TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, November 22, 2011

Mattaka na waliokuwa maafisa wa ATCL kizimbani




David Mataka akitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuweka kumbukumbu za manunuzi ya magari chakavu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni moja.

Mbali ya Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Elisaph Ikomba aliyekuwa Kaimu Mhasibu Mkuu na William Haji alliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya ndani wa shirika hilo.

Mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincon alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai 2007.

Katika shitaka la kwanza ambalo linawahusu washtakiwa wote, ilidaiwa kuwa kati ya Juni na Julai 2007 Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washitakiwa kwa nafasi zao walishindwa kutunza kumbukumbu za taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa shitaka la pili nalo linawahusu washitakiwa wote ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 washtakiwa kwa pamoja walishindwa kufuata taratibu za manunuzi ya umma katika ununuzi wa magari chakavu 26 yenye thamani ya Dola za Marekani 809,300,000 kutoka katika kampuni ya Bin Dalmouk Morots Co. Ltd ya nchini Dubai.

Katika shitaka la tatu linalomuhusu Mattaka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 mshitakiwa akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa ATCL alitumia madaraka yake vibaya katika ununuzi wa magari hayo bila kuwepo kwa mkataba wa zabuni uliosainiwa na pande zote mbili na kuhakikiwa na bodi ya zabuni ya shirika hilo suala ambalo ni kinyume cha sheria.

Washitakiwa wapo nje kila mmoja kwa dhamana ya Shilingi Milioni 20/= huku wakiwa na wadhamini wawili ambao kila mdamini alitia saini ya Shilingi milioni kumi.

No comments: