TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 7, 2011

Mpambano wa Lowassa na Serikali ya Jakaya sasa wazi
HATIMAYE mvutano wa makundi ndani ya CCM vilivyojitokea wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, sasa umedhirisha wazi kuwapo kwa vita ya kisiasa kati ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Hii inatokana ukweli kwamba, haijawahi tokea katika historia ya CCM na Tanzania kwa ujumla kuingia katika malumbano ya wazi namna hiyo.Watanzania walizoea kusikia mvutano wa chini kwa chini ambao baadaye ulimalizwa ndani ya chama bila wahusika kuvutana hadharani kama ilivyotokea sasa kati ya Lowasa na Serikali.

Majibu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kauli ya Lowassa bungeni kuwa Serikali inaogopa kufanya uamuzi mgumu, yanadhirisha kuwapo kwa vita hiyo ya kisiasa.

Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika utawala wa Awamu ya nne wa Rais Kikwete, alisema Serikali inasumbuliwa na ugonjwa wa woga katika kutoa uamuzi mgumu na matokeo yake mambo mengi hayaendi kama yalivyopangwa, hivyo kuitaka ibadilike.

Akijibu hoja mbalimbali zilizojitokeza bungeni wakati wa kujadili bajeti ya ofisi yake waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inazingatia na kutoa maamuzi magumu wa umakini na uhakika.

Hata hivyo baadhi wachambuzi wa mambo ya siasa nchini walisema kauli ziliyotolewa na Lowassa na majibu ya Pinda kwa niaba ya Serikali kuwa ni vita ya kisiasa baina ya pande hizo mbili iliyotoka ndani ya chama tawala (CCM).

Wakizungumza na blog hii jana, kwa nyakati tofauti, wasomi na wachambuzi wa siasa nchini walisema hali hiyo ni vita mpya kati ya Lowassa na Serikali ya Kikwete.

Walisema malumbano hayo ni matokeo ya makundi ndani ya chama hicho yaliyosababishwa na Uchaguzi Mkuu wa 2010 na maandalizi ya uchaguzi wa 2015 ambayo ni vita ya kisiasa.

Mmoja wa wachambuzi hao, Dk Bashiru Ally, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alismea malumbano haya yanaashiria kuwa hali ya nchi kisiasa kwa sasa si nzuri.

Bashiru alisema ni jambo la kushangaza watu kutojitokeza kupiga kura kiasi cha kutosha wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, huku kilimo kikishindwa kuchangia pato la taifa pamoja na kushuka kwa kiwango cha ufaulu na elimu kwa ujumla.“ Yakitatuliwa hayo ndiyo maamuzi magumu yanayotakiwa kufanywa. Lowassa ni kada wa CCM, mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na ni mwanasiasa mkongwe, hivyo ni wazi kuwa anayoyazungumza anamaanisha,” alisema Bashiru.

Aliongeza; “ Tatizo hili linaweza kuwa limetokana na makundi, uchaguzi uliopita na pengine maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2015.”Alifafanua kwamba, uamuzi mgumu aliyosema Pinda si uamuzi mgumu na kusisitiza kuwa suala la Serikali kujenga shule za sekondari ni wajibu wake siyo uamuzi mgumu kama alivyosema Lowassa.

“ Alitakiwa atueleze jinsi ya kukomboa asilimia 80 ya Watanzania masikini na namna ya kulinda rasilimali za taifa zisiporwe na wajanja…, tena hiyo sio kazi ya Serikali ni kazi ya chama tawala,” alisema Bashiru.

Alisema ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma(Udom) pamoja na shule za kata hauwezi kuwa na faida kama wanaomaliza elimu wanakosa ajira.Alifafanua kuwa, uamuzi mgumu ni pamoja na Serikali kuwaacha wananchi watunge katiba yao kwa maslahi yao na nchi yao.

“ Baraza la Mawaziri kuvunjwa sio uamuzi mgumu, binafsi nasema Serikali haijafanya maamuzi magumu…, uamuzi gani mgumu unaofanyika wakati nchi ipo gizani” alisema Bashiru akihoji.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema ndani ya CCM kuna tofauti kubwa ya utoaji uamuzi huku akitolea mfano dhana ya kujivua gamba.

“ Hizi ni dalili za wazi za kutoelewana.., huko tunakokwenda CCM itapata matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kung’oka madarakani,” alisema Profesa Baregu.

Alisema ukosefu wa umakini unadhihirisha wazi kuwa anguko la utawala wa CCM linawadia huku akifananisha anguko hilo na vyama vikubwa vya siasa nchini Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Zimbabwe ambavyo vilianguka kwa kukosa umakini katika maamuzi yake.

Alisema uamuzi unaotakiwa kufanywa lazima uwe wa hekima na busara ili usije kuleta matatizo kwa taifa na wananchi wake.“ Kabla ya kufanywa kwa uamuzi kinachotakiwa kuangaliwa ni madhara yake, kwa kufanya hivyo ndiyo tutakwenda mbele,” alisema Baregu.

Mchambuzi mwingine wa siasa ambaye pia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa Lowassa anatakiwa kuomba likizo ili atafakari kabla ya kuzungumza, kwa kuwa iwapo utafanyika uamuzi mgumu yeye anaweza kuwa wa kwanza kuhukumiwa.

Alisema Lowassa alikuwa na nafasi yake ya kushiriki na kwamba, mbunge huyo wa Monduli (CCM), alitakiwa kueleza maamuzi aliyotaka yafanywe na Serikali na siyo kuishia kulaumu tu.

“Yeye mwenyewe alikuwa serikalini anajua kuwa kila uamuzi ni lazima upimwe kwanza…, yeye (Lowassa) alichukua uamuzi mgumu wakati akiwa Waziri Mkuu, lakini majibu yake aliyaona,” alisema Bana

Lowassa alisema ugonjwa huo ni hatari kwa uchumi wa taifa kwa kuwa kuthubutu ni msingi wa mafanikio katika nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi.”Heri uhukumiwe kwa kutoa maamuzi mabaya kuliko ulaumiwe kwa kushindwa kutoa maamuzi," alisema Lowassa.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Lowassa ilijibiwa juzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya matumizi ya ofisi yake na kueleza kwamba serikali imekuwa ikizingatia hilo kwa umakini mkubwa.

Pinda bila kumtaja Lowassa alisema hata hatua ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kulivunja Baraza la Mawaziri mwaka 2008 ulikuwa ni uamuzi mgumu.

Akianza kujibu hoja hiyo ya kuchukua uamuzi mgumu, Pinda alianza kwa kueleza mambo yaliyofanywa na serikali zote tatu zilizotangulia, awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu alizosema zilifanya uamuzi mgumu sana ambapo mengine hadi leo yamekuwa yakiinyima Serikali ya sasa baadhi ya fursa.

Akieleza yaliyofanyika katika awamu ya nne, Pinda alisema serikali imefanya uamuzi mgumu ikiwa pamoja na kuwafikisha baadhi ya waliokuwa mawaziri mahakamani jambo ambalo kabla halikuwahi kufanyika.

“…Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa ikifanya maamuzi magumu sana, … ni awamu hii ya iliyofanya uamuzi mgumu wa kuvunja Baraza la Mawaziri …,”alisema Pinda.

Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, ametangaza hatua ya kujivua gamba inayoelezwa pia kuwa ni uamuzi mgumu ukiwataka watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kutafakari na kuchukua hatia ya kujivua nyadhifa ndani ya chama.

Kwa mujibu wa CCM watuhumiwa hao walipewa siku 90 kujitafakari na kuchukua uamuzi wa kuachia ngazi kabla ya vikao vya chama havijaanza mwezi Julai na kutoa uamuzi.

Tayari baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho wamekutana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa na kuzungumza.CCM kupitia Katibu Mkuu wake Wilson Mukama imekiri kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kukutana na watu hao, kila mmoja kwa wakati wake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape, Nnauye naye alisema kuwa hatua ya kujivua gamba haitaishia ndani ya chama hicho pekee, bali itafika kwa watendaji wote wa Serikali.

No comments: