TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, July 22, 2011

DAVID JAIRO APEWA LIKIZO YA LAZIMA NA IKULU

Philemon Luhanjo

IKULU imetangaza rasmi kushughulikia tuhuma za rushwa zinazomkabili Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, baada ya kumpa likizo yenye malipo na kumkabidhi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kazi ya kumchunguza ndani ya siku kumi.

Kwa muda wa siku tano sasa Jairo amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari nchini na kuibua mjadala mzito, baada ya mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo, kuibua tuhuma nzito bungeni dhidi yake, akisema alitoa dokezo la siri kwenda kwenye taasisi za chini za wizara hiyo akizitaka zichangie Sh50 milioni ili kufanikisha kupitishwa kwa bajeti yao.

Hata hivyo, jana sakata hilo liliingia katika hatua ya juu zaidi baada ya Ikulu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza hatua hizo dhidi ya Jairo, kipindi ambacho tayari wanasheria, viongozi wa dini na wasomi, wakitaka mtendaji huyo ajiuzulu au awajibishwe na Rais ambaye ndiye aliyemteua, baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuutua mzigo.

Luhanjo ambaye ni Mkuu wa Utumishi wa Umma, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba, Jairo ambaye yuko chini yake, analazimika kwenda likizo kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa mujibu wa sheria zinazoongoza utumishi wa umma.

"Nimeanzisha uchunguzi wa awali (Preliminary Investigation) kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo. Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini amepewa likizo ya malipo kupisha uchunguzi wa awali (Relieve of duties administratively pending preriminary investigation)..., hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye zitategemea matokeo ya uchunguzi huo wa awali," alifafanua Luhanjo.

Licha ya mchakato wa hatua dhidi ya mtumishi huyo wa umma ambaye ni mteule wa Rais kupitia katika mchakato mrefu, mwisho wake unaweza kuwa kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara, kufukuzwa kazi, kuachishwa kazi au kurejeshwa kazini kwa kutegemea matokeo ya taratibu zitakazofuatwa.

Akionyesha msisitizo wa mchakato huo, Luhanjo alisema “Jairo analazimika kwenda likizo kutokana na uzito wa tuhuma dhidi yake na kuongeza, zingekuwa ni tuhuma nyepesi ningeruhusu aendelee na kazi wakati uchunguzi huo wa awali ukifanyika, lakini tuhuma hizi ni nzito mno, hivyo lazima aende likizo ili kupisha uchunguzi huo."

[Mr David Jairo]

Mr David Jairo
Akiweka bayana namna uchunguzi huo utakavyofanyika, Luhanjo, alisema uchunguzi dhidi ya Jairo kwa kuwa unahusu masuala ya fedha, utafanywa na Ofisi ya CAG, ambayo inatakiwa kukamilisha kazi yake katika muda wa siku kumi kisha kuwasilisha kwake matokeo ya uchunguzi huo kwa hatua zaidi.

Hata hivyo, tayari pia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, aliweka bayana kwamba taasisi yake imezichukulia kwa uzito wa pekee tuhuma hizo za kutaka kuhonga wabunge, ambazo ni moja ya sababu za kuahirishwa kwa Bajeti ya Nishati na Madini hadi baada ya wiki tatu.

Jairo anakabiliwa na tuhuma za kuwaandikia barua wakuu wa idara zote zilizoko chini ya wizara yake, ili watoe fedha kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, fedha ambazo zinatafsiriwa kwamba zililenga kutoa rushwa kwa wabunge.Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo ndiye aliyemlipua Jairo bungeni Julai 18, 2011 wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini na kwamba amekusanya fedha kiasi cha Sh1 bilioni kutoka idara 21 zilizopo chini ya Wizara yake, fedha zisizo na maelezo.

Hatua dhidi ya Jairo
[David Jairo]

David Jairo
Luhanjo alisema ikiwa uchunguzi wa CAG utabaini Jairo ana makosa ya kinidhamu, atapewa taarifa za tuhuma husika (Notice) ambayo itaambatana na hati ya mashtaka (charge), ambayo itaeleza kwa kifupi makosa hayo na jinsi makosa hayo yalivyotendekea."Taarifa ya tuhuma itatoa maelezo kuhusu lini mtuhumiwa anapaswa awe amejibu tuhuma hizo, na katika kipindi hiki mtuhumiwa atasimamishwa kazi na kulipwa nusu mshahara,"alisema Luhanjo.

Katibu Mkuu Kiongozi alisema ikiwa atapelekewa tuhuma hizo, Jairo atalazimika kujibu kwa kukubali au kuzikataa na kwamba ikiwa atakubali mamlaka ya nidhamu ambayo kwa mujibu wa sheria ni Katibu Mkuu Kiongozi, yanaweza kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.

"Kama mtuhumiwa amekanusha au amekana, mamlaka ya nidhamu itaunda kamati ya uchunguzi ambayo itapewa hadidu za rejea, ambazo pamoja na mambo mengine itaeleza lini uchunguzi huo unapaswa kukamilika,"alisema Luhanjo na kuongeza:

"Taarifa ya Kamati itawasilishwa ikiwa kwa Mamlaka ya Nidhamu ikiwa ni mapedekezo. Ikumbukwe kuwa Kamati hii haitoi adhabu kwa watuhumiwa isipokuwa inatoa mapendekezo tu".

Kwa mujibu wa Luhanjo, mamlaka ya nidhamu itaendelea kutoa adhabu kwa mujibu wa Sheria ya Umma na kanuni zake kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati ya uchunguzi na kwamba iwapo adhabu ni kuvuliwa madaraka, mamlaka ya nidhamu italazimika kuwasiliana na mamlaka ya uteuzi ambaye ni Rais.

"Kama mtuhumiwa hataridhika na unaoishia kwa Mamlaka ya Nidhamu, Sheria na Mamlaka ya Umma na Kanuni zake zinampa fursa ya kukata rufaa kwa Rais.Rais ana Mamlaka ya kuthibitisha au kukataa uamuzi wa Mamlaka ya Nidhamu,"alisema Luhanjo.

Kauli za Pinda
Akizungumza wakati wa kuondoa bungeni hotuba ya makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini Julai 18, mwaka huu baada ya bajeti hiyo kuwa imekataliwa na wabunge, Pinda alisema alikuwa akifanya utaratibu wa kuwasiliana na Rais Kikwete aliyekuwa safarini Afrika Kusini ili kupata ridhaa ya kuchukua hatua dhidi ya Jairo.

"Kikwazo pekee nilichokipata ni kwa sababu Rais hajatua South Africa (Afrika Kusini) na mwenye mamlaka ya kuteua Makatibu Wakuu ni Rais mwenyewe. Nikatamani sana nije hapa mimi niwaambieni nimeishachukua hatua, nimeamua hivi. Lakini, nikaambiwa utakuwa unaingia katika maeneo ambayo si ya kwako,"alisema Pinda na kuongeza:

"......kwa hiyo, kwa hili, naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa dhati kabisa, kwamba kwa sababu sina mamlaka juu ya mtu huyu ya kumtimua kazi leo au kumwambia ondoka, mwenye mamlaka ni Rais mwenyewe, kwa hili mnipe baraka zenu, akifika South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo mimi nitawasilisha maelezo haya kwake".

Siku moja baadaye Pinda aliliambia Mwananchi kuwa alikuwa amepewa maelekezo mapya na Rais Kikwete ambayo hata hivyo, hakuwa tayari kuyataja.

Lakini, juzi Pinda aliwaambia waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge kwamba suala la kuwajibishwa kwa Jairo kama wanavyotaka wabunge lilikuwa likimsubiri Rais Kikwete arejee kutoka Afrika Kusini.
"Tumemuarifu, amelisikia sasa jamani mnataka afanye uamuzi huu akiwa huko mbali? Amesema akirudi tutakaa na kuangalia jinsi ya kuchukua hatua,"
alisema Pinda.

Jairo bungeni
Mapema wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jana, Mbunge wa Tumbe (CUF), Rashid Ally Abdallah, alihoji sababu za Jairo kushindwa kuchukuliwa hatua na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal ambaye anatakiwa kutekeleza majukumu wakati Rais akiwa hayupo.

"Kwa mujibu wa Ibara ya 47(1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Makamu wa Rais anatakiwa kuchukua mamlaka wakari Rais akiwa hayupo, tarehe 19 Julai mwaka huu Waziri Mkuu alisema hawezi kuchukua hatua dhidi ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini hadi Rais awepo, je huoni kwamba ni kukiuka katiba,?",alihoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema pamoja na kwamba katiba inaruhusu Makamu wa Rais na hata Waziri Mkuu kukaimu nafasi ya Rais pale yeye anapokuwa hayupo, alisema kuna vifungu vingine vya katiba vinaweka ukomo wa kufanya uamuzi kwa watu wanaokaimu.

"Kweli hicho kipengele kinasomeka hivyo, lakini zipo sheria na vifungu vingine vya katiba ambavyo vinaweka wazi kwamba sisi tunaopata fursa hizi za kukaimu tufike wapi, si kwamba ukiachiwa ofisi basi unaanza kufanya kila kitu, eti leo nianze kusamehe wafungwa, hili haliwezekani,"alisema Pinda.

Pinda alisema lengo la ukomo wa uamuzi kwa watu wanaokaimu nafasi ya Rais ni kulinda dhana ya uwajibikaji kwani lazima awepo mtu wa kuwajibika au kuulizwa pale unapokuwa umefanyika uamuzi mkubwa wa masuala yanayohusu nchi.

No comments: