TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, September 8, 2011

LIYUMBA APONZWA NA SIMU ALIYOMPIGIA JAKAYA, SASA KUFIKISHWA TENA MAHAKAMANI KUJIBU HOJA

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba

BAADA ya kukutwa na simu akiwa jela, Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba sasa anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kukutwa na nyenzo hiyo ya mawasiliano gerezani.

Liyumba ambaye kwa sasa anatumikia adhabu katika Gereza la Ukonga kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya umma wakati wa akifanya kazi BoT, anatuhumiwa kukutwa na simu hiyo gerezani na Septemba 2, alifikishwa katika kituo cha Polisi Stakishari kwa mahojiano na polisi.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), John Minja alisema Dar es Salaam jana kwamba kitendo alichokifanya Liyumba kilivunja sheria za nchi na kanuni za jeshi la Magereza.

Hatua hiyo ya Magereza imekuja baada ya polisi kutangaza kwamba haina kanuni inayoweza kutumiwa na jeshi hilo kumtia mtuhumiwa hatiani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alikaririwa mara baada ya Liyumba kuhojiwa akitoa wito kwa Jeshi la Magereza kutoa kanuni zinazoonesha kuwa hilo ni kosa.

Minja alisema Liyumba atapandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo wakati wowote mara baada ya polisi kukamilisha upelelezi wake.

DCP Minja alisema Liyumba alivunja Sheria ya Magereza Namba 34 ya mwaka 1967, Sura ya 58 kifungu cha 85 pamoja na Kanuni za Magereza Tangazo la Serikali (GN) Namba 13 la mwaka 1968.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye hana mamlaka ya kisheria atakayeingiza au kutoa kitu chochote gerezani kilichopigwa marufuku atakuwa na hatia. Kanuni hiyo ya Magereza inabainisha kuwa ni kosa kwa mfungwa yeyote kumiliki kitu chochote asichoruhusiwa kuwa nacho gerezani.

“Simu ni miongoni mwa vitu vilivyopigwa marufuku gerezani. Si mfungwa wala mahabusu tu lakini hata askari wa kawaida haruhusiwi kuingia na simu gerezani isipokuwa mkuu wa gereza na wasaidizi wake tu,” alisema.

Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 85 (1) adhabu ya kukutwa gerezani na kitu chochote kilichopigwa marufuku, ni faini isiyozidi Sh1,000 au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja.

Alisema athari za mahabusu au mfungwa kuwa na simu gerezani ni uwezekano wa kuathiri usalama wa gereza kwa kuwa mhusika anaweza kuitumia kupanga njama za uhalifu au hata kuvuruga ushahidi kwa kuwatishia mashahidi, hakimu au jaji.

“Kwa hiyo Liyumba alipokamatwa na alifikishwa katika kituo cha Polisi Stakishari kuhojiwa na alifunguliwa jalada namba STR/IR/8661/2011 na baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema DCP Minja na kuongeza;

“Wapo wengi tu ambao tulishawakamata na kuwapeleka mahakamani ambao walipatikana na hatia ya kosa na wakatumikia adhabu”.

Akizungumzia suala hilo wakili mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema: “Hili ni kosa la jinai. Ni hatari sana kwa usalama wa gereza kwani mfungwa au mahabusu akiwa na simu anaweza kushirikiana na watu wa nje kupanga njama dhidi ya gereza.”

Wakili huyo aliongeza: “Kwa kuwa anakuwamo ndani, basi anakuwa ameyajua mazingira yote ya gereza na udhaifu wake. Hivyo anaweza kutoa kwa watu wa nje ambao wanaweza kufanikisha kuvamia au kuingia na kuwatorosha wafungwa na mahabusu gerezani.”

Alisema kutokana na kosa hilo, mfungwa au mahabusu anayekamatwa na simu gerezani anafunguliwa mashtaka mahakamani na akipatikana na hatia adhabu yake huwa ni faini au kifungo jela au vyote viwili.

Siku alivyodakwa

Baada ya kubainika alikuwa na simu gerezani anayodaiwa kumpigia Rais Jakaya Kikwete, Liyumba alifikishwa kituo hicho cha Stakishari saa 3:00 asubuhi na kuhojiwa kwa muda wa takriban dakika 30.

Ili kukamilisha uchunguzi wake, Polisi inatarajiwa kushirikiana na kampuni ya simu iliyotumiwa kumwezesha mtuhumiwa kuwasiliana pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kujua alichokuwa akikifanya kwenye hiyo simu.

Liyumba alihukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 24, 2010 baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi. Hadi sasa Liyumba amekaa gerezani kwa muda wa miezi 15 tangu alipohukumiwa.

No comments: