TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, September 20, 2011

Kesi ya ajali ya Meli Zanzibar yasitishwa

Watuhumiwa wa kesi ya kufanya uzembe uliosababisha vifo vya watu katika ajali ya meli ya Mv Spice Islander iliyotokea eneo la Nungwi wakifikishwa katika Mahakama kuu ya zanzibar jana


KESI ya ajali ya meli ya MV Spice Islanders iliyofunguliwa dhidi ya manahodha wa meli hiyo na mmiliki wake, imesitishwa.Kesi hiyo ambayo jana ilitajwa kwa mara ya pili katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, imesitishwa kupisha uchunguzi wa kamati iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Hatua hiyo imefikiwa na Mrajisi wa Mahakama hiyo, George Kazi baada ya wakili wa utetezi, Hamidi Mbwezeleni, kuiomba Mahakama iiahirishe kwa sababu Katiba ya Zanzibar inapinga kesi moja kusikilizwa na vyombo viwili vinavyofanya kazi kwa mujibu wa katiba hiyo.

“Kama kuna haja ya watu hawa kushtakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, basi tume hiyo ikae pembeni mpaka Mahakama itakapomaliza kazi yake na kama kuna haja ya tume hiyo kufanya kazi yake, basi Mahakama inabidi ikae pembeni mpaka tume hiyo itakapomaliza kazi yake,” alisema.

Bila kufanya hivyo alisema: "Hukumu ya watu hawa itakuwa na utata kwa sababu endapo Mahakama ikisema kuwa wana makosa na wanastahili adhabu halafu tume hiyo ikasema kuwa hawana makosa na hawastahili adhabu, Wazanzibari hawatatuelewa,” alisema Mbwezeleni na kusisitiza:

“Upande mwingine ni kwamba kama Mahakama ikisema kuwa watu hawa hawana makosa na wanastahili kuwa huru halafu tume hiyo ikasema kuwa watu hawa wana makosa na wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria, hali itakuwa tete kwa wananchi dhidi ya Serikali yao na Mahakama kwa ujumla.”

Awali, maelezo hayo ya upande wa utetezi yalipingwa na Wakili wa mashtaka, Ramadhan Nasibu ambaye alisema kama Serikali, haina shaka yoyote juu ya kamati hiyo kwa sababu inafahamu kwamba uamuzi wake hauwezi kuingilia wala kuharibu uamuzi wa Mahakama, kwa kuwa Mahakama ni chombo huru kinachosimamia haki.

“Upande wa mashtaka unajizuia kuhoji uhalali wa tume hiyo kwa sababu ushahidi wao hauwezi kuizuia Mahakama isifanye kazi yake wala haitakuwa mwisho wa mashtaka ya watu hao. Tume hiyo haina meno kwa sababu ushahidi wao utakaopatikana hauwezi kuwatia watuhumiwa hao hatiani,” alisema.

Baada ya malumbano hayo, Mrajisi wa Mahakama alikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuahirisha kesi hiyo.

Akisoma uamuzi huo Mrajisi Kazi alisema: “Siko tayari kusema kuwa tume hiyo ni halali ama si halali, ila kwa pointi iliyotolewa na upande wa utetezi, nami ninaona kwamba ni ya msingi, hivyo ninalazimika kuiahirisha kesi hii mpaka tume hiyo itakapomaliza kazi yake na kutoa mapendekezo.”

“Siwezi kuwa katika mtizamo tofauti na upande wa utetezi kuhusu suala hilo, kwa sababu kuna hatari ya uamuzi wa tume na mahakama, kupingana. Hivyo ninaahirisha kesi hii mpaka tume hiyo itakapomaliza kazi yake.”
Mrajisi Kazi pia alisema kuwa dhamana ya watuhumiwa hao iko wazi hivyo wanatakiwa kudhaminiwa kwa hati ya Sh1milioni kila mmoja na watahitajika Mahakamani hapo mara tu baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake na kutoa uamuzi.”

Septemba 10, mwaka huu meli ya MV Spice Islanders iliyokuwa ikitokea Unguja kwenda Pemba ilizama katika Kisiwa cha Nungwi, kilometa 20 kutoka Unguja na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 na majeruhi zaidi ya 600, huku ikiaminika kwamba mamia ya abiria wengine hawakuolewa baharini.

Siku tatu baada ya ajali hiyo, watu wanne akiwamo
Nahodha wa meli hiyo, Saidi Abdala Kinyanyite (58), mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam na Nahodha Msaidizi, Abdallah Mohamed Ali (30), mkazi wa Bububu, Zanzibar walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa uzembe na kusababisha vifo vya watu.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Simai Nyange Simai (27), Mkazi wa Mkele, Zanzibar ambaye ni Ofisa Usalama wa Bandarini na vyombo vyote vya usafiri wa majini na Yussuf Suleiman Jussa (47), Mkazi wa Kikwajuni Zanzibar ambaye ni Ofisa wa meli hiyo na mwanahisa.

No comments: