TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, August 31, 2011

Kikwete, Rostam wafikia muafaka • Akubali kumpigia debe mgombea CCM Igunga


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameingia katika muafaka na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, na amekubali kumpigia debe mgombea wa chama hicho, Dk. Dalaly Kafumu.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, zilisema kuwa mbali ya Rostam kukubali kupanda jukwaani kumnadi Dk. Kafumu, pia amekubali kuchangia fedha kwa ajili kuwezesha kampeni za mgombea wao.

Rostam na Kikwete kabla ya kutofautiana kisiasa, walipata kuwa watu wa karibu sana, hasa mwaka 2005 ambapo mfanyabiashara huyo akishirikiana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, walianzisha mtandao uliofanikisha kumwingiza Kikwete madarakani.

Hata hivyo uhusiano wao ulidorola hivi karibuni hasa baada ya Rais Kikwete kuanzisha vita ya kuwavua magamba makada wake watatu, akiwamo Rostam waliotuhumiwa kwa ufisadi na kusababisha kipate ushindi wa kura kiduchu kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Makada wengine wanaopaswa kujivua gamba ni pamoja na Lowassa (Monduli) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).

Habari zaidi kutoka ndani ya duru za CCM, zinasema kuwa Kikwete mwenyewe ndiye aliyefanya juhudi binafsi kuhakikisha wanamaliza tofauti zao na Rostam ili aweze kushiriki kampeni za uchaguzi mdogo Igunga ambao tayari umeshaanza kuvuta hisia za wengi nchini.

Kwa mujibu wa habari hizo, CCM imebaini kuwa bila Rostam kushiriki kampeni hizo, chama hicho kitakuwa na wakati mgumu hasa kutokana na uhasama uliopo kati ya chama hicho na mfanyabiashara huyo.

Katika uchaguzi huo, CCM inaihofia zaidi CHADEMA ambayo imezidi kuimarika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu na kufanikiwa kupata viti vingi vya ubunge.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ametangaza kuwa chama hicho, wabunge na makada wake maarufu wote watapiga kambi Igunga kuhakikisha wanapata ushindi katika jimbo hilo.

“Unajua Rostam amejiuzulu ubunge, lakini bado ana hasira na chama hasa na Kikwete aliyemfikisha hapa. Kule Igunga ana watu wengi wanaopenda, kama hataonekana kwenye kampeni Igunga, ushindi kwa CCM utakuwa mgumu. Walichokubaliana na Rais wanakijua wao, lakini atakwenda kwenye kampeni,” alisema mtoa habari wetu.

Mbali ya Rostam, CCM pia imeamua kumuangukia Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kwenda kuzindua kampeni hizo Igunga.

Mkapa ambaye jana alishiriki kikao cha Kamati Kuu, aliwahakikishia wajumbe wa kikao hicho kwamba licha ya kukabiliwa na ratiba ya mikutano mingi nje ya nchi, atashiriki kwenye mkutano wa kwanza wa kampeni kwani kwake chama kinakuja kwanza.

Katika hatua nyingine, licha ya wito wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe, kumtaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, wakutane Igunga kwenye kampeni, Rais huyo hatakwenda Igunga.

Habari ambazo gazeti hili imezipata, zilisema azimio hilo lilipitishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichokutana jana jijini hapa ambapo pamoja na mambo mengine, kilipitisha jina la mgombea wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo la Igunga.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu Kikwete kwenda Igunga, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema mwenyekiti wao hawezi kwenda kwenye kampeni hizo sio utaratibu wa chama hicho.

“Rais hawezi kwenda Igunga, ule ni uchaguzi mdogo tu na kwa kawaida hatujawahi kumpeleka Rais kwenye uchaguzi mdogo. Miaka mitano iliyopita tumefanya uchaguzi mdogo Tarime, Busanda, Kiteto na kwingineko, hatujampeleka Rais na hata Igunga, hataenda,“ alisema Nape.

Uchaguzi mdogo katika jimbo hilo, unatarajiwa kufanyika Oktoba 2.

Vyama vilivyokwisha thibitisha ushiriki wake mbali ya CCM ni pamoja na CHADEMA, kilichomsimamisha ambacho kimeonekana kuungwa mkono na wengi. Mwingine ni Joseph Kashindye na Leopard Mahona wa CUF.

No comments: