TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, September 21, 2011

CHADEMA YASHINDA KESI DHIDI YA MADIWANI WAKE


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imetupilia mbali kesi ya madai namba 17/2011 iliyofunguliwa Agosti 10, mwaka huu na madiwani watano waliokuwa wakipinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).Madiwani hao, John Bayo, Ruben Ngowi, Charles Mpanda, Rehema Mohamed na Estomih Mallah walikuwa wamefungua kesi hiyo kupinga kuvuliwa uanachama na kupinga kusemwa vibaya kwenye mikutano ya hadhara itakayofanywa na chama hicho mkoani Arusha.

Hakimu Mkazi Mahakama hiyo, Hawa Mguruta alisema mahakama
haiwezi kuingilia uamuzi wa Chadema akisema ni sahihi kwa sababu kimesajiliwa kisheria kikiwa ni chama cha siasa.

Alisema Mahakama hiyo haiwezi kukiuka katiba ya chama hicho pamoja na uamuzi wowote uliofikiwa huku akinukuu kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na mahakama mbalimbali nchini.

“Hoja zilizotolewa na walalamikaji katika hati yao ya madai hazina
msingi kwa sababu Chadema ni chama cha siasa na si chama chenye maslahi binafsi hivyo siwezi kupingamana na maamuzi ya chama, kwa hiyo kesi hii naitupilia mbali,” alisema hakimu huyo.

Hakimu huyo alikuwa akitoa uamuzi wa pingamizi za awali zilizowekwa na mawakili wa utetezi wa Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliowakilishwa mahakamani hapo na Method Kimomogoro na Albert Msando.Baada ya uamuzi huo kutolewa, Mallah, Bayo na Ngowi waliokuwa mahakamani hapo walisema hawana la kusema juu ya uamuzi huo.

Washangilia ushindi
Baadhi ya wanachama wa Chadema walishangilia ushindi huowakiwa ndani ya mahakama mara baada ya Hakimu Mguruta kuondoka huku baadhi yao wakisema mahakama ni mkombozi katika kuleta amani nchini na kuwasihi mahakimu wengine kutopindisha sheria, bali kutoa haki kwa kila raia.

Nje ya mahakama, wanachama hao walikata miti na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali za ushindi hadi Ofisi ya Mbunge wao, Godbless Lema huku polisi wakiwasindikiza bila kutumia nguvu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Lema alisema hakuna mbunge anayefurahia kupoteza madiwani wake watano aliowapata kwa gharama lakini ikiwa wanakiuka sheria na kanuni hakuna jinsi.

Mbunge huyo alisema wanakusudia kufungua mashtaka dhidi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Estomih Chang'ah na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika kutokana na kuamuru madiwani waliofukuzwa kuendelea na vikao na kulipwa posho.

Alisema kutokana na ushindi walioupata wametoa televisheni tano, taulo za kike, kompyuta moja na printa tatu kwa mahabusu na wafungwa waliopo Gereza Kuu la Arusha.

Alitaka uchaguzi wa Meya wa Arusha Mjini urudiwe upya akisema hata kama Chadema hakitashinda akisisitiza kwamba hakimtambui Meya wa sasa, Gaudence Lyimo.

Awali, Wakili Kimomogolo katika pingamizi zake alizoziwasilisha
mahakamani kwa njia ya maandishi alidai Mbowe hawezi kushtakiwa binafsi, Chadema hakiwezi kushtakiwa kwa jina lake na kwamba maombi ya kufukuzwa uanachama yamepitwa na wakati kwani madiwani hao walishakata rufaa Baraza Kuu la Chama hicho, hivyo Mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, bali Mahakama Kuu.

Naye wakili upande wa wadai, Severine Lawena katika pingamizi zake kimaandishi alidai kuwa kesi hiyo ina mchanganyiko wa mambo mengi na kusisitiza kuwa wateja wake warudishiwe uanachama kwani walivuliwa kimakosa.

Barua ya Mkuchika
Waziri Mkuchika alindika barua yenye kumbukumbu namba
HA.23/235/01/06 iliyotolewa Agosti 23 na kumfikia Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Chang'ah ambayo ilisema kuwa Tamisemi bado inawatambua madiwani hao na kwamba wataendelea kulipwa posho zao hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi.

Barua hiyo pia ilisema kuwa Mahakama ndiyo mwamuzi wa mwisho hivyo ni vyema suala hilo likasubiriwa kutolewa uamuzi lakini madiwani hao kisheria wataendelea kuhudhuria vikao na kulipwa posho zao .

Awali, Chang'ah alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari alisema alipokea barua hiyo ya Mkuchika kutokana na barua ya awali ya aliyoandika Agosti 12 mwaka huu.

Alisema suala la madiwani hao kuendelea na nyadhifa zao litaamuliwa na mahakama kwa kuwa walishafungua kesi ya madai. Alisema Sheria ya Serikali za Mitaa namba 8 ya mwaka 1982 kifungu cha 26 (1) (e) inafafanua kuwa waziri mwenye dhamana na Serikali za mitaa atatamka kuwa nafasi ya diwani iko wazi baada ya kupokea taarifa rasmi ya maandishi kutoka kwa Mwenyekiti au Meya wa Jiji.

No comments: