TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, July 9, 2011

CHUO CHAWAACHA SOLEMBA WANAFUNZI

ZAIDI ya wanachuo 140 waliokuwa wakichukua masomo ya uhasibu katika Chuo cha Tanganyika Christian University kilichokuwa kimekodi majengo ya madarasa katika Chuo cha Veta jijini hapa, wamedai kutelekezwa na wamiliki wa chuo hicho na kwamba hatima yao ya masomo hawaijui na wameiomba Serikali kuingilia kati.

"Tumeondoka chuoni tangu Juni 5 hatujui kinachoendelea, walimu waliokuwapo hawalipwi mishahara na wamiliki wanavyoonekana wamekitelekeza chuo tumelipa fedha za muhula wote huu wa mwaka huu, lakini tunashangaa walimu kukosa mishahara hadi siku nyingine tulipokuwa tukiingia madarasani walimu walikuwa hawaiingii kufundisha," alisema Mariam Kuppa mkazi wa Masiwani jijini hapa.

Alisema licha ya kutelekezwa, lakini tatizo kubwa lililowakumba ni ukosefu wa walimu wa kutosha ambao mmiliki wa chuo hicho waliyemtaja kwa jina moja la Lukindo, amekuwa akiwaahidi kuleta walimu wapya.

Mwanafunzi mwingine Neema Aloyce alisema Mei mwaka huu, walitakiwa kwenda Mombasa nchini Kenya kufanya ziara ya mafunzo na kwamba kila mwanafunzi alitakiwa kuchanga Sh 40,000, lakini safari hiyo haikufanyika licha ya kuchanga fedha.

Akizungumza kwa simu na, mmiliki wa chuo aliyejitambulisha kwa jina la Abraham Lukindo, alikiri kukifunga chuo kutokana na wanafunzi hao kushindwa kulipa ada.

Alisema kutokana na hali hiyo uongozi wa chuo ulishindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na suala la kuwalipa mishahara walimu na wafanyakazi wengine.

Alisema chuo chake kilikuwa na wanafunzi 140 ambapo 70 kati ya hao walikuwa wakisoma bure bila kulipa malipo yoyote kutokana na kwamba walipokelewa kwa kigezo cha watoto yatima na wengine 70 waliobaki walikuwa wakilipa lakini tangu Januari hadi Mei mwaka huu ni wanafunzi watano tu ndiyo waliokuwa wamelipa ada ya chuo hicho.

"Ni kweli chuo tumekifunga wanafunzi hawataki kulipa ada, pale tulikuwa na wanafunzi 140, na wanafunzi 70 kati ya hao ni yatima waliokuwa wakisoma bure na wengine walitakiwa kulipa ada, lakini hivi ninavyoongea na wewe ni wanafunzi watano tu ndiyo waliolipa tangu Januari hadi sasa.

No comments: