TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, September 17, 2011

WABUNGE WA CHADEMA WASWEKWA LUPANGO HUKO IGUNGA

Mkuu wa wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario akiwa amekamatwa na wanachama wa Chadema

JESHI la Polisi wilayani Igunga limefungua majalada mawili na kuwahoji watu watano wakiwamo wabunge wawili wa Chadema; Suzan Kiwanga na Sylvester Kasulumbayi, kwa vurugu zilizotokea juzi, kufuatia Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Kimario, kukamatwa na makada wa chama hicho. Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na viongozi wa Chadema zimeeleza kuwa, wabunge hao walihojiwa kwa nyakati tofauti jana katika Kituo cha Polisi cha Igunga wakiwa na mwanachama mmoja wa chama hicho, Anuari Kashaga.

Mkuu wa kitengo cha ufuatiliaji wa tathimini kutoka Makao Makuu ya Upelelezi wa makosa ya jinai, Issaya Mungulu, alieleza kuwa polisi imewashikilia watu sita na kufungua majalada mawili kituoni hapo kuhusu shambulio la aibu na kuingiliwa kwa ratiba ya mkutano wa kampeni.

Jalada moja ni la Mkuu wa Wilaya kunyanyaswa na kufanyiwa shambulio la aibu na la pili na Chadema wanaodai kuwa ratiba yao iliingiliwa na Mkuu huyo wa Wilaya na kwa lengo la kuvuruga mkutano wao wa kampeni uliokuwa unafanyika katika eneo hilo

Alisema Chadema walitakiwa kufanya mkutano katika eneo hilo kuanzia saa 4 asubuhi juzi hadi saa 6 mchana na wakati huo huo mkuu wa Wilaya alikuwa akifanya mkutano wa ndani na watendaji wa Serikali.

“Kufuatia mkutano huo wa mkuu wa Wilaya kuingiliana na Chadema eneo hilo, wanachama, viongozi, wafuasi na wapenzi wao, walichukizwa na hali hiyo wakidai kuwa wameingiliwa kwenye mkutano wao na Mkuu huyo wa Wilaya,” alisema Mungulu.

Aliongeza kuwa: “Kwa pamoja waliamua kuvamia kikao cha Mkuu wa Wilaya kwa nia ya kumshambulia na kuvunja kikao alichokuwa akikiendesha.”

Alisema kuwa katika tukio hilo Mkuu wa Wilaya alivuliwa hijabu, viatu, alikatiwa mkufu ambao thamani yake haijajulikana na simu yake ya mkononi aina ya Sumsung yenye thamani ya Sh400,000 ilipotea. “Pia walimtukana matusi mbalimbali ya kumdhalilisha,” alisema.

Alisema jeshi la polisi lilipokea taarifa hizo kutoka kwa Afisa Tawala wa Wilaya aitwaye, Sumera Manoti na baadaye kuzipokea kutoka kwa askari walikwenda eneo la tukio kwa lengo la kukabili vurugu, kurudisha hali ya amani na kukagua eneo la tukio kwa nia ya kukusanya vielelezo na ushahidi.

“Askari walikuta hali ya eneo hilo ni shwari na upelelezi ulianza mara moja ambapo majalada mawili ya uchunguzi yalifunguliwa moja la madai ya Chadema na lingine la madai ya DC,” kudhalilishwa alisema.

Alitoa wito kwa vyama, viongozi wao, wanachama na wafuasi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi hususani katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi mdogo jimbo la Igunga.

Chadema walia na maadili
Katika hatua nyingine Chadema imewasilisha malalamiko dhidi ya Mkuu huyo wa Wilaya kwa Mwenyekiti wa Kamati ya maadili ya uchaguzi kufuatia kuitisha mkutano katika eneo la mkutano la chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila, alisema kuwa mkuu huyo wa Wilaya amevunja sheria ya maadili ya vyama vya siasa na Serikali wakati wa kampeni ambayo inamtaka ofisa wa Serikali kutokutumika na au kujihusisha na kampeni za vyama vya siasa.

Alisema kuwa katika nyaraka walizomkuta nazo mkuu huyo wa Wilaya ni kufanya zoezi la kuweka wasimamizi wa vituo na waelekezaji katika uchaguzi kitendo ambacho ni hujuma ya uchaguzi na kinyume cha sheria.

“Kwa sababu ya makosa haya, tunataka kamati yako imwite Mkuu wa Wilaya na aeleze kwa nini amefanya makosa hayo na aadhibiwe kwa mujibu wa sheria ya maadili ya uchaguzi,” alisema.

Alisema wamepeleka nakala ya malalamiko hayo kwa Kamanda wa polisi wa wilaya, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Jeshi la polisi nchini na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kigaila alisema nyaraka zote walizomkuta nazo mkuu huyo wa Wilaya watazipeleka katika balozi za mataifa yote nchini na katika mifumo yote ya Serikali ili waelewe nini kinatendeka.

Ofisi ya msimamizi
Wakati hayo yakitendeka, Ofisa Uchaguzi wa Jimbo la Igunga, Martha Bayo, alisema kuwa hakuwa alipata taarifa za kitu gani Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa anafanya, lakini kimaadili kama alikuwa hafanyi shughuli za mhadhara basi alikuwa hana tatizo lolote.

“Hatuwezi kulitolea ufafanuzi, DC alikuwa anafanya shughuli zake za kiserikali na wale wengine walikuwa na mkutano ila hatujapata taarifa rasmi,” alisema Bayo.

Kuhusu ratiba alisema kuwa jana Chadema walikuwa na mkutano saa 4 hadi saa 6 katika Kata ya Mbutu na wakati huohuo, walitakiwa wawe na mkutano katika Kata ya Isakamaliwa.

Waandishi wakosa uvumilivu
Katika mkutano huo baadhi ya waandishi wa habari walionekana kukosa uvumilivu baada ya kuonyesha waziwazi itikadi zao na kuanza kujibizana wenyewe kwa wenyewe juu ya mambo ambayo majibu yake yalipaswa kutolewa na Kamanda wa Polisi.

Waandishi hao walionekana kuuliza maswali mengine ambayo yalikuwa hayahusiani na polisi kitendo ambacho kilifanya waanze kujibizana wenyewe mbele ya Mungulu.

Kiravu ailamu Chadema
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Rajabu Kiravu, amesema kitendo cha Chadema kumkamata Mkuu wa Wilaya ya Igunga na kumweka chini ya ulinzi wao ni uhuni.Kiravu alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na tume hiyo na viongozi wa vyama vya siasa nchini.

Alisema kitendo cha Chadema kumkamata Mkuu huyo wa Wilaya ni uhuni, kwani hata kama alikuwa amefanya kosa, walipaswa kufuata taratibu za kisheria.”Walitakiwa wafuate taratibu, hawawezi wakajichukulia hatua za kumkamata. Kama alikuwa amevunja sheria walitakiwa wampeleke kwenye tume ya maadili,” alisema Kiravu na kuongeza:

“Ule ni uhuni tu, kama kosa limetendeka kuna taratibu zake, Ifike mahala watu tuheshimiane huu, utaratibu wa kukamata umetoka wapi?” alihoji.

Kwa mujibu wa Kiravu, uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga haufanyi shughuli za kiserikali kusimama na Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kiseriakali, hakuna kosa.

“Uchaguzi haimanishi shughuli za Serikali zinasimama. Serikali ipo na inaendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Kiravu.Kiravu alisema majina ya mawakala yanapaswa kuwasilishwa kwa wasimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya siku ya kupiga kura hivyo kanuni za uchaguzi huo mawakala wa vyama vya siasa wanatakiwa kula kiapo cha kutunza siri siku tatu kabla ya siku ya uchaguzi.

“Kutokuwepo kwa mawakala hakutazuia mchakato wowote kuendelea,” alisisitiza Kiravu

Mwenyekiti wa Mkutano huo, Jaji Mstaafu Mary Longway, alipiga marufuku mawakala wa vyama vya siasa kuorodhesha majina na namba za kadi za wapigakura wakati wa la kupiga kura.

“Vilevile ni marufuku kwa mgombea, chama cha siasa au wakala kupiga kampeni siku ya uchaguzi kwani mwisho wa kupiga kampeni ni siku moja kabla ya siku uchaguzi,” alisema Longway.

No comments: