TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, February 6, 2012

Aggrey Mwanri Atimuliwa na Nyoka Kanisani

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri



NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, juzi alitimua mbio kunusuru maisha yake pamoja na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Usharika wa Sanja Juu Mtaa wa Kilingi, baada ya nyoka kuibuka ghafla kanisani humo.

Tukio hilo la kushangaza lilitokea juzi katika ibada ya saa nne iliyokuwa ikiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao ya kuweka jiwe la msingi pamoja na harambee ya ujenzi wa kanisa hilo.

Mwanri aliyekuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kuendesha harambee hiyo ya ujenzi wa Kanisa la Kilingi, akiwa na mkewe katika meza kuu, aliwashangaza waumini alipokimbia huku na kule akiwa amenyanyua mikono yake. Kutokana na kuibuka kwa nyoka huyo, waumini walikimbizana na kiumbe huyo kwa mawe na viti bila kujali walikuwa ibadani, huku Askofu na wachungaji wengine wakiendelea kusali ambapo waumini walitakiwa kurudisha utulivu katika ibada.

Hata hivyo, jitihada za waumini za kumkimbiza nyoka huyo kutaka kumuua hazikufanikiwa, baada ya nyoka huyo kutoweka na kutooneka tena, jambo lililoacha simulizi ni kwa jinsi gani alifika mahali hapo.

Katika harambee hiyo, alitazamiwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwa mgeni rasmi, lakini kutokana na kubanwa na shughuli za sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa CCM, alishindwa kufika.

'Habarileo' lilishuhudia Mwanri ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha akikimbia huku akitoa sauti kubwa akisema ‘shindwa kwa jina la Yesu wewe shetani, shetani shindwa kwa jina la Yesu,’ huku wageni wengine waalikwa wakianguka chini wakati wakikimbia kujiokoa.

Akizungumza na 'Habarileo', Mwanri alisema tukio hilo ni la kushangaza zaidi, kwani nyoka huyo alipita nyuma ya watu wote, lakini hakuonekana hadi kufika katika meza yake huku akiwa ameweka kichwa chake juu akitema sumu.

“Inashangaza sana kwani lazima ujiulize kalifikafikaje hapo mbele, wakati nyuma yangu kulikuwa na watu wengi...alikuwa na hasira sana kwani alikuwa tayari kung'ata, kwa kweli hadi sasa mimi sielewi ni mambo gani haya,” alisema Mwanri.

No comments: