TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 23, 2011

Mbowe Asita kususia Posho BungeniKIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema licha ya kurejesha kwa hiari gari alilopewa na serikali ataendelea kuchukua posho za ubunge nyinginezo anazopewa kutokana na nafasi hiyo ya uongozi.

Mbowe alisema hayo jana wakati alipotakiwa kujibu hoja zilizotolewa kwa nyakati tofauti na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ofisi ya Bunge zikimtaka aeleze kama ameamua kurejesha gari, basi aache pia kuchukua posho mbalimbali anazozipata kama mbunge na nafasi yake ya uongozi wa kambi ya upinzani.

Katika mahojiano na gazeti hili, Mbowe aling’aka na kusema kuwa hayuko tayari kuacha posho anazopewa kwa vile zipo kisheria na ni muhimu katika kufanikisha majukumu yake."Naweza kusema kuwa huu ni upuuzi!” Aling’aka Mbowe alipoulizwa kama yuko tayari kufuata ushauri wa CCM na ofisi ya bunge.

Lakini, akaongeza: “Kuna mambo mengi ya msingi tunaendeleaa kuyafanya. Unaposema niache na huduma zingine, ofisi ile inaendeshwaje?

"Mambo hayo (kuacha gari) tunayafanya kwa sababu tunaangalia pia ni kwa namna gani hayaathiri shughuli za kiofisi. Ukisema nisichukue Sh2 milioni kwa mfano, unataka ofisi hii iendeshweje?"

Alieleza kuwa ataendelea kupata huduma hizo kwa kuwa ni haki yake, hivyo kuzikubali au kuzikataa ni uamuzi wake na hashurutishwi na mtu.Wiki hii, Mbowe alitangaza kuacha kulitumia gari alilopewa na serikali kwa ajili ya shughuli zake kama kiongozi wa upinzani ikiwa ni mkakati wake wa kutekeleza kwa vitendo ushauri wa chama, Chadema wa kuitaka serikali itekeleze sera ya kuondoa malipo mbalimbali na posho zisizo na tija kwa watumishi wa serikali.

Tangazo hilo la Mbowe lilipokewa kwa kebehi na CCM pamoja na ofisi ya bunge juzi, wakimtaka asisusie gari tu bali pia na posho anazopata ili kuonyesha nia yake ya dhati ya kutekeleza mkakakti wa chama chake.

CCM ilimwita Mbowe kuwa ni mnafiki na mwongo anayetafuta sifa zisizo na msingi kwa ajili ya kuudanganya umma.Chama hicho tawala kilieleza kuwa kitendo cha Mbowe kukataa gari, mafuta na dereva wakati akiendelea kupokea huduma zingine ni unafiki uliovuka mipaka.

Nayo ofisi ya bunge nayo ilisema huduma zote anazopewa kiongozi huo wa upinzani zipo kisheria, hivyo hawezi kuikubali nusu na sehemu nyingine asiikubali.Juzi, Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki alisema kama kweli Mbowe anataka kubana matumizi, akubali na kurudisha posho za Sh 2milioni ambazo hupewa na serikali kila mwezi kwa ajili ya viburudisho pajoma na na Sh45 milioni alizopewa kwa ajili ya kununua gari.

"Mwezi huu amepokea Sh2 milioni kwa ajli ya viburudisho kwenye ofisi yake kama kiongozi wa kambi ya upinzani. Ninamwuliza na hizo nazo atazirudisha? na je, ataendelea kupokea au hatapokea?" alihoji Nchemba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Naye Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel kwenye mahojiano na gazeti hili alisema:"Haya ni mambo ya kisiasa na sisi kama watendaji hatutaki kujiingiza kwenye siasa. Lakini, niseme tu kwamba lile gari hakupewa kufanyia shughuli za kisiasa ni la serikali kwa ajili ya kazi zake kama kiongozi wa upinzani." "Wabunge wote wanaongozwa kwa masharti, Spika anayo yake, Kiongozi wa Upinzani Bungeni kadhalika na hata wabunge wengine nao wanayo masharti yao.

"Sasa, mtu hawezi kukubali masharti fulani na kukataa mengine. Huku ni kuvunja sheria."

Kwa mujibu wa Joel, moja ya masharti aliyopewa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Oktoba 25 mwaka 2010 ni kupokea gari la serikali, dereva na kuwekewa mafuta kwenye gari hilo wakati wa shughuli za bunge.

"Sasa pamoja na kupewa gari, ofisi ya bunge pia inawajibika kisheria kumpa kiongozi huyo nyumba mbili; Dar es Salaam na Dodoma na mlinzi Ili kuhakikisha usalama wake wa kila siku," alisema Joel.

Aliongeza,"Sasa akisema gari sitaki, huu ni utashi wake, lakini kwa nini akatae gari pekee wakati kuna huduma zingine anazopewa?"

Jumanne, baada ya kupitishwa kwa bajeti ya serikali, kambi ya upinzani ilitangaza mgogoro na bunge wa kutochukua posho za vikao kuanzia jana.Lakini, hilo lingefanyika baada ya kuwasilisha rasmi taarifa bungeni jana.

Hata hivyo, wakati kambi hiyo ikitoa msimamo huo wa pamoja, Mbowe alitangaza kurejesha gari alilopewa na serikali, dereva na kutochukua mafuta.Hatua hiyo ilielezwa pia ni sehemu ya uamuzi wa kuonyesha kutoridhishwa na hatua ya serikali kudharau mapendekezo yaliyotolewa na kambi hiyo katika kuiboresha bajeti ya mwaka huu wa fedha.

"Msimamo wetu kama kambi ya upinzani baada ya serikali kuyakataa baadhi ya mapendekezo yetu… Kwa kukataa kuondoa sitting allowances (posho za vikao)," alisema Mbowe na kuongeza:

" Serikali haikukubaliana nasi pia kuuza magari ya anasa (mashangingi), kuondoa misamaha ya kodi kwenye kampuni za madini na kupunguza gharama za kuwasafirisha viongozi wa umma daraja la kwanza."

"Sisi tunaamini kuwa viongozi wanaopaswa kusafirishwa kwa ndege katika daraja la kwanza ni rais na mke wake, makamu wa rais na mkewe, waziri mkuu na mke wake, Spika wa Bunge na mwenza wake.

“Halafu mawaziri wanapaswa kusafiri kwa busines class (daraja la kati) na wabunge wote, economy (daraja la watu wa kawaida)."

Kwa sababu hiyo, Mbowe alisema atawasilisha barua ofisi ya Bunge kuijulisha kuwa wabunge wote wa kambi rasmi ya upinzani hawataachukua posho.

Alisema ataitaka ofisi hiyo iandae fomu mbili bungeni; ya mahudhurio ya wabunge na fomu za malipo ya posho ili wao wasaini hiyo ya mahudhurio.Alisema pia kuwa kuanzia siku hiyo ahlitaki tena gari alilopewa na serikali kwa kuwa mkakati wa upinzani ni magari yote ya kifahari, likiwepo alilopewa, kuuzwa na fedha zitumike kwa ajili ya kupambana na kero za wananchi.

Hata hivyo, pamoja na ahadi hiyo, Joel alithibitisha kwamba Ofisi ya Bungte haijapokea barua yoyote kutoka kwa kambi hiyo ya upinzani katika kutekeleza ahadi yao.Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu alidai kuwa tayari Mbowe amerejesha gari tangu Jumatatu lakini akakiri kuwa bado hawajaandika barua kama walivyoahidi.

"Ni kweli barua hatujapeleka ila itapelekwa kesho, lakini tayari Mbowe amerudisha gari hilo tangu juzi (Jumatatu) na ameanza kutumia usafiri binafsi," alisema Lissu.

No comments: