TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, September 8, 2011

USHAIDI WA KAGODA WAITIKISA SERIKALI

Mfanya biashara Maarufu Yusuph Manji

Sakata la Kampuni ya Kagoda iliyokwapua sh bilioni 33 kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), limechukua sura mpyaa baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuunda kikosi kazi kuchunguza sakata hili.

Habari ambazo zimetapakaa jijini Dar zinasema kuwa ofisi hizo zimeteua maafisa wake kuunda kikosi kazi kuchunguza sakata hilo lililoibuka upya wiki iliyopita baada ya mwanaharakati maarufu nchini, Kainerugaba Erick Msemakweli, kuja na ushahidi mpya.

Msemakweli ambaye pia ni mwanasheria, alimtaja mfanyabiashara maarufu nchini Yusuph Manji and Rostam Aziz kwamba ndio wamiliki wa kampuni hiyo tata ya Kagoda Agriculture Ltd.

Kwa mujibu wa Msemakweli, wengine katika sakata hilo ni Tabu Omari, John Kato, Barati Goda, Gulam Abdurasul Chakaar na Bahram Abdurasul Chakaar.

Majina ya walioteuliwa kuunda kikosi kazi hicho na taasisi wanazotoka kwenye mabano ni pamoja na Benn Lincoln (TAKUKURU) na askari aliyejulikana kwa jina moja la Mswano, pia kutoka TAKUKURU.

Wamo pia Fadhili Mdemu toka ofisi ya DCI na Biswalo Makanga kutoka ofisi ya DPP.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya taasisi hizo, zilisema kuwa serikali imeamua kuchunguza upya sakata la Kagoda kutokana na ushahidi huo ambao ni wa kwanza kwa uzito kutolewa nchini.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Msemakweli amewasilisha ushahidi unaonyesha jinsi Rostam na Manji na washirika wao walivyohusika kuchota fedha hizo.

Moja ya ushahidi huo unaonyesha jinsi fedha hizo kutoka Kagoda, zilivyokuwa zikihamishwa kupelekwa Uarabuni.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, inaonyesha kuwa kati ya Oktoba 28 na Desemba 27, 2005, kiasi cha sh bilioni 3,081,648,500, kilitolewa kutoka katika akaunti ya Agriculture Company Limited. Kiambatanisho KM-15 cha kivuli cha moja ya maombi yaliyofanywa na kampuni hiyo kwa Meneja wa Tawi la Holland House Novemba 24, 2005 kwa vielelezo namba KAL/CRDB/09/05.

Desemba, 2005 fedha yote katika matawi mbalimbali ya CRDB ilikuwa tayari imebadilishwa kuwa dola za Marekani na kuhamishiwa katika akaunti ya dola ambayo Kagoda Agriculture Company Limited waliifungua kwa msaada wa Yusuf Manji na Rakesh Mehta katika CRDB Holland House.

Desemba 2005 na mwanzoni mwa mwaka 2006, fedha yote ya Kagoda Agriculture Company Limited kwenye akaunti yake katika tawi la Holland House yenye jumla ya dola za Marekani 28,960,000, ilihamishiwa katika akaunti ya mhusika wa kwanza kwenye tawi hilo kupitia cheki nne za benki kama ifuatavyo: cheki hizo ni dola 7,600,000 ya Desemba 27, 2005, cheki ya dola 7,400,000 ya Desemba 29, 2005, cheki ya dola 7,060,000 ya Januari 2, 2006 na cheki ya dola 6,900,000 ya Januari 2, 2006.

Kwa mujibu wa ushahidi huo ambao nakala tunayo, zaidi ya miezi kadhaa taratibu zilifanywa na Rakesh Mehta kwa maelekezo ya Yusuf Manji, kuhamisha dola za Marekani 28,960,000 nje ya nchi na kuzipeleka Dubai.

Fedha hiyo ilihamishwa kwa wingi wa dola 1,000,000 au jumla pungufu kiasi; kwamba Machi 31, 2006 kulikuwa na salio la dola 9,084,762.64 ambazo zilikuwa hazijahamishwa.

Katika tarifa yake, Msemakweli alikanusha kuwepo uhusiano wowote wa fedha hizo na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani.

Badala yake, Msemakweli alisema uchunguzi ulionyesha waliohusika na Kagoda ni wafanyabiashara maarufu wawili nchini kwa kushirikiana na jamaa zao wa karibu, “Watu hawa wamekuwa wakieneza uvumi kwamba fedha ziliibwa na kutumika kwa madhumuni ya kampeni ya CCM mwaka 2005, jambo ambalo si kweli.”

Akasema kati ya Desemba 30, 2005 na Januari 2, 2006 fedha hizo zilikuwa hazijatumika na uchaguzi ulikuwa umemalizika.

Alisema waliohusika katika kusajili Kagoda BRELA ni watu wawili chini ya udhamini wa mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam kwa kutumia kampuni zake na watu hao walitumia majina ya uongo ya Francis William na John Kyomuhendo, tofauti na majina yao halisi.

Alisema Kamati ya Johnson Mwanyika iliyoundwa na serikali kuchunguza sakata la wizi wa fedha za EPA, ilibaini kuhusika kwa wafanyabiashara hao, hivyo iliamua kumnyang’anya mmoja wao hati ya kusafiria, kufunga akaunti zote za kampuni zake na kumuamuru kurejesha fedha hizo.

Msemakweli alisema uzushi unaenezwa kwamba mwizi wa Kagoda hajulikani, wakatiKamati ya Mwanyika ilimwita na kumpa muda wa kurejesha na akafanya hivyo.

No comments: