TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, July 9, 2011

Dk. Slaa arusha kombora CCM




• Adai imeandaa waraka mzito wa kuichafua CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kubaini mchezo mchafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaolenga kukihusisha chama hicho cha upinzani na utetezi wa mafisadi ili kudhoofisha mapambano ya CHADEMA dhidi ya mafisadi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, mchezo huo umetungwa na maofisa waandamizi wa CCM, wanaolenga kukigawa chama hicho kikuu cha upinzani ili kukisambaratisha.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema wamekamata waraka wa CCM unaodai wapinzani hao wamehongwa pesa na mafisadi ili kutibua njama za CCM kuwatimua.

“Waraka wenyewe umeandaliwa na Nape (Nnauye, ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM), baada ya kuona chama chao kimeshindwa kuwafukuza mafisadi. Sasa wanadai eti CHADEMA imepewa pesa zaidi ya sh bilioni tatu na mapacha watatu.

“Kwa mujibu wa waraka huo, inasemekana mapacha hao watatu walitupatia pesa hizo mwaka jana kabla ya uchaguzi ili kusaidia wabunge wa CCM ambao wangehamia CHADEMA, kwamba kama wangeshindwa uchaguzi pesa hizo zitumike kufidia gharama zao baada ya uchaguzi.

“Wanadai kwamba katika uchaguzi wa mwaka jana tulitumia sehemu ndogo ya pesa hizo, na sasa zilizobaki zinajulikana na Mbowe na mimi (Slaa). Hiki ni kichekesho kweli. Wanadhani wanaweza kuleta mgogoro na kutugombanisha kirahisi hivyo; wanapoteza muda wao.”

Dk. Slaa alidai kwamba mbinu hiyo chafu ya CCM inalenga kuhamishia CHADEMA mgogoro wa chama tawala baada ya kuona dhana yao ya kujivua gamba imewashinda kutekeleza.

Alisema watungaji wa waraka huo wanamshutumu yeye (Slaa) kwa kumnasua Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, katika orodha ya vigogo mafisadi.

Hata hivyo, yeye alisema hajatetea ufisadi wa Sumaye, na akasisitiza kwamba ni yeye aliyemtuhumu Sumaye bungeni kuhusu shamba la Kibaigwa alilokuwa analima huku likilalamikiwa na Magereza.

“Lakini Sumaye hayuko katika ufisadi mkubwa huu tunaouzungumzia unaolitafuna taifa. Kama mtu ana vielelezo vya ufisadi wake, ambavyo sijui, atuletee. Sisi tunapozungumzia ufisadi mkubwa hatumwoni Sumaye miongoni mwao, lakini haina maana kwamba tunalinda mafisadi.

“CHADEMA haitaacha vita ya ufisadi hadi hapo watuhumiwa watakapojisafisha. Wao kama wameshindwa kuvuana magamba, washindwe tu, lakini sisi tutaendelea kuwang’ang’ania hadi watakapoacha ufisadi,” alisema.

Alisema CHADEMA imeshtushwa na jitihada za serikali kuanza kuwasafisha mafisadi, hasa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, huku CCM ikimtaja kuwa mchafu na anayepaswa kuvuliwa nyadhifa za uongozi ndani ya chama hicho.

Akisisitiza kwamba CCM wanajikanganya wenyewe, hawana sababu ya kusukumia lawama CHADEMA, kwani chama hicho cha upinzani kimejipambanua kwa muda mrefu kuwa kinara wa vita ya ufisadi.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa CCM wamekuwa na tabia ya kuiandama CHADEMA kwa kashfa mfululizo za ukabila, udini na “ujinga” mwingine ambao chama hicho kimeupangua na kujihalalisha mbele ya umma.

Alisema hizi ni dalili za CCM kutapatapa baada ya kuishiwa hoja za kisiasa na kukosa mvuto kwa umma. Alisisitiza kwamba mbinu chafu hizi za CCM haziwezi kuinusuru wala kuisafisha mbele ya umma, na kwamba CHADEMA haitakatishwa tamaa na mbinu hizo chafu.

Blog hii ilipowasiliana na Nape kuhusu tuhuma hizo za Dk. Slaa, alisema maneno hayo si mageni masikioni mwa Watanzania, kwani kiongozi huyo amekuwa akiyazusha kila mara.

Alisema hajawahi kuandika waraka wala kumtuhumu Dk. Slaa, kwa kuwa ni mtu wa kawaida, hivyo hana muda wa kupoteza kwa ajili ya kiongozi huyo.

Nape aliongeza kama Dk. Slaa ameshindwa siasa ni bora arudi kijijini kwake akalime vitunguu kuliko kuendelea na jambo asiloliweza.

Kuhusu mapacha watatu, Nape alisema kuwa CCM haijashindwa kuwatimua mafisadi bali kinachosubiriwa ni kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambacho ndicho kitatoa hitimisho juu ya suala hilo.

“Hayo maneno ya kusema tumeshindwa kuwatimua mafisadi tumeshayazoea…sisi tunachojua NEC itakapokutana ndiyo itawawajibisha, sasa wanaharaka ya nini?” alihoji Nape.

Alisema Dk. Slaa amekuwa akiwazushia hadi wanachama wenzake ndani ya CHADEMA hata anapohitajika kutoa ushahidi anashindwa kufanya hivyo.

“Hiyo ni tabia yake Dk. Slaa, amekuwa akiwazushia hadi wenzake katika chama na pindi akibanwa aonyeshe ushahidi anashindwa kuonyesha nyaraka, hivyo tumeshamzoea katika hilo,” alisema.

No comments: