TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, August 29, 2011

MKUCHIKA VUNJA KATIBA YA NCHI, AAMURU MADIWANI WALIOFUKUZWA NA CHADEMA WAHUDHURIE VIKAO


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), George Mkuchika, amedaiwa kukiuka Katiba ya nchi kutokana na kuandika barua ya kuruhusu madiwani watano waliofukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuruhusiwa kuendelea kuhudhuria vikao vya baraza na kutakiwa kulipwa stahili zao zote.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kesi ya viongozi wa chama hicho katika Mahakama Kuu mwanasheria, Methodi Kimomogolo, ambaye alitoa kauli hiyo baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa kuonyesha nakala ya barua iliyotoka kwa Mkuchika yenye kumb Na HA 23/235/01/16 ya Agosti 23, mwaka huu, iliyotumwa kwa Meya wa Manispaa ya Arusha, Gaudensi Lyimo, kuhusu hatma ya madiwani hao.

Nakala ya barua hiyo ambayo ilibeba kichwa cha habari kinachosema ‘Kuvuliwa uanachama hivyo kukosa sifa ya kuwa diwani’ huku mwisho wa barua hiyo ikisema kuwa ’kutokana na madiwani hao watano kufungua kesi na kuiomba mahakama kuwarejesha uanachama wataendelea kuhudhuria vikao vyote vya baraza na kulipwa stahili zote hadi mahakama itakapotoa uamuzi’.

Wakili Kimomogolo alisema maamuzi yaliyofikiwa na Mkuchika yalikiuka Katiba ya Muungano kwa vile mtu anayehitaji kugombea uongozi katika nafasi yoyote ni lazima awe na dhamana ya chama.

Alisema kuwa vipengele vingine vinaweka bayana kuwa katika suala la urais, ubunge na udiwani utakoma pindi chama kilichomwekea dhamana kitaondoa dhamana yake na kusema kwa kuwa tayari CHADEMA ilikwishaondoa dhamana kwa madiwani hao sasa hawana sifa.

Wakili Kimomogoro alisema kuwa inashangaza kuona serikali iliyopinga mgombea binafsi mahakamani na kushinda kesi lakini inakuja kuwatambua madiwani ambao mdhamini wao amekwishawafukuza ambaye ni CHADEMA.

“Kwenye kesi aliyofungua Mchungaji Christopher Mtikila ambapo mahakama imeamua hakuna mgombea binafsi hivyo maamuzi yanayofanywa na madiwani hao kwenye vikao vya baraza nayo ni batili na posho wanazopokea ni wizi na anayewapa atawajibika kuzilipa, ” alisema Kimomogoro.

Naye Dk. Slaa alisema alishangazwa na maamuzi hayo kwa kuwa madiwani hao walishavuliwa uanachama na kupelekea kukimbilia mahakamani ili kurejeshewa uanachama wao hivyo iwapo waziri ataendelea kuwatambua wakati chama hicho kiliondoa dhamana ni kukiuka taratibu za sheria.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Estomii Chang’a, alikiri kuipata barua hiyo anachokitekeleza ni maamuzi hayo yaliyotoka ngazi za juu.

Madiwani waliofukuzwa CHADEMA baada ya kukaidi maamuzi ya Kamati Kuu yaliyowataka kujivua nyadhifa walizopata kupitia muafaka walioingia bila baraka za chama hicho na kata zao kwenye mabano ni Naibu Meya , Estomih Mallah (Kimandolu), Charles Mpanda (Kaloleni), Ruben Ngowi (Themi) na Rehema Mohamed (Viti Maalum).

No comments: