TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, June 24, 2011

Zitto sasa awalipua Mawaziri, adai wameshawishiwa


Zitto Kabwe akisisitiza jambo Bungeni mjini Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe(Chadema) jana alichafua hali ya hewa bungeni na kuzua mvutano mkubwa kati yake na mawaziri baada ya kueleza kuwa baraza la mawaziri limeshawishiwa na watu kulifuta Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa faida ya wachache.

Zitto alitoa kauli hiyo iliyomgharimu na kutakiwa kuithibitisha ifikapo Juni 29 mwaka huu, wakati akichangia azimio la serikali la kuongeza muda wa uhai wa shirika la hilo lililosomwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo.

Akiwa mchangiaji wa kwanza katika mjadala huo, uliosomwa baada ya kipindi cha maswali na majibu, Zitto alirudia mara tatu kauli hiyo na kuwataka wabunge wasikubali kupitisha azimio hilo kwa kuwa ni 'wizi kwa rasilmali za taifa'.

"Hoja ya kuliongezea muda CHC wa miaka mitatu na baada ya hapo lifutwe na kazi zake apewe Msajili wa Hazina (TR) sio bure, baraza la mawaziri limeshawishiwa ili watu fulani wanufaike," alisema Zitto na kuongeza:

"Mapendekezo hayo yaliletwa kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na kwenye Kamati ya Fedha na Uchumi na zote ziliyakataa... Tukasema CHC iongezewe muda zaidi ili ifuatilie madeni na mali za mashirika kadhaa ambayo zimeonekana kuliwa.

"Ukitaka kuifuta leo, Mheshimiwa Spika, madeni ya mashirika ya umma yatapotea na naamini kuna watu wanafurahia jambo hilo kwani watanufaika. Tumewaagiza CHC wafuatilie madeni hayo, halafu hata kabla hawajaanza kazi, tunasema tunataka kulifuta baada ya miaka mitatu, siyo sahihi CHC ni jicho letu la kufuatilia ubadhirifu katika mashirika ya umma."

"TR (Msajili wa Hazina) ana majukumu mengi na tayari tumeona ameshindwa kufuatilia mashirika mengi. Kuna mashirika 25 na taasisi zingine kadhaa hana hati ya mashirika hayo wala hajui mali. Unawezaje kumwongezea majukumu kama huo siyo mpango wa watu kutaka kutuhujumu?"

"Naombeni waheshimiwa wabunge kwa umoja wetu, bila kujali tofauti za itikadi zetu, tulikatae azimio hili, limeletwa baada ya mawaziri kupitiwa na ma-lobbyist(washawishi). Halina manufaa kwa taifa, ni wizi na uporaji wa mali ya umma. Tuliliagiza shirika hilo lisaidie kufuatilia ubadhirifu kwenye mashirika ya umma, sasa leo tunataka kuiondoe hope (matumaini )yote kwa azimio hilo! Tusikubali,"

Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kapteni George Mkuchika alisimama na kuomba mwongozo wa spika, kisha akasema: "Mheshimiwa spika, natumia kanuni inayozuia mbunge kutoa maneno ya kuudhi na lugha chafu bungeni."

Mimi ni mjumbe wa baraza la Mawaziri, sijafikiwa na mtu na pia naamini hakuna mmoja wetu aliyepitiwa. Mheshimiwa Zitto umetudhalilisha wabunge wenzio. Spika naomba mwongo wako."

Spika Anne Makinda akasema, "Waheshimiwa wabunge, kwa kuwa azimio hilo limekuja kwa dharura, naomba kwanza tusiingize mambo ambayo yatachelewesha utekelezaji wake. CHC inatakiwa kufa ifikapo Juni 30, sasa leo tupitishe kwanza muda huo ulioombwa halafu mijadala mingine iendelee baadaye. Mheshimiwa Zitto endelea."

Zitto akaendelea, "Nasisitiza kwamba baraza la mawaziri limepitiwa na kufanyiwa lobbying (ushawishi). Ila, ninachosema ni wabunge kuwa makini na kutokubali kupitisha azimio hili kwa kuwa tunawapa ulaji watu,"

Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi aliomba tena mwongozo wa spika na kusema, "Nasikitika kusema kuwa hata baada ya wewe mheshimiwa spika kutoa mwongozo katika suala hilo, yeye (Zitto) ameendelea kurudia, maana yake kwamba ana hakika na kile anachokisema. Sasa, naomba atoe ushahidi."

Spika alionekana pia kutojali ombi hilo na badala yake akamtaka Zitto aendelee kutoa hoja yake.

"Napenda kurejea kwamba, maamuzi haya ni ushawishi wa lobbyists, Kama sivyo, serikali ilete hapo mbele pendekezo la kamati lililoitaka liipe miaka mitatu shirika hilo na baadaye lifutwe na kazi zake zichukuliwe na TR. Tusiruhusu baraza la mawaziri kuendeshwa na lobbyists,"alisisitiza Zitto.

Baadaye Lukuvi aliomba tena mwongozo wa spika na kusisitiza Zitto atoe ushahidi akisema, "Cabinet (Baraza la mawaziri), kamati za bunge kazi yake ni kuishauri baraza la mawaziri na ushauri huo siyo lazima usikilizwe."

"Cabinet (Baraza) halifanyi kazi kwa shinikizo la mtu. Sasa, tunamtaka mheshimiwa Zitto aseme ni kina nani waliorubuniwa katika cabinet, na wamerubuniwa na nani? Baraza la mawaziri ni kikao huru ambacho hakina uhusiano wowote na watu wengine."

Lukuvi alipomaliza kuzungumza alisimama, Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki- Chadema) na kuomba mwongozo wa spika akisema, "Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 63 (3 )na (4) inaeleza kuwa mtu wa kwanza mwenye wajibu wa kuthibitisha hilo ni serikali. Lukuvi athibitishe kwa kiwango cha kuliridhisha bunge na baadaye Zitto ajitetee."

Malumbano hayo yalimwamsha Spika Makinda kwenye kiti chake na kueleza, "Nyie watu mnapenda sana kubadilisha mambo. Baraza la mawaziri haliwajibiki kwa bunge. Anayetakiwa kuthibitisha hapo ni Zitto na sasa namtaka alete uthibitisho huo, Juni 29 mwaka huu."

Katika mjadala huo Zitto aliungwa mkono na wabunge kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwamo Dk William Mgimwa wa Kalenga ambaye alilieleza Bunge kuwa azimio hilo la serikali ni kinyume na makubaliano ya Kamati ya Fedha na Uchumi.

"Hoja ya CHC kupewa miaka mitatu na baadaye kazi hizo zipelekwe kwa TR ni kinyume na makubaliano. Kwenye kamati tulisema hili lisifanyike ili TR asije aka-compromise, na huu ni usalama kwa shirika hilo," alisema.

Naye Mbunge wa Mwibara , Alphaxard Lugora (CCM) akichangia hoja hiyo alisema, "Mimi ni mbunge wa CCM na ni mjumbe wa Kamati ya Mashirika ya Umma. Lazima katika jambo hilo wabunge tuwe na uchungu na mali ya Watanzania. Nimepitia mashirika hayo na nimeona yanavyoliwa, TR hana hata certificate (cheti ) za hisa, nchi hii imefika pabaya."

Aliendelea, "Ubinafsishaji ni unyonyaji kwa Watanzania. Spika, ukiona mashirika yanafungwa na kuhamishwa majukumu, ujue kuna wizi unataka kutendeka. Kazi za CHC kuanza kufanywa na Hazina wakati tumeipa kazi ya kufuatilia madeni na mali zetu, huku ni kupotosha institutional memory (kumbukumbu za taasisi) kwa sababu kuna wizi unataka kufanyika."

Kwa mujibu wa Lugora, wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo chochote kinachoanzia bungeni kikiharibika wao ndio wa kwanza kulaumiwa. Alisema ni bora CHC ikapewa kazi hiyo moja kwa moja au kwa kipindi cha miaka mitano ili ikamilishe kazi ya kufuatilia madeni hayo ya masharika ya umma yaliyobinafsishwa.

"Ushauri wangu, serikali ikubali kuwapa muda zaidi, iwe ya kudumu madeni yetu yatapotea bure. Kwa nini TR asichukue kazi za NSSF? Kuna nini CHC? Kama mashirika haya tunayoyaangalia wabunge yana wizi, yale ambayo hatuyachunguzi, kukoje?"

Baada ya malumbano hayo, Spika alimwita Waziri Mkulo kumalizia hoja yake na baadaye wakakubaliana kuwa shirika hilo lipewe muda huo wa miaka mitatu, kuanza Julai Mosi hadi Juni 30, 2014. Lakini, katika kipindi hicho serikali itakuwa inalichunguza shirika hilo na kupeleka ripoti yake bungeni kabla ya kufanya mabadiliko mengine yoyote.

Zitto Kabwe akisisitiza jambo Bungeni mjini Dodoma

No comments: