TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, July 19, 2011

Ngeleja:Tatizo la umeme ni la Serikali nzima

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema kwamba hawezi kujiuzulu kwa tatizo la bajeti yake kukwama bungeni akisema tatizo la umeme si lake peke yake, bali Serikali nzima. Ngeleja alisema jana mara baada ya kuahirishwa kwa Bunge juzi jioni kwamba: "Hilo sidhani kama ni muhimu.

Muhimu hapa ni kutekeleza maagizo na ushauri wa wabunge kwa Serikali. Wabunge wamesema wanataka umeme na jinsi Serikali inavyoweza kuja na mpango wa dharura wa kuondokana na giza." Alipoelezwa kuwa miongoni mwa mapendekezo ya wabunge ni kumtaka ajiuzulu ili kupisha watu wengine wenye uwezo wa kuongoza wizara hiyo, alisema hilo kwa sasa siyo kipaumbele na kwamba kujiuzulu kwake hakuwezi kusaidia kuondoa tatizo lililopo.

"Tunakwenda kujipanga upya na baada ya wiki tatu tutarudi na majibu mazuri kwani tatizo ni fedha kidogo ambazo zilitengwa kwa ajili ya wizara yangu, sasa si mmemsikia Waziri Mkuu, (Mizengo Pinda) ameshasema nyie tupeni nafasi tunakwenda kutekeleza hayo," alisema Ngeleja na kuongeza:

"Bajeti ni ya Serikali si ya wizara ya nishati pekee, hivyo mimi si kwamba ndiye niliyetenga fedha hizo zinazosemwa kwamba hazitoshelezi, lakini hayo si muhimu kwa sasa, muhimu ni kwamba tumepewa fursa nyingine tunakwenda kukaa ili kuona jinsi tunavyoweza kutoka hapa." Shinikizo la kumtaka Ngeleja aachie ngazi lilitokana na kikao cha wabunge wa CCM ambao walikutana juzi mchana na kudai kwamba waziri huyo amewatia aibu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kiasi cha kuilazimisha Serikali kuondoa bajeti yake bungeni.

Juzi, Pinda aliondoa hoja ya Waziri wa Nishati na Madini Bungeni akisema hatua hiyo inatokana na hoja nzito zilizotolewa na wabunge wakitaka Serikali kuwasilisha bungeni mpango unaotekelezeka wa kuliondoa taifa gizani kutokana na mgawo wa umeme unaondelea.

Mkulo atema cheche Akizungumzia suala hilo la kujipanga upya na kuja na bajeti bora zaidi itakayokuwa na majibu juu ya tatizo la nishati, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema jana kwamba: "Waziri Mkuu hakusema kwamba tutaongeza bajeti kwa ajili ya kupatikana kwa umeme, bali alisema tutatafuta njia za kuondokana na tatizo la umeme nchini. Njia za kutatua mgawo wa umeme uliopo ni nyingi siyo lazima uongeze fedha za uwekezaji mpya."

Mkulo alisema anaishangaa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushindwa kuweka katika bajeti yao njia zisizohitaji fedha za umma kuwekeza ambazo zinaruhusu uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta hiyo. "Tulipitisha hapa bungeni Sheria ya PPP, yaani Public Private Patnership (Ushirikiano wa Sekta za Umma na Binafsi), hii inaruhusu sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya umeme," alisema Mkulo na kuongeza:

"Ngoja nikwambie, mimi nilikuwa China siku chache zilizopita, pale kuna makampuni manne yako tayari kuja Tanzania kuwekeza bila hata Serikali kutoa senti tano halafu wauze umeme wao Tanesco, sasa hapo si lazima Serikali itoe fedha za mtaji". Mkulo alisema uwekezaji wa Serikali katika uzalishaji wa umeme unaongeza mzigo kwa watumiaji wa nishati hiyo na kwamba ingekuwa vyema Wizara ya Nishati ikatumia mfumo wa kuruhusu wawekezaji ambao wanakuja na mitaji yao. "Tukitumia njia hii, suala la umeme tunaweza kuondokana nalo katika muda mfupi tu usiozidi miezi minne,"alisema
Mkulo.

Mgogoro wa Kanuni
Kuondolewa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kunaashiria mgogoro wa kikanuni baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana juzi jioni chini ya Uenyekiti wa Spika wa Bunge, Anne Makinda kushindwa kukubaliana jinsi ambavyo hoja hiyo itarejeshwa bungeni baada ya kuondolewa chini ya Kanuni ya 69 (1) na 69(2). Kwa mujibu wa marekebisho ya tatu ya ratiba ya Bunge la Bajeti yaliyofanywa juzi jioni na ratiba mpya kutolewa jana, hoja ya Wizara ya Nishati na Madini iliyoondolewa juzi, sasa itajadiliwa Jumamosi, Agosti 13, 2011.

Habari kutoka katika kikao hicho kilichofanyika mara tu baada ya Bunge kuahirishwa juzi jioni, suala la jinsi ya kuwasilisha upya hoja hiyo liliibuliwa na baadhi ya wajumbe na kwamba Spika alisema hoja hiyo itaanza kwa mawaziri husika kuwasilisha maelezo ya mpango wa dharura wa kukabiliana na uhaba wa umeme. Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya waziri kuwasilisha mpango huo, ataendelea kujibu baadhi ya hoja za wabunge na baadaye Bunge litakaa kama kamati ili kupitisha bajeti hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina walitofautina na msimamo huo wa Spika. "Spika alisema hivyo ingawa mimi sikubaliani naye, hapa kuna mgogoro wa kikanuni kwani kanuni hazisemi kitu jinsi ya kurejeshwa kwa hoja iliyoondolewa bungeni," alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi.

Spika Makinda hakupatikana jana kutoa ufafanuzi wa suala hilo kwani alikwenda Kongwa kuhudhuria mazishi ya bibi mlezi wa Naibu Spika, Job Ndugai. Kutokana na utata huo wa kikanuni hueda Spika akafuata utaratibu uliotumiwa na mtangulizi wake, Samuel Sitta, Julai 2009 wakati Serikali ilipolazimika kuondoa bungeni Bajeti ya Wizara ya Miundombinu wakati huo baada ya wabunge kuikataa.

Mgogoro wa 2009 Julai 2, 2009 aliyekuwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Phillip Marmo alilazimika kuondoa bungeni hoja ya Wizara ya Miundombinu baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo kuwasilisha mapendekezo ya kufanya marekebisho makubwa. Waziri wa Miundombinu wakati huo, Dk Shukuru Kawambwa alikuwa amewasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake lakini wabunge wakiongozwa na Diallo waliikataa wakidai kwamba rafu ilikuwa imechezwa katika mgawo wa fedha za ujenzi wa barabara nchini.

Kama ilivyokuwa katika Wizara ya Nishati na Madini juzi, wabunge wengi hawakuunga mkono hotuba ya Dk Kawambwa na kushinikiza yafanyike mabadiliko makubwa ambayo yaliifanya Serikali kuondoa hoja yake na kwenda kujipanga upya.

Hoja ya Diallo ilikuwa ikisababisha kuwepo kwa mabadiliko ya matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha, hivyo Spika Sitta aliielekeza Serikali kukutana na Kamati ya Miundombinu ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Mohamed Missanga ili kufikia mwafaka. Bajeti hiyo ilipitishwa Julai 4, 2009 siku ya Jumamosi na ikipata wakati mgumu kutokana na maoni mengi yaliyoibuliwa na wabunge wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi, chini ya Mwenyekiti Sitta.

Kabla ya Bunge kukaa kama Kamati ya Matumizi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Missanga, alisoma taarifa ya kamati yake kuhusu hoja ya Diallo ya kufanya mabadiliko katika matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2009/10.

Katika mchakato huo, Diallo alipewa nafasi ya kutosha mbele ya Kamati na baadaye Waziri Kawambwa kutoa maelezo ambayo yaliwezesha Bunge na Serikali kukubaliana jinsi ya kutatua mgogoro uliokuwepo wakati huo. Kutokana na uzoefu huo, upo uwezekano mkubwa kwa Spika Makinda kuamua kuipa nafasi Kamati ya Bunge ili itoe maoni kuhusu mpango mpya wa Serikali katika kukabiliana na tatizo la umeme kabla ya Bunge kukaa kama kamati na kupitia bajeti hiyo kwa vifungu.

Kadhalika, upungufu wa kanuni unaojiokeza sasa unaashiria kuwapo kwa umuhimu wa kanuni hizo kupitiwa upya, ili kukidhi matakwa ya kimatukio yanayojitokeza sasa hivyo kumpa nafasi kubwa Spika kuamua jambo "kadri anavyoona inafaa".

No comments: