TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, December 26, 2011

Kesi kupinga Katiba Mpya yaiva




CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimesema kimekamilisha mchakato wa kufungua kesi ya kikatiba, kupinga sheria ya mapitio ya katiba iliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete, Novemba 29 mwaka huu.Rais wa chama hicho, Francis Stolla, aliliambia gazeti hili jana kuwa chama kinatengeneza hati ya mshtaka ambayo yatafunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, katikati ya Januari mwakani.

"Hii ni kesi ya kikatiba, haihitaji kutoa taarifa kwa Serikali. Tunatumia sheria ya haki za msingi na wajibu wa kutekeleza ya mwaka 1994," alisema alipoulizwa kama tayari walishaitaarifu Serikali kuhusu kusudio hilo.Kwa mujibu wa Stolla, kesi hiyo ni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tumeunda kamati ya kushughulikia katiba, yenye wajumbe wanane. Kwa sasa wajumbe hao wako katika mchakato wa kuandaa hati ya mashtaka. Wakimaliza, tutateua mawakili watatu wa kuisimamia kesi hiyo mahakamani kwa niaba ya chama,” alisema Stolla.

“Kwa sababu sheria inasema ukitaka kishitaki serikali inabidi umushitaki Mwanasheria Mkuu, kwa hiyo tutafanya hivyo lakini kesi hii ni ya kikatiba na mlengwa wetu ni Bunge,” alisisitiza.

Alisema hatua ya kulishtaki inatokana na dhamana ya chombo hicho ya kutunga sheria. "Tunalishtaki kwa sababu sheria hiyo iliyoitunga ni mbovu,”alisema.

Stolla alisema sababu za kufungua shtaka hilo ni pamoja na sheria hiyo kukiuka katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Alitaja ibara zilizokiukwa kuwa ni pamoja na ile ya 18 inayowapa nafasi wananchi kutoa maoni yao na ibara ya 22, inayotaka wananchi washirikishwe kwenye masuala muhimu na yenye maslahi kwao.Kwa mujibu wa Stolla sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo, ni sheria hiyo kukiuka taratibu za utungwaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge baada ya kusoma mara mbili, badala ya mara tatu kama inavyotakiwa kisheria.

“Mara ya kwanza walipowasilisha hati ya dharura bungeni, kelele zilipigwa kuwa iondolewe na utaratibu wa kutungwa kwa sheria hii uwe wa kawaida. Pia kutaka ule muswada uandikwe kwa lugha ya Kiswahili, mambo yale yalitekelezwa,”alisema.Alisema kuwa baada ya kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo Watanzania wengi wanaielewa, muswada ulipaswa kurudishwa kwa wananchi ili waujadili lakini jambo hilo halikufanyika.

“Siku ile wanasoma ule muswada wa Kiingereza kwa mara pili, waliusoma ule wa Kiswahili kwa mara ya kwanza lakini wakadai kuwa ni mara pili. Halafu wakaja kusoma tena mara ya pili na kuupitisha. Sheria inataka usomwe mara tatu, kwa hiyo ni wazi kuwa huu ulipitishwa baada ya kusomwa mara mbili badala ya mara tatu kama inavyotakiwa,”alifafanua Stolla.

Alisema sababu nyingine ni sheria hiyo kuwa na vipengele vinavyozuia watu au asasi nyingine nje ya tume itakayoundwa kuwaelimisha wananchi juu ya katiba.

Stolla alisema katika kifungu cha 22, sheria hiyo inaweka makosa ya jinai na adhabu kwa mtu ama taasisi, itakayofanya kampeni ya kuhamasisha juu ya katiba.

“Kwa sheria hii midahalo kama inayofanywa sasa hivi inaharamishwa, ni tume ya katiba mpya tu ndiyo itahamasisha kwa mikutano maalumu, kwa hiyo sisi tunadhani kuwa hali hiyo inanyima uhuru wa kutoa maoni,” alieleza.

Msimamo huo wa TLS unakuja siku moja tangu vyombo vya habari vimkariri Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Profesa Issa Shivji akiikosoa sheria hiyo kwa kile alichosema kuwa ni mbovu na haitazaa katiba bora.

Akichambua sheria hiyo, Profesa Shivji alikosoa kifungu cha 21 akisema kuwa kinashangaza kwani kinazuia hata watu kuikosoa sheria hiyo.

“Mimi nasema kuwa sheria hii ni mbovu, katika sheria hii, kifungu hiki kinanizuia hata kusema, sheria hii ni mbovu’. mimi sijui kulikuwa na fikra gani kuweka kifungu kama hiki, kitu kimoja tu ni kwenda mahakamani kuipinga,” alisema.

Akichambua kifungu kimoja baada ya kingine katika sheria hiyo, Profesa Shivji alisema imewatenga kabisa wananchi katika mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya.

“Wananchi wanatakiwa kushirikishwa tangu hatua ya kwanza, kwa mchakato wa Bunge, yaani sisi wenyewe tumeshirikishwa kupitisha sheria hiyo kuhakikisha kuwa vyombo vyote vinavyohusika vinafuatwa.” Alisema Profesa Shivji.

Akitoa mfano wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Katiba, Profesa Shivji alisema haikufanya kazi yake kikamilifu hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kutoa maoni.

Novemba 29 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitia saini muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 huku kukiwa na malumbano makali kutoka asasi za kiraia, vikiwemo vyama vya siasa, kupinga hatua hiyo kwa maelezo kwamba, mchakato huo uliendeshwa kwa mizengwe.

Hata hivyo, taarifa ya kusainiwa kwa muswada huo iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema hatua hiyo ya Rais Kikwete, ilikamilisha safari ya kutungwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 baada ya Bunge kupitisha muswada huo uliowasilishwa na Serikali huku ikiweka wazi kuwa Serikali itaendelea kusikiliza maoni na
mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria
hiyo.

‘’ Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru
kutoa maoni yake na Serikali itayasikiliza na kuchukua hatua zipasazo’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

No comments: