TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, July 29, 2011

N.G.Os NA VYAMA VYA UPINZANI KUBANWA.SHERIA YA KUZUIA MAANDAMANO INAANDALIWA

Jaji Frederick Werema

KAULI za kuendelea na maandamamo mpaka kieleweke ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wa Chadema zinaonekana kuikera Serikali na sasa inakusudia kuifanyia marekebisho sheria husika ili kuyadhibiti.Maandamano ni miongoni mwa mambo ambayo yalitawala mjadala wa siku mbili bungeni wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, iliyowasilishwa juzi na Waziri Shamsi Vuai Nahodha.

Akichangia hotuba hiyo jana kabla ya kuahirishwa kwa Bunge kwa ajili ya mapumziko, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema mabadiliko hayo ya sheria yatalenga kuzuia bughudha katika maeneo ambayo watu hawashiriki maandamano husika.

"Tunadhani kuna haja ya kurekebisha sheria ili kuregulate (kudhibiti) maandamano katika maeneo ambayo watu si washiriki wa maandamano hayo, hili linawezekana maana nchi kama Ujerumani wamefanya hili," alisema Werema na kuongeza:

"Nimesikia hapa kauli mbalimbali zinazohamasisha maandamano na wengine wanasema tutaandamana mpaka kieleweke na wengine wanasema kutoka Mwanza mpaka Dar es Salaam, tunasema ndiyo ni haki ya kisheria, lakini lazima tuzingatie kwamba wapo wasiopenda maandamano haya."

Kadhalika, Werema alitumia nafasi hiyo kutoa somo kwa wabunge kuhusu mivutano iliyotokea bungeni siku chache zilizopita: “Peaneni nafasi kwa kila mtu na mwenzake na muwe na ushirikiano kama ambavyo mikono ya kushoto na kulia inakuwa na ushirikiano mzuri.”

Jaji Werema aliwaambia wabunge kuwa kazi ya kuwakilisha wananchi inahitaji uvumilivu kuliko kazi nyingine na akawataka wabunge wa pande zote kutumia lugha za kistaarabu wanapo kuwa ndani ya ukumbi wa bunge.

Hata hivyo, alikemea tabia za baadhi ya wabunge kutumia lugha za maneno makali akitolea mfano wa hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi... “Ni kweli Mheshimiwa Lema (Godbless) alitumia lugha kali kidogo.

Hapa naomba ifahamike hivyo, lakini yote mimi ambaye ni Mwanasheria wa Serikali nasema muendelee kuvumiliana na kuangalia lugha za kutumia. Namshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi (William), katika hotuba ile alitaka kusimama amzuie Lema, lakini nikamwabia muache aendelee kwani kuna njia nyingi za kuzungumzia hivyo akimaliza utaomba mwongozo.’’

Alisema kuwa katika suala lile yeye (Werema) akiwa Mwanasheria Mkuu, ndiye mwenye dhamana ya kulisemea jambo hilo.

Kauli za Wabunge wa Chadema
Wabunge wengi wa Chadema katika kuchangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi walisisitiza kwamba maandamano lazima yafanyike ili kudai haki ambazo zimekuwa zikiminywa na Serikali kwa kutumia vyombo vyake vya dola.

Mbunge wa Nyamagana, Highness Kiwia alisema kwake maandamano ni sawa na "mama na baba wa ubunge" wake akidai kwamba kama si maandamano asingetangazwa kuwa mshindi wa nafasi yake hiyo.

"Nataka mtambue kuwa bila ya maandamano, mimi Kiwia nisingetangazwa na kuwa mbunge maana hali ilikuwa ni mbaya kuliko mnavyofikiri na ndiyo maana mkitaja maandamano napata tabu sana kwa kuwa nayaona maandamano sawa na baba na mama," alisema Kiwia.

Mbunge huyo alisema kuwa maandamano ya Chadema yanawaamsha Watanzania kutoka katika usingizi mzito wa kuibiwa kwa rasilimali ya nchi ambayo kila siku wanadangwa na amani.

“Hata hayati Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliwahi kusema, ufisadi na rushwa wakati wa amani ni adui mkubwa kuliko wakati wa vita na hiyo ilikuwa ni hotuba ya Nyerere ya mwaka 1965 katika Bunge la Bajeti, sasa nasema haki ya mama lazima kupiga kelele hadi kieleweke."

"Wakati naingia katika chumba cha kujumlishia kura saa 1:00 jioni mwaka 2010, niliingia nikiwa mbunge tayari maana utaratibu wa kuweka matokeo vituoni ulikuwa ukinihakikishia hilo, lakini siku ya kwanza ilishindikana na siku ya pili wananchi wa Ilemela, (Mwanza) waliamua kuandamana kushinikiza mbunge wao atangazwe."

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje alisema kuwa yuko tayari kukamatwa na kuwekwa ndani wakati wowote, lakini maandamano ni lazima kwa Tanzania hadi kitakapoeleweka.

Mbunge mwingine aliyezungumzia maandamano ni Philipa Mturano Viti Maalumu (Chadema) ambaye alisema ukiukwaji wa haki za binadamu ni miongoni mwa mambo yanayochochea uwepo wa maandamano hayo.

Mturano alitoa mfano wa mtoto Juma Hamza (12), ambaye alipigwa risasi na polisi wa doria wa Kituo cha Chang'ombe, Dar es Salaam kwamba licha ya kuhusika kwao na tukio hilo wamemtelekeza.

"Haya ndiyo mambo ambayo yanasababisha watu waandamane, leo hii nasema ikiwa mtoto huyu hatapata huduma lazima nitahamasisha wananchi wa Temeke tuandamane hadi kwa waziri na yeye tumchukue twende naye Ikulu ili tukapate hela ya kumtibu mtoto huyu."

"Mtoto huyu picha yake inaonekana hapa kwenye gazeti ni kama amepoteza matumaini kwa sababu ana kidonda kikubwa kinachotoa usaha mwingi, jamani kama ni bahati mbaya kwa nini wanashindwa hata kumhudumia?"

Hata hivyo, kwa upande wake Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliponda kufanyika kwa maandamano akisema CCM hakiwezi kutishwa na maandamano kwani ni chama kilichokomaa kisiasa.

Alisema vyombo vya dola vinavyomilikiwa na umma lazima vifanye kazi yake na kwamba lazima wale wote wanaokaidi sheria wachukuliwe hatua.

"Sheria zipo kwa ajili hiyo, kama wewe unaambiwa twende kituoni halafu unakataaa ni dhahiri kwamba polisi watakulazimisha hivyo lazima usukumwe kidogo," alisema Lusinde.

Uchunguzi wa Mauaji
Katika hatua nyingine, Werema amekiri bungeni kwamba Serikali imekuwa dhaifu kwa kutochunguza vifo vya raia ambavyo vimekuwa vikitokea katika mazingira yenye utata na kuahidi kwamba taratibu zinafanywa ili uchunguzi ufanyike.

"Nakiri kwamba tulilegalega kidogo kwa kutofanya uchunguzi wa mauaji yaliyotokea bila kujua sababu zake, lakini tumejiandaa shughuli hiyo itaanza karibuni".

Alisema uchunguzi wa vifo hivyo utafanywa na Mahakama za Korona (Coroner’s Court) ambazo zilikwishaundwa tangu mwaka 2004 kwa Tangazo kwenye Gazeti la Serikali namba 252 la Julai 16, 2004.

"Jaji Kiongozi kwa kushirikiana na Jaji Mkuu waliwateua mahakimu wote wakazi kuwa makorona (viongozi wa Mahakama za Korona), hivyo watu wa kufanya kazi hii (ya uchunguzi) wapo. Tutatumia taarifa hizi zilizotolewa, ipo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora na yingine ili kujua nini hasa kilichotokea," alisema Jaji Werema.

Kwa muda mrefu Chadema kimekuwa kikishinikiza kufanywa uchunguzi wa mauaji kadhaa ambayo kinadai kuwa yalifanywa na polisi katika sehemu mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Arusha, Tabora na eneo la Mgodi wa Nyamongo mkoani Mara.

Lema, akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani juzi, alihoji sababu za kutoundwa kwa mahakama za uchunguzi wa mauaji hayo.

Alisema uundwaji wa mahakama hizo ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquest Act) Sura ya 24 na kwamba Waziri Mkuu wakati anahitimisha mjadala kuhusu Bajeti ya ofisi yake, alikubaliana na ushauri wa kambi ya upinzani kwamba Serikali itaanzisha mahakama ya kuchunguza mauaji hayo.

"Kambi rasmi ya Upinzani inachotaka sasa ni kuona utekelezaji. Je, ni lini waziri mwenye dhamana atatangaza uteuzi wa kuundwa kwa mahakama hiyo katika Gazeti la Serikali ili wauaji wahukumiwe? Tunataka uchunguzi ufanyike haraka ili haki itendeke mapema," alisema Lema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania, kifo chochote ambacho kimetokea katika mazingira ya shaka kinatakiwa kuchunguzwa. Uchunguzi huo ni pamoja ule wa kidaktari ili kubainisha sababu halisi ya kifo husika na hatua ya pili ni uchunguzi wa kimahakama kwa kutumia mahakama ya korona ili kujiridhisha kwamba kifo hicho hakijatokana na vitendo au sababu za kijinai.

No comments: