TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, May 11, 2012

TAMKO DHIDI YA VITISHO, VIKWAZO NA VITENDO VYA VIONGOZI VINAVYOTIA WANANCHI HOFU KATIKA KUSHIRIKI MCHAKATO WA KATIBA MPYA TANZANIA

Jukwaa la Katiba Tanzania na Baraza la Katiba Zanzibar tumeendelea kufuatilia maandalizi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya ikiwa ni pamoja na kuteuliwa na kuapishwa kwa Tume ya Katiba; Hotuba mbalimbali za viongozi wa kitaifa kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya pamoja na mwitikio wa wananchi kwa ujumla. Kwanza, tunawapongeza wote walioteuliwa kulitumikia taifa letu kama wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania. Kwa maoni yetu, Tume iliyoteuliwa imesheheni watu wenye sifa, uwezo na uweledi mkubwa kiasi kwamba kama itazingatia misingi mikuu ya uundaji wa Katiba Mpya na ya Kidemokrasia inaweza kufanya kazi hiyo vizuri sana. Kwa madhumuni ya kujikumbusha, baadhi ya misingi hiyo ni ushiriki mpana wa wananchi, usikivu na ukusanyaji maoni unaozingatia uhuru kwa kila mtanzania kutoa maoni yake bila kukwazwa, kuzuiwa au kutishiwa. Aidha, tunawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha kuelekea hatua hii ya tatu ya mchakato huu wa Katiba mpya Tanzania. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kwa serikali, kupitia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza rasmi kuanza kwa Mchakato wa kuandaa Katiba Mpya Tanzania. Hatua ya pili ilikuwa ni kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Namba 8 ya Mwaka 2011 ambayo sasa imekwisharekebishwa mara moja mwezi Februari 2012. Hatua hii ya uteuzi wa Tume inaanzisha rasmi mchakato wa ukusanyaji maoni mara baada ya kuweka sawa mambo kadhaa ndani na nje ya Tume yenyewe. Pamoja na maendeleo hayo mazuri ya Mchakato huu, Jukwaa la Katiba Tanzania na Baraza la Katiba Zanzibar tumesikitishwa na kukerwa sana na matukio, matamshi na kauli mbalimbali za baadhi ya viongozi wa kitaifa wa Serikali ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama walivyonukuliwa na vyombo mbalimbali kuhusiana na ushiriki wa wananchi katika mchakato mzima wa kujipatia katiba mpya ya taifa letu. Kwetu, tunaona kuwa matukio hayo hayawezi kupita bila kukemewa kwa kuwa yanaweza kuwatia hofu na kuwaogofya Wananchi na hivyo kupunguza hamasa ya ushiriki wa wananchi katika Mchakato huu muhimu. Aidha vitisho, kukamatwa na mashitaka dhidi wananchi wanaoguswa na vitisho hivyo vya viongozi vinaweza kujenga chuki katika jamii yetu na kupelekea uvunjifu wa amani siku za usoni. Baadhi ya matukio yaliyotustua hatuna budi kuyajadili kwa undani kidogo. Kwanza, tulishtushwa na Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano aliyoitoa tarehe 13/04/2012 wakati wa kuwaapisha wajumbe wa tume ya Katiba. Kwa maneno yake Mhe. Rais alisema : “......huu siyo mchakato wa kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni Katiba ya nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo siyo referendum of the Union. Huu ni mchakato kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za Muungano Wetu. Kama una mawazo toa, sema jamani mimi nadhani hivi tunavyokwenda siyo sawa. Tukifanya hivi, tukifanya hivi, tukifanya vile, kwenye hili kwenye lile, Muungano wetu tutauimarisha na utakuwa mzuri zaidi” Kwa uchambuzi wa kawaida tu, Watanzania wamekwishapangiwa nini cha kusema wakati wa kutoa maoni na nini wasikiseme. Hivi sivyo Katiba Mpya ya kidemokrasia inavyoandikwa. Wananchi lazima waachwe watumie busara zao kujadili mambo yote wanayoona wangependa yajadiliwe kutokana na uzoefu wao na tena kwa namna wanayoona wao inafaa! Pili, tumesikitishwa sana na kauli aliyoitoa Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani akiwa bado Waziri wa Katiba na Sheria kama alivyonukuliwa akisema kuwa wananchi hawapaswi kujadili Muungano. Jukwaa la Katiba linaamini kuwa katiba bora inayotokana na wananchi itapatikana kutokana na mijadala huru na wazi yenye ushiriki mpana wa wananchi wote bila shinikizo, ubaguzi, vitisho au vipingamizi. Aidha Katiba ya watanzania itatokana na maoni ya kila Mtanzania juu ya masuala yote wanayotaka yaingie katika Katiba na si kwa kuzuia nini kisijadiliwe. Tatu, tumestushwa na kufadhaishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye alinukuliwa akisema kuwa Tume yake haitataka mashinikizo katika ufanyaji wake wa kazi. Kauli hii ya Mheshimiwa Warioba ingawa inaweza kuwa ilitolewa kwa dhamira nzuri imetafsiriwa na wananchi wengi kuwa Tume itapenda iachwe, iandike Katiba ya Watanzania bila kusukumwa na mtu yeyote. Hata hivyo, ukweli na uzoefu ni kwamba uundaji wa Katiba mpya ni ujenzi wa muafaka wa Kitaifa na hakuna muafaka unaweza kujengwa bila msukumo wa wananchi. Kwa maoni yetu, mwana Tume asiyetaka mashinikizo kutoka kwa umma atalazimika kujiengua na kupisha wenye uwezo wa kusikiliza matakwa ya wananchi. Tatu, tumestushwa na Hotuba ya Rais wa Zanzibar ambayo ilikuwa na ujumbe kuwa wanaotaka fujo waondoke Zanzibar na kwamba wazanzibari wasubiri maelekezo ya Tume na wasiendelee na mijadala kuhusu Katiba. Kwa hili, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ameshindwa kutofautisha mijadala ya wananchi kuhusu muungano na uvunjifu wa amani. Akihutubia siku ya tarehe 8 Mei alipokuwa Koani, Kisiwani Unguja, Mh. Dr. Shein alitamka wazi kuwa ‘yeyote aliyechoka na amani ahame Zanzibar’ Jukwaa la Katiba Tanzania na Baraza la Katiba Zanzibar tunaamini kuwa mijadala ya amani kuhusu Muungano siyo lazima imaanishe kuvunja amani wala kuvunja sheria. Sisi tunaamini kuwa inawezekana kabisa kujadili Muungano bila kuvunja amani ya Nchi! Sambamba na matamshi ya Rais wa Zanzibar, tumestushwa na kusikitishwa zaidi na kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi na baadaye Waziri katika ofisi yake Mheshimiwa Mohammed Aboud, aliyepiga marufuku mihadhara, mikutano au makongamano yoyote kuhusu Katiba kwa madai kuwa Tume ya Katiba imeshaanza kazi kwa sababu hiyo ibaki Tume hiyo tu ikishughulikia masuala yote kuhusu Katiba na si Asasi za kiraia, shirika wala kikundi chochote kingine. Katazo hilo limefanana na lile alilotoa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba ndugu, Dadi Faki Dadi ambaye naye alipiga marufuku mihadhara ya wananchi kuhusu katiba. Aidha wananchi wa eneo la Machomanne walizuiwa na jeshi la polisi kukutana na kujadili masuala ya Katiba, jambo linaloonekana kuwa mwendelezo wa vitisho na makatazo ya serikali kwa wananchi kujadili Katiba yao. Mwisho tumefadhaishwa na kitendo cha vitisho vya vyombo vya dola dhidi ya wale wote wenye mawazo tofauti kuhusu kuwepo kwa muungano au aina ya muungano unaohitajika. Ikiwepo kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wananchi 12 waliokuwa wakifurahia haki yao ya kikatiba kuhusu uhuru wa mawazo/maoni kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa. Aidha kukamatwa kwao ni ukiukwaji pia wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa ambayo inaweka bayana: Ibara ya 18 (1) ‘.......kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa’ (2) ‘Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii’. 19 (1) ‘Kila Mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo..........’ 20(1) ‘Isipokuwa kwa hiari yake, hakuna mtu atakayezuiwa kufurahia uhuru wake wa kuchanganyika au kujiunga yaani haki yake ya kuchanganyika na kujihusisha atakavyo na watu wengine .............’ Kutokana na matukio na kauli hizo, tumebaini uvunjifu mkubwa wa Katiba ya Zanzibar. Aidha, tunatoa tahadhari kwa viongozi pamoja na vyombo vya dola na kuwataka waache kuweka mazuio na makatazo kwa mijadala huru na ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika mchakato mzima wa kuandika Katiba mpya. Pia, Jukwaa na Baraza tunawahimiza wawakilishi wa wananchi katika vyombo vya kutunga sheria hususan Bunge la Jamhuri ya Muuungao wa Tanzania liifanyie marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 8 ya 2011 ili kutoa uhuru mpana zaidi wa ushiriki wa wananchi. Jukwaa la Katiba Tanzania na Baraza la Katiba Zanzibar tunaona kuwa, hali inayoanza kujitokeza ya kuwabana au kutaka kuwanyamazisha wananchi wasitoe mawazo yao kwa uhuru itasababisha kupungua kwa hamasa ya wananchi kuhusu Katiba mpya na hatimaye kupunguza ushiriki wa wananchi katika kuandika Katiba yao wenyewe. Kwa mantiki hiyo, tunapendekeza vipengele vifuatavyo vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba virekebishwe au kufutwa: 18 (6) ‘....Tume inaweza kuruhusu asasi, taasisi au makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni.......’ 20 (2) Kurekebisha makosa ya Tafsiri kwa kuwa siku thelathini na moja tafsiri yake siyo – [thirty one days]! 21(1) – (4) kinachotamka makosa mbalimbali na adhabu zake kifutwe chote kwa kuwa hakina nia nzuri na kwamba kukitokea wahalifu katika Mchakato, sheria nyingine za Nchi zipo na zitatukimika. Kwa hali ya sasa, kifungu hiki kinatishia wananchi na kitafanya wasishiriki katika kutoa elimu, maoni au mawazo kwa kuogopa kifungo cha kati ya mwaka mmoja na mitatu jela au faini ya kati ya shilingi milioni mbili na tano au adhabu zote mbili kwa pamoja! Kwa kuhitimisha, Tume ya Katiba haiwezi kuendelea na kazi ya kukusanya maoni kabla ya kurekebishwa kwa sheria hii. Kutokuwepo kwa Mkutano Mkuu wa Katiba na kuwa na Bunge Maalum la Katiba linaloshirikisha wabunge wa sasa wa Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bado ni upungufu mkubwa katika upatikanaji wa Katiba Mpya. Mwisho, Tume ni lazima itambue mchango wa wanahabari katika Mchakato mzima wa uundaji wa Katiba Mpya Tanzania na kuhakikisha makosa yaliyofanyika ya kuwasahau wanahabari katika uundaji wa Tume yasijirudie tena katika uundaji wa vyombo kama Mkutano Mkuu Maalum wa Katiba, Bunge Maalum la Katiba na hata katika ufuatiliaji wa zoezi la ukusanyaji maoni ya Wananchi. Imesainiwa na kutolewa kwa niaba ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA na BARAZA LA KATIBA ZANZIBAR, Deus M Kibamba Prof. Abdul Sheriff Mwenyekiti Mwenyekiti JUKWA A LA KATIBA TANZANIA BARAZA LA KATIBA ZANZIBAR

No comments: