TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, July 25, 2011

MGOGORO NA MADIWANI WA ARUSHA WAELEKEA KUKIUA CHADEMA


KATIKA kile kinachoonekana ni kutafuta suluhu ya mgogoro wa madiwani wa Chadema katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amefika hapa juzi kwa lengo la kukutana nao. Hata hivyo, hakufanikiwa kwani alishauriwa kutozungumzia mgogoro huo kwa kuwa yupo katika ngazi ya Kamati Kuu ya chama hicho.

"Ni kweli Mbowe alikuwapo hapa tangu Jumamosi, lengo lake lilikuwa kukutana na madiwani hao lakini baadaye alishauriwa kuwa asifanye hivyo kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama," mmoja wa wabunge wa Chadema Kanda ya Kaskazini, alilieleza gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini na kuongeza:,

“Mwenyekiti yuko hapa, nadhani atakutana na madiwani wanaovutana na viongozi wa kitaifa akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kuhusu hatua yao ya kufikia muafaka na kukubali baadhi ya nyadhifa ndani ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Arusha,” alisema mtoa habari wetu kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Pamoja na mambo mengine, mwenyekiti huyo ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alitarajiwa kusikiliza hoja za madiwani hao na kujadiliana nao kutafuta njia nzuri na sahihi za kuchukua badala ya kutunishiana misuli na vikao vya uamuzi, kama ilivyojitokeza kwa walioamriwa kujiuzulu nyadhifa zilizopatikana kutokana na muafaka wa umeya wa jiji hilo.

Kikao cha CC ya Chadema kiliagiza madiwani waliopata nyadhifa za unaibu meya na uenyekiti wa kamati kujiuzulu nafasi hizo ndani ya siku tatu kufikia Julai 21, mwaka huu. Madiwani hao wakiongozwa na Estomih Mallah wa Kata ya Kimandolu na John Bayo wa Kata ya Elerai wamegoma kutekeleza agizo hilo na badala yake nao wakatoa masharti ya kuombwa radhi na Dk Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwa madai ya kudhadhalilishwa kwa tuhuma za kula rushwa ili kufikia muafaka huo na CCM.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, wakati jitihada za Mbowe zikigonga mwamba, mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amechukua hatua za makusudi kumaliza mgogoro huo kwa kuzungumza kwa nyakati tofauti na pande zote zinazovutana. Mtei amekutana na madiwani hao, Lema na uongozi wa Chadema kuzungumzia mgogoro huo akitaka pande hizo zinazovutana zimalize tofuati zao kwa busara.

Mtei alikutana na madiwani hao baada ya kumwomba afanye hivyo ili kuumaliza kwa amani badala ya kuvutana hadharani. Madiwani hao wa Chadema wilayani Arusha walikutana na Mtei nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya jiji la Arusha mwishoni mwa wiki na kuomba ushauri juu ya mvutano huo unaoendelea kukipasua chama hicho.

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Mtei hakukiri wala kukataa kukutana na madiwani hao. Alisisitiza kuwa Chadema hakiwezi kumeguka kutokana na mgogoro huo. "Sisi (Chadema) tuna mipango na sera zenye matumaini kwa Watanzania, hatuwezi kumeguka kwa mgogoro huo."

Hata hivyo, Mtei aliwataka viongozi wa Chadema, madiwani wake na Lema kutumia busara na kupunguza jazba katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

No comments: