TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 14, 2011

Lowassa: Nitasema yangu • Asikitishwa kujiuzulu Rostam, aahidi kuzungumza



WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa amesema kitendo cha Rostam Aziz kujiuzulu ubunge wa Igunga (CCM) na Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Akizungumza na Tanzania Daima nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana, Lowassa alisema, “Nimesikitishwa na kitendo cha kujiuzulu kwa Rostam, hasa pale wananchi wake walipokuwa wakimlilia,” alisema Lowassa huku akiondoka.

Hata hivyo alipotakiwa kueleza iwapo atakuwa tayari kujiuzulu kwa kuwa ni miongoni mwa wanaotajwa na viongozi wa sekretarieti ya CCM kwa tuhuma za ufisadi, alisema atazungumza wakati wake utakapofika.

“…Nitazungumza wakati ukifika,” alijibu kwa kifupi Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli.

Aidha, juhudi za gazeti hili kumpata Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), ili azungumzie suala hili kwa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa (gamba) ndani ya chama chake ziligonga mwamba baada ya kupata taarifa kutoka kwa chanzo cha kuaminika kwamba mbunge huyo yuko safarini nchini Uingereza.

Katika hatua nyingine Bunge limesema halina taarifa ya kujiuzulu kwa Rostam. Kauli hiyo ilitolewa na Spika Anne Makinda, baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, kuomba mwongozo wa kiti cha spika kuhusu suala hilo.

“Nimeona kama mlivyoona ninyi, ukifika wakati nitawaambia lakini mpaka sasa ofisi yangu na Bunge haijapata taarifa,” alisema Spika Makinda.

Viongozi wengine wanasemaje?

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa, ameitaka serikali kumfikisha mahakamani Rostam kwa tuhuma za ufisadi zinazomwandama baada ya kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi ndani ya CCM.

Alisema kujiuzulu kwa mbunge huyo ni mchezo wa CCM kwa kushirikiana na serikali yake ili kubadili upepo wa wananchi wanaotaka watuhumiwa wote wa ufisadi kufikishwa mahakamani.

Dk. Slaa ameshangazwa na hotuba ya Rostam kwa wazee wa Igunga na waandishi wa habari iliyoelezea sababu za kujiuzulu kwa kuwa ni kuchoshwa na siasa uchwara ndani ya chama chake ambazo zinaathiri biashara zake.

“Mchezo huu wa CCM kuwataka mafisadi wajivue gamba kwa kuachia nafasi walizonazo ndani ya chama chao kwa Rostam wamefanikiwa…tunataka na wengine wafuate, lakini suala linabaki pale pale kuwa wanazo tuhuma za ufisadi ambazo lazima zichukuliwe hatua za kisheria,” alisema Dk. Slaa.

Bila kutafuna maneno, Dk. Slaa alisema, “Kama Rostam amethubutu kusema kuwa kujiuzulu kwake kutamsaidia kufanya biashara zake vizuri ina maana hata alipokuwa kiongozi hakuwatumikia vema anaowaongoza, alikuwa akitizama biashara zake… hata hivyo nampongeza kwa kuchukua hatua na kujisafisha ndani ya chama chake.”

Wakati kiongozi huyo wa CHADEMA akizungumza hayo, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amepongeza uamuzi wa kujiuzulu kwa Rostam.

Akizungumza kwa njia ya simu, Butiku alisema hakuna haja ya kubeza uamuzi huo kwa vile mbunge huyo wa Igunga aliyeachia ngazi amefanya hivyo akitii dhamira yake ya kuachana na siasa uchwara ili kuendeleza biashara zake.

Alisema amezingatia hali ya siasa iliyoko ndani ya CCM, kutokana na kusukumwa na dhamira yake; ni jambo la kupongezwa si kwa chama bali hata kwa taifa.

“Ametoa sababu iliyomsukuma kufanya hivyo kama alivyodai kuwa ni siasa uchwara iliyopo; hivyo hawezi kuendelea kujihusisha na siasa ya namna hiyo basi acha aondokane na siasa ya namna hiyo…tukubali uamuzi wake,” alisema.

Butiku alisema kuwa cheo na uongozi ni dhamana hivyo si wa kwanza kuchukua maamuzi hayo kwani walikuwepo wengi miaka ya nyuma kama Mtei, Abuu Jumbe na wengine ni jambo jema linalomjengea heshima ndani na nje.

Alisema kuwa hivyo atakumbukwa kwa kuwa amekisaidia chama kwa sehemu yake hasa kutokana na kuwa kiongozi na kushika nyadhifa mbalimbali hivyo anapaswa kupongezwa hasa kutokana na ujasiri huo aliouonyesha.

“Kama maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anaona yalichakachuliwa basi huo ndiyo aliouita ni siasa uchwara hivyo hana budi kufanya biashara zake,” alisema Butiku aliyekuwa msaidizi wa karibu wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Maombezi la Ubungo Kibangu (GRC), Antony Lusekelo, alisema kuwa tatizo la CCM si Rostam bali ni mfumo uliopo hasa ya dhambi ya ufitini ambayo inawamaliza kwa sasa.

Alisema iwapo watashindwa kutubia dhambi hiyo basi si ajabu chama hicho kikashindwa kupona katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Lusekelo akinukuu vifungu vya maandiko matakatifu alisema ‘Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo yake itavunjika ghafla’, hivyo chama lazima kiangalie mfumo unaowamaliza ya makundi ya kuwania urais kwa 2015.

Alisema katika chama hicho uchafu si wa watu wachache pekee bali zipo tuhuma nzito zinazowamaliza ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa nyumba za serikali ambapo aliwataka wale waliojiuzia nyumba hizo kutoandika urithi kwa vizazi vyao.

Aliongeza kuwa kama watashindwa kuachana na siasa hizo za ukatili na kuumizana si ajabu kabla ya uchaguzi mkuu makundi hayo yakaishia kuuana.

“Jambo kubwa ninaloliomba ni kuombea amani kwa kuwa Mungu hana chama wala dini bali ana taifa; inawezekana 2015 tukaongozwa na vyama vingine kutokana na CCM kuendekeza dhambi ya ufitini ambayo itawamaliza, alisema na kuongeza: “Ni rahisi ngamia kupita katika tundu la sindano lakini si kwa CCM kupona katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Lusekelo.

Wananchi wa kawaida

Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, wameitaka serikali kutaifisha mali za Rostam baada ya kujiuzulu ubunge kwa madai kuwa asilimia kubwa ya utajiri wake umetokana na kodi za wananchi kisha kumfikisha mahakamani.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana waliitaka pia serikali kuwashinikiza watuhumiwa wengine akiwemo Lowassa na Chenge kujiuzulu nafasi zao ili waweze kushtakiwa kwa kuisababishia serikali hasara.

Juma Hamis alisema uamuzi wa Rostam ulikuwa ukisubiriwa na baadhi ya wana CCM na kwamba kilichobaki ni kutaifisha mali zake kwa lengo la kuzirejesha serikalini.

Alisema zao la ufisadi bado halijaisha kwa kuwa watu watuhumiwa wengine wapo na wataendelea kukihujumu chama na serikali yake. “Mimi nashangaa watu wanasema pigo kwa chama wakati mtu mwenyewe ameshiriki katika ufisadi kwa kila kona hata kuondoka ni sahihi lakini bado kuna watu wengine tunataka wafanye kama alifanya Rostam,” alisema Hamis.

Naye Josephat Mbali alipongeza uamuzi wa Rostam huku akiwashauri wengine wanaohisi kuonewa ndani ya CCM kuiga mfano huo ili kukinusuru chama hicho tawala na kukirejeshea imani na heshima yake machoni pa Watanzania.

Kwa upande mwingine mjumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Augustino Matefu, ameitaka serikali kuwafilisi watuhumiwa wote wa ufisadi bila woga.

Alisema kujiuzulu kwa mbunge huyo hakutoshi, badala yake afilisiwe mali zake na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuwa ameiingiza serikali katika hali ngumu kiuchumi kutokana na maamuzi aliyopitisha akiwa kiongozi ndani ya chama tawala.

“Tunashangaa mpaka leo hawa Takukuru wapo wakati kuna watu kama hawa ambao wanatuhumiwa kila kukicha sasa kwa kuwa wameshajitathmini ni wakati muafaka wa kufikishwa mahakamani…tuanze na huyu Rostam,” alisema Matefu.

Juzi, Rostam alitangaza kujiuzulu ubunge wa Igunga na ujumbe wa NEC kwa maelezo kuwa amechoshwa na siasa uchwara zenye lengo la kuchafuana kwa chuki na visasi huku akisisitiza kwamba hakuna shinikizo la kujivua gamba katika maamuzi yake.

Rostam alitangaza hayo alipozungumza na wazee wa CCM Igunga na kuongeza kuwa amesukumwa na kashfa mbalimbali anazotuhumiwa kwa kiasi kikubwa ambazo pia zimemuathiri kibiashara na kifamilia.

Rostam amekuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 1994 na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM.

Habari hii imeandikwa na Betty Kangonga, Chalila Kibuda, Janet Josiah, Abdallah Khamis, Milembe Dashina (Dar) na Tamali Vullu (Dodoma).

No comments: