TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 21, 2011

Makinda asubiri barua ya Rostam na CCM

Spika wa Bunge, Anne Makinda,

UAMUZI wa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM, unaonekana kukitesa chama hicho kutokana uongozi wake hadi sasa kushindwa kuandika barua Ofisi ya Bunge kumjulisha hatua ya mbunge wake huyo.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliliambia gazeti hili jana kuwa ofisi yake haikuwa imepata barua ya CCM hadi jana na kuongeza, "Sisi tungepata tungetangaza mara moja bungeni na kisha tungeiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)".

Kwa mujibu wa Makinda, kiutaratibu mbunge anapojiuzulu, chama chake ndicho kinachopaswa kumjulisha Spika kwamba, kiti cha ubunge katika jimbo husika kiko wazi.Spika Makinda alikiri kupata barua ya Rostam, lakini hiyo haiwezi kuwa kigezo cha kutangaza kiti hicho kuwa kiko wazi kwani katiba inataja chama kuwa ndicho kinachopaswa kuliarifu Bunge.

Awali Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema, "Ofisi yangu bado haijapata taarifa rasmi za maandishi kuwa amejiuzulu (Rostam)! Hiyo ina maana bado tunamtambua kuwa ni mbunge." Joel alisema kwa mazingira hayo, Rostam bado anapata haki zake za kiubunge ikiwa ni pamoja na mshahara.

Alifafanua kwamba hata angefika bungeni na kusaini mahudhurio, angepatiwa posho kama ilivyo kwa wabunge wengine.Kwa mujibu wa Joel, Ibara ya 71(f) ya Katibu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza kuwa mbunge atakuwa amepoteza nafasi hiyo iwapo ataacha uanachama wa chama kilichompa kofia hiyo.

Lakini ibara hiyo hiyo kifungu cha (C) kinalipa Bunge madaraka ya kumuengua mbunge kwenye nafasi hiyo iwapo hatahudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika."Ibara hiyo hiyo kipengele cha (g) kinazungumzia kuhusu nafasi kuwa wazi iwapo mbunge amefariki au kujiuzulu," alisema Joel.

Lakini, suala la kujiuzulu kama lilivyoelezewa kwenye kipengele hicho halijafafanuliwa kwa undani hivyo ofisi ya Bunge lazima itumie busara za kisheria katika kuamua.

CCM wapata ganzi kulijulisha Bunge

Sekretarieti ya CCM imepata ganzi kuandika barua hiyo huku viongozi wake wakirushiana mpira katika kuzungumzia suala hilo.Jana Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alishindwa kuzungumzia suala hilo alipotafuta na gazeti hili akieleza kuwa alikuwa kwenye kikao.Mukama alitoa sababu hiyo hata baada ya kupigiwa simu kwa zaidi ya saa tano.

Hii si mara ya kwanza kwa Mukama kukata simu punde anapoulizwa kuhusu suala la Rostam kujiuzulu ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec).Majira ya asubuhi jana, mwandishi wa blog hii aliyefika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Dar es Salaam, alizuiwa na katibu muhutasi kukutana na Mukama.

“Wewe na mhariri wako mnaonekana hamjui suala hili mtalifuatilia wapi, hii sio sehemu husika ya kufuatilia barua ya Rostam,”alisema Ramadhani Gabriel, katibu muhutasi wa Mukama.

Nape akwepa jukumu
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, alipopigiwa simu kuulizwa juu ya suala hilo, alisema “Ndio naingia ofisini nitakupa majibu baadaye nitakapopata taarifa hizi.”

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Kapteni John Chiligati alisema, "Katibu Mkuu alishatoa tamko kwamba amepokea barua ya Rostam."

Hata hivyo, Chiligati alipotakiwa kueleza lini barua hiyo itapelekwa kwa Spika wa Bunge alijibu,"taarifa hizo aulizwa Katibu Mkuu mwenyewe."

Habari za ndani zimeeleza kuwa CCM imechelewa kutoa taarifa hiyo kwa spika kwa sababu ilipata mshituko kutokana na hatua ya Rostam kuachia ujumbe wa Nec hadi ubunge.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, CCM ilitegemea Rostam angejiuzulu ujumbe wa Nec pekee, lakini hatua yake ya kujiuzulu na ubunge imekishtua chama hicho na hivyo kulazimika kuhaha kunusuru hali hiyo kwani kuna uwezekano Jimbo la Igunga likawa na upinzani mkubwa uchaguzi mdogo utapoitishwa.

No comments: