya pili ni uchunguzi wa kimahakama – kwa kutumia mahakama ya korona – ili kujiridhisha kwamba kifo hicho hakijatokana na matendo au sababu za kijinai.
Mheshimiwa Spika, katika matukio yote ya mauaji yanayolihusisha Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vya Tanzania, utaratibu huu wa kisheria haujawahi kufuatwa. Aidha, ukiachia matukio ya mauaji yaliyomhusisha aliyekuwa Afisa Upelelezi wa Jinai wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake ambao hata hivyo waliachiwa huru, matukio mengine yote ya mauaji hayajawahi kuchunguzwa na wahusika kufikishwa mahakamani. Huu ni ushahidi tosha kuwa serikali yetu kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vyake vingine vya usalama imekuwa ikiua wananchi wasio na hatia.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa ukiukwaji huu mkubwa wa haki za binadamu unafanyika kutekeleza sera isiyo rasmi ya Serikali ya Tanzania. Ndio maana, licha ya Katiba yetu kukataza vitendo hivyo, mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo vya dola pamoja na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu hayapungui badala yake yanaongezeka kila mwaka. Na ndio maana Serikali haijawahi kuchukua hatua yoyote kuhakikisha mauaji haya yanachunguzwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo na wala kuhakikisha wahusika wa mauaji haya wanachukuliwa hatua za kisheria au za kinidhamu pamoja na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu. Uthibitisho mkubwa zaidi,
Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali ya Tanzania haijawahi kuleta kwenye Bunge hili tukufu Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Utesaji na Matendo au Adhabu Nyingine za Kinyama, Zinazotweza na Kudhalilisha wa mwaka 1984 (the UN Convention Against Torture and Other Cruel, Inhuman or Degrading Treatment or Punishment, 1984) uliopitishwa na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 39/49 la tarehe 10 Desemba 1984 na kuanza kutumika mwaka 1987.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayoruhusu vyombo vyake vya usalama kufanya mauaji kinyume na sheria dhidi ya raia wasiokuwa na hatia; Serikali inayoruhusu vyombo vyake vya usalama kutesa raia wake kwa namna za kinyama kama zinazoelezwa katika taarifa za taasisi za haki za binadamu; Serikali ya aina hiyo inapoteza uhalali wake machoni mwa wananchi wake na mbele ya macho ya dunia.
Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo, wananchi wanakuwa na haki ya kupinga udhalimu na ukandamizaji huo. Uhamasishaji wa upinzani dhidi ya serikali ya aina hiyo unakuwa ni wajibu wa kila mzalendo wa kweli. Kama alivyosema Frederick Douglass zaidi ya miaka 150 iliyopita, “he is a lover of his country who rebukes rather justify its sins”, yaani, “mpenzi wa nchi ni yule anayekemea madhambi ya nchi yake, badala ya kuyahalalisha”!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi kwa nini matukio yote ya mauaji ya raia yaliyo kinyume na sheria hayajawahi kuchunguzwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo; Na kwa nini hakuna hata mhusika mmoja ambaye amewahi kuchukuliwa hatua za kisheria au za kinidhamu kwa kuhusika kwao na mauaji haya.
Mheshimiwa Spika, pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania kwa nini inakwepa kuridhia Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Utesaji na Matendo au Adhabu Nyingine za Kinyama, Zinazotweza na Kudhalilisha kwa karibu miaka thelathini tangu Mkataba huo upitishwe na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na karibu robo karne tangu uanze kutumika!
Mheshimiwa Spika, mifano hiyo michache inaonyesha kuwa nchi hii haina amani ya kweli. Kilichopo si amani, bali utulivu unaojengwa na nidhamu ya woga. Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inatahadhirisha kuwa utulivu wa nchi hii upo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu kuu mbili; Kwanza, ni kuongezeka kwa matabaka baina ya Watanzania wengi walio maskini na wasiotendewa haki, na tabaka la Watanzaniawachache matajiri na wawekezaji wanaopata zaidi haki kwa sababu ya uwezo wao wa kifedha. Iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa, basi dalili zipo wazi kuwa uvumilivu wa Watanzania wengi maskini sasa umefika mwisho na lolote linaweza kutokea.
Mheshimiwa Spika, pili, amani ya nchi hii ipo hatarini kutoweka kabisa kwa sababu ya mtazamo potofu wa serikali yetu wa kuamini kuwa njia sahihi ya kudumisha amani ni kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwafyatulia wananchi risasi, mabomu ya machozi na kuwapiga kwa virungu. Hata hivyo, sasa wananchi wameanza kuzoea hali hiyo na ni dalili mbaya kwa utawala. Ni lazima serikali ikaelewa kuwa umma wa Watanzania milioni 40 kamwe hauwezi kusambaratishwa kwa risasi za Jeshi la Polisi, ambao idadi yao ni takribani 50,000.
Mheshimiwa Spika, ukweli kwamba majeshi ya nchi yoyote duniani hayawezi kushindana na haki, ukweli na utu unaopiganiwa na nguvu ya umma, tayari umeshadhihirika sehemu mbalimbali duniani, kabla na baada ya uhuru wa nchi hii. Mfano mzuri ni nchi ya Afrika Kusini, Msumbiji, Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, na Sudan ya Kusini, ambayo imepata uhuru hivi karibuni. Aidha, hivi karibuni wananchi waliochoka kunyanyaswa katika nchi za Misri, Tunisia, Yemen, Bahrain, Libya na hivi sasa jirani zetu wa karibu kabisa Malawi, wameanza na bado wanaendelea na vuguvugu la kudai haki zao bila kuhofia majeshi na silaha nzito za kivita.
Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote inayopuuza haki na utu, na kufikiri kwamba kuongeza idadi na vifaa vya kijeshi ndiyo suluhisho la amani na utulivu, ni serkali yenye viongozi waliopotoka. Kambi rasmi ya Upinzani kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania, inachukua fursa hii kuionya serikali hii inayoongozwa na CCM, kwamba amani ya nchi hii kamwe haiwezi kulindwa na FFU wala majeshi, bali italindwa kwa kuhakikisha haki inatendeka na utu wa Mtanzania unaheshimiwa, tena bila kuwepo kwa matabaka ya kinyonyaji dhidi ya Watanzania wengi maskini.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anahitimisha mjadala kuhusu bajeti ya Ofisi yake, alikubaliana na ushauri wa Kambi rasmi ya Upinzani, na kuahidi kwamba serikali itaanzisha mahakama ya kuchunguza mauaji hayo, yaani “Coroner’s Court”, kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, (The Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inachotaka sasa ni kuona utekelezaji; Je, ni lini Waziri mwenye dhamana atatangazauteuzi wa kuundwa kwa mahakama hiyo katika Gazeti la Serikali, ili wauaji wahukumiwe? Tunataka uchunguzi ufanyike haraka ili haki iwe itendeke mapema.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa mbali na kuwabaini polisi waliohusika na mauaji hayo, pia uchunguzi huo uhakikishe serikali inatekeleza yafuatayo;
1. Ilipe Fidia stahili kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na/au jamaa wa wale wote waliouawa kutokana na vitendo vya Jeshi la Polisi la Tanzania na kwa wale wote walioumizwa kwa namna yoyote ile na/au kuharibiwa mali zao kutokana na vitendo hivyo;
2. Iwachukulie hatua kali za kinidhamu na kisheria askari Polisi wote, wakiwemo askari Magereza na wale wa Wanyamapori ambao wamehusika katika mauaji haya tuliyoyabainisha katika hotuba hii na kwenye hotuba iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Mhe. Freeman Mbowe; Vinginevyo, hali hii ikiachwa iendelee kama ilivyo sasa ni hatari kwa usalama wa Watanzania.
AJALI ZA BARABARANI
Mheshimiwa Spika, mbali na mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi, pia Watanzania wengi wamekuwa wakipoteza maisha na kupata vilema vya maisha, kwa sababu ya kukithiri kwa ajali za barabarani. Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa ajali za barabarani ziliongezeka kutoka 22,019 mwaka 2009 hadi 24,926 mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika, katika ajali hizo watu 3,689 walifariki na wengine 22,064 walijeruhiwa. Kiasi hiki ni kikubwa sana kwani ni sawa na ajali 68 kwa kila siku. Hii ni sawa na kusema Watanzania 10 hufariki kila siku kutokana na ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na uzembe na rushwa, baina ya wadau wa barabara na Jeshi la Polisi kitengo cha barabara (Traffic).Mathalan, ukaguzi wa magari siku hizi umekuwa ukilenga zaidi kuuza stika za nenda kwa usalama, badala ya kukagua hali halisi magari. Ni aibu kwa serikali kubakia kutuma salamu za rambi rambi vifo vya ajali vinapotokea, badala ya kuchukua hatua kali za kudhibiti uzembe.
Mheshimiwa Spika, vifo vitokanavyo na ajali vimekuwa vingi zaidi kutokana na kuongezeka kwa ajali za pikipiki. Kwa mfano, kwa mwaka 2009 ajali za pikipiki zilikuwa 3,406 , mwaka 2010 ajali hizi zilikuwa 4,363 na jumla ya watu waliokufa kutokana na ajali hizi mwaka 2010 ni 657 kutoka vifo 385 vilivyotokea mwaka 2009.Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2010, ukurasa wa 63. Kambi rasmi ya Upinzani tunataka kujua serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na wimbi hili la vifo vya vijana wetu kutokana na ajali hizi za pikipiki.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani pia inapendekeza Askari Polisi wa Usalama Barabarani waanze kupewa mafunzo maalum ya kutoa Huduma ya Kwanza, ili ajali za barabarani zinapotokea, kazi yao isiwe ni kupima nani kasababisha ajali, bali pia wawe na uelewa wa kutoa huduma za dharura za kuokoa na kusaidia majeruhi.
RUSHWA NDANI YA VYOMBO VYA USALAMA
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linanuka rushwa likilinganishwa na taasisi nyingine za serikali. Ripoti ya kiwango cha rushwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki “East Africa Bribery Index 2010” inaonyesha kuwa jeshi la polisi limeshika namba moja kwa rushwa hapa nchini kwa mwaka 2010 kwa kupata asilimia 65.1 kati ya taasisi nyingine za umma hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Rushwa hii imekuwa ikiwaumiza sana wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wakikosa huduma na hasa kwa kuwa hawana fedha za kuwahonga maafisa wa polisi. Hali hii imepelekea hata baadhi ya wananchi kubambikiwa kesi mbalimbali kwa makusudi kwasababu tu wanakuwa hawana fedha za hongo kwa polisi na hata wengine wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kujua jeshi la polisi haliwezi kuwatendea haki. Hivi sasa kuna msemo maarufu, “kuingia kituo cha polisi ni bure, ila kutoka ni pochi”. Hii ni aibu kubwa kwa Jeshi la Polisi na Serikali. Badala ya kuwa Jeshi la kulinda usalama wa raia na mali zao, sasa vituo vya polisi vimekuwa ni pango la kufanyia biashara ya rushwa na hongo.
Mheshimiwa Spika, rushwa pia imekithiri ndani ya vitengo vyote vya Wizara ya Mambo ya Ndani kama vile Idara ya Magereza, Kikosi cha Zimamoto, na Polisi Usalama Barabarani (Traffic). Kibaya ni kuwa rushwa hii ni ya kitaasisi, kwani hata raia wema wanapopenda kutoa taarifa kuhusiana na kuombwa rushwa hujikuta wakiwa kwenye wakati mgumu zaidi badala ya kupatiwa msaada.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa vipato vidogo, maslahi duni na maisha ya umaskini ya askari wetu wakiwemo wale wa Idara ya Magereza, vinachangia kwa kiasi kikubwa cha rushwa ndani ya Jeshi la Polisi. Pia, ukiukwaji mkubwa wa utawala wa sheria na maadili ya jeshi polisi ndio vinavyosababisha kushamiri matendo maovu na usaliti wa kweli, haki na utu ndani ya vikosi vya Jeshi la Polisi na idara zake zote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka serikali na Bunge lako tukufu kuhakikisha maslahi ya walinzi hawa wa usalama wa raia na mali zao, yanaboreshwa kwa kiwango cha kuwafanya waone kwamba raslimali wanazolinda na raia wanaowalinda, wanathamini mchango na wajibu wao. Kwa kuzingatia umuhimu wa majeshi yetu ya Usalama wa Raia, Kambi rasmi ya Upinzani inataka mishahara ya askari wetu ipandishwe ili waweze kumudu gharama zote za msingi za kimaisha.
Mheshimiwa Spika, njia nyingine ni kuhakikisha utawala wa sheria ndani ya Jeshi la Polisi unaheshimiwa kikamilifu. Badala ya kuwahamisha vituo polisi wanaotuhumiwa na makosa mbalimbali ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa, Kambi rasmi ya Upinzani, inasisitiza kuwa ni lazima utawala wa sheria uheshimiwe kikamilifu. Yeyote anayebainika kujihusisha na rushwa achukuliwe hatua kali za kinidhamu na kisheria, ili kukomesha uhalifu huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inawataka Askari polisi wote wa nchi hii, wasikubali kutumiwa vibaya kukandamiza demokrasia na haki za wananchi, kwa maslahi ya kukibeba chama fulani cha siasa na badala yake watende haki kwa manufaa ya Watanzania wenzao. Wajue kuwa Watanzania wanaowafyatulia risasi, mabomu ya machozi na kuwapiga virungu, ni Watanzania wenzao. Ni sawa na Baba zao, Mama zao, Kaka zao au wadogo zao, kwa hiyo wasikubali kutumika vibaya kuua au kukandamiza ndugu zao. Badala ya kufanya hivyo, tunawashauri waishinikize serikali hii inayowatumia vibaya, iboreshe mishahara na maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, Askari mmoja mwenye hekima wa nchini Ujerumani, wakati wa utawala wa Dikteta Adolf Hitler, aliwahi kusema, “Nilifarijika pale nilipofukuzwa kazi kwa kutokutii amri dhalimu inayokiuka haki na utu wa mwanadamu.... kwa sababu nilijua siku moja nitakufa na nitakuwa na wajibu mbele ya Mwenyezi Mungu. Nilikataa kuheshimu amri katili za wakuu wangu kazini, kwani Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko wao”. Kambi rasmi ya Upinzani, inawasihi polisi wote nchini wasikubali tena maagizo yote katili ya makamanda wao.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa malalamiko mbalimbali kuhusu ajira za polisi na maslahi yao mengine, Kambi rasmi ya Upinzani, inashauri serikali kufanya yafuatayo;i) Kuondoa utaratibu wa Askari polisi kuthibitishwa ajira yake baada ya kipindi cha miaka 12 ya sasa, na kuhakikisha ajira ya polisi inathibitishwa angalau ndani ya miaka 3.ii) Askari polisi wapandishwe vyeo kutokana na utumishi wao jeshini na vigezo viwe vya wazi, ili kuondoa malalamiko ya upendeleo.iii) Viwepo vigezo vya wazi katika kuwapanga Askari wetu kwenye vitengo mbalimbali, kwani hili linalalamikiwa sana kuwa sasa baadhi ya vitengo ni kwa ajili ya kundi fulani, huku wengine wakiwa wao ni kukaa vitengo hivyo hivyo mpaka wastaafu.iv) Ngazi za kupanda mishahara ziwe kama kwa watumishi wengine wa umma badala ya polisi wao kuwa na utaratibu wa kupanda vyeo. Pawe na vigezo ambavyo Askari akivifikia basi hata kama hajapanda cheo, basi ngazi yake ya mshahara nayo iongezeke.
Mheshimiwa Spika, hii itasaidia kuhakikisha kuwa Askari waliokaa muda mrefu wanakuwa na mishahara iliyoboreka na hata wakistaafu wanaweza kupata pensheni nzuri na hivyo kuweza kukabiliana na ukali wa maisha pindi wanapostaafu.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha zaidi utendaji wa Jeshi la Polisi na kuwatendea haki askari wetu, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja, kwani hilo si jukumu lao, ni jukumu la serikali. Kambi rasmi ya Upinzani tunatoa msimamo wa kuitaka serikali ihakikishe inawarudishia askari polisi fedha zote ilizowakata kila mwezi kwa ajili ya mazishi, kwani haikuwa halali kufanyiwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza, iwapo serikali haitawarudishia askari polisi pesa zao zote ilizowakata kila mwezi kwa madai ya kugharamia mazishi yao pindi wanapofariki, na iwapo utaratibu huu utaendelea; Kambi rasmi ya Upinzani inatangaza rasmi kwamba tutapanua ajenda yetu ya maandamano na kufanya pia maandamano nchi nzima ya kushinikiza pesa zote walizokatwa askari polisi warudishiwe na utaratibu huo ukome.
JESHI LA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika, Mwezi Mei mwaka 2010, Chama cha wanasheria wa Tanganyika (Tanganyika Law Society) walichapisha ripoti ya matokeo ya ukaguzi katika Magereza waliyoifanya katika magereza 24 mwaka 2009. Ripoti hiyo inaeleza kuwa wafungwa walifanyiwa ukatili na kuteswa wakati wakiwa mahabusu, na pia kulikuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya Dar es Salaam, Tabora, Arusha, Mara, Mwanza, na Tanga.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo pia ilidokeza kuwa katika gereza la Segerea kulikuwa na wafungwa 170 katika vyumba vya jela ambavyo vilijengwa kwa ajili ya watu 50, na katika Gereza la Ilagala mkoani Kigoma, wafungwa walilazimika kutembea zaidi ya maili 4 kwenda kuchota maji kwa sababu ya matatizo ya usafiri. Ripoti ilielezea kushindwa kwa gereza kuwapatia wafungwa huduma ya msingi ya usafi pamoja na chakula cha kutosha.
Mheshimiwa Spika, katika ripoti yake ya nusu-mwaka (2010), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kimeeleza kuwa Idara ya Magereza imetumia takriban shilingi 650 kwa siku kwa ajili ya chakula kwa wafungwa, badala ya shilingi 2,420 ambayo ilikuwa imeidhinishwa na serikali. Kwa mantiki hiyo, uhaba wa chakula magerezani hautokani na uhaba wa fedha, bali unasababishwa na ufisadi wa fedha za chakula zinazoidhinishwa na Bunge hili. Kiasi kinachoidhinishwa sicho kinachotumika, fedha nyingi inabanwa na kuingia kwenye mifuko ya watu wachache.
Mheshimiwa Spika, serikali isiyojali wafungwa ni serikali katili. Kambi rasmi ya Upinzani haiko tayari kuvumilia ufisadi na ukatili huu unaofanywa dhidi ya wanadamu wafungwa. Tunataka kujua; Je, mpaka sasa ni Watumishi wangapi wachechukuliwa hatua ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na ndani ya Idara ya Magereza, kwa kufanya mchezo huu mchafu wa kutafuna fedha za chakula cha wafungwa? Pia, tunataka kujua serikali imejizatiti vipi kuhakikisha hali hii haijirudii tena.
MRADI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, uamuzi wa kuwa na vitambulisho vya taifa ulifikiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1968, katika kikao cha Kamati ya Usalama cha Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kilichohusisha Kenya, Uganda, Zambia na Tanzania. Kwa mantiki hiyo, imepita takribani miaka 43, tangu nchi hii iamue kuwa na vitambulisho vya taifa lakini hadi leo bado havijaanza kutolewa.
Mheshimiwa Spika, hakuna lugha yoyote nzuri ya kuuzungumzia ucheleweja huu isipokuwa kusema tu, serikali yetu imefanya uzembe na haina dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wanapata vitambulisho vya taifa mapema.Pia ni vema ikazingatiwa kuwaMradi hu umechukua muda wa mwaka mmoja tangu tarehe ambayo Bodi ya Zabuni ya Wizara ilitoa idhini kwa ajili ya kazi ya ushauri na kusainiwa kwa mkataba wenyewe. Ucheleweshwaji wote huu, una athari katika kufikia na kutimiza malengo ya shughuli za mradi.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inashauri kwamba menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa iongeze juhudi katika kuongeza kasi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa kwa manufaa ya Taifa, angalau viwe tayari ifikapo mwaka 2014, ili pamoja na mambo mengine, Tume Huru ya Uchaguzi itakayoundwa, iangalie uwezekano wa kuvitumia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo katika uchaguzi mkuu uliopita lilionekana kuwa na dosari kubwa.
IDARA YA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, Idara ya zima moto ni muhimu sana kwa usalama wa raia na mali zao, pindi majanga mbalimbali yanapotokea. Hata hivyo, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika ukurasa wa 82, inathibitisha serikali haina sera ya usimamizi wa vihatarishi na namna ya kuvidhibiti. Kambi rasmi ya Upinzani inahoji, serikali inawezaje kunusuru maisha ya wananchi dhidi ya majanga kwa ufanisi, ikiwa hata sera yenyewe haipo?Kambi rasmi ya Upinzani inataka hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha vikosi hivi ambavyo vipo kwa ajili ya kusaidia jamii vinakuwepo katika kila sehemu ya nchi ili kushughulikia majanga mbalimbali yanayotokea wakati wa dharura kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, wakati hakuna ufanisi wa kutosha katika kudhibiti na kushughulikia majanga, ripoti ya Mdhibiti naMkaguzi na Mkuu wa serikali, imegundua upotevu mkubwa wa fedha za umma, kiasi cha shilingi 1,441,689,620 ambazo hazina maelezo ya kutosheleza na hivyo kusababisha hasara. Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuimarisha idara hii na pia kuwachukulia hatua waliohusika na ufisadi huu.
IDARA YA UHAMIAJI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje na limekuwa jambo la kawaida, kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini. Imeripotiwa hata kwenye vyombo vya habari kuwa Mkoani Morogoro, katika kipindi cha Desemba 2009 hadi Februari 2010, raia wa Somalia 80 wanaoishi nchini kinyume cha sheria walikamatwa na Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, kukamatwa kwa wageni hao ni uthibitisho wa namna tatizo la wahamiaji haramu lilivyo sugu na kubwa, kwani hao ni idadi ndogo tu kulingana na watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu za uhamiaji, na kuishia mitaani wakiishi na kufanya shughuli zao kama vile ni raia nchi hii. Mbali ya raia hao wa Somalia, pia wamo raia wa nchi zingine zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan, Nigeria na China, India, Bangladesh, ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake, kiusalama ni hatari, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa tatizo la ugaidi na uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu na hata ulaghai na utapeli. Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza hoja yake ya kutaka mchakato wa kupata vitambulisho vya taifa uharakishwe, kwani pia vitasaidia kuwabaini kwa urahisi wageni ambao wataingia nchini bila kuzingatia taratibu zilizopo.
WAKIMBIZI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu yameripotiwa matukio yanayotishia usalama wa raia wetu pamoja na mali zao hasa maeneo yenye wakimbizi. Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kutoa taarifa ya kina juu ya usalama wa mipaka yetu na watu wake katika maeneo hayo.Pia serikali itupe taarifa kuhusu makambi yaliyofungwa, Je, yatatumika kufanyia shughuli gani baada ya kambi hizo kufungwa?
MAPENDEKEZO YA JUMLA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, tunapenda kutoa mapendekezo yafuatayo ili kuweza kuliboresha Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji na kuyafanya yawe ya kisasa zaidi na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na za kisasa ambazo zimetokea na zinaendelea kutokea.Tunapendekeza mambo yafuatayo yaweze kufanywa kikamilifu;
(i) Ijengwe maabara ya kitaifa ya masuala ya Uhalifu (National Crime Laboratory). Hii itasaidia kupata vipimo vya kubaini uhalifu na hivyo itarahisishia kazi jeshi la polisi katika kuchunguza na kupambana na uhalifu.
(ii) Vyuo vya polisi vya Moshi, Dar Es Salaam na vile vya Magereza kama vya Ukonga na Tukuyu viimarishwe ili kuhakikisha maofisa wanaohitimu kwenye vyuo hivi wanakuwa na weledi wa kutosha katika kupambana na uhalifu unaotumia mbinu mpya na za kisasa.
(iii) Kikosi cha Uokoaji kiboreshwe kwa kupatiwa nyenzo na vifaa vya kisasa, ili kiweza kukabiliana vizuri na majanga.
(iv) Sheria ya Uhamiaji irekebishwe ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Mikoa zinakuwa na uwezo wa kutoa hati za kusafiria (Passport). Hati hizo ziwe zinapatikana kwa haraka mara baada ya maombi badala ya hali ilivyo sasa ambapo huchukua muda mrefu hadi mtu kupata Passport.
(v) Zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kununulia fulana za kuzuia risasi (bullet proof vest), ili Askari polisi wote nchini waweze kukabiliana vizuri na uhalifu mkubwa hasa ujambazi wa kutumia silaha.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba ukandamizaji na ukiukwaji wa utu na haki za binadamu, hautavumiliwa kamwe. Na ieleweke kwamba, tishio la Usalama na Amani ya Nchi hii si Maandamano ya Amani yanayofanywa na CHADEMA, kupinga uovu, bali ni ukiukwaji wa haki na utu wa Mtanzania, unaofanywa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
..............................
Godbless Lema (Mb)
Jimbo la Arusha MjiniMsemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
28/07/2011
No comments:
Post a Comment