TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, June 26, 2011

Wanafunzi Udom wadaiwa kutengeneza mabomu

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idrisa Kikula amesema hawezi kushawishika kwa lolote katika kuwarudisha chuoni hapo wanafunzi kwa kuwa anazo taarifa kuwa baadhi walitengeneza mabomu ya kupambana na polisi.

Profesa Kikula alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakuu wa wilaya wa wilaya zote nchini ambao walitembelea chuo hicho kwa ajili ya kujifunza.

Alisema kuwa hakuna kitu kitakachomshawishi kuwarudisha wanafunzi kwa kuwa anasimamia taaluma sio siasa kama ambavyo baadhi ya wabunge wanataka iwe.

“Siwarudishi wanafunzi kwa shinikizo la kisiasa maana siku ya mgomo mimi niliweka rehani maisha yangu baada ya kuambiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa wanafunzi wasigome nikawafuata saa sita usiku nikawaambia Serikali inashughulikia madai yenu, lakini baadaye saa tisa usiku nikasikia wameandamana,’’ alisema Profesa Kikula na kuongeza:

“Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini kuwa baadhi yao siku moja kabla walikwenda mjini kununua petroli ambayo walitaka kutengeneza mabomu ya kupambana na polisi.

“Sasa, kwa hali hiyo mnadhani ingekuwaje lazima tufanye uchunguzi wa kina kabla ya kuwaruidisha.’’

Kauli ya makamu mkuu huyo iliungwa mkono na wakuu hao wa wilaya ambao walitaka uongozi wa Udom usiwarudishe kirahisi wanafunzi hao ili wajifunze kwanza kuwa walichofanya hakikuwa kizuri.

“Tena mkianza kuwarudisha rudisheni wana-CCM, hao wa Chadema achana nao maana ndio wanaoanzisha vurugu na uvunjifu wa amani hawana shukrani hao hata siku moja na wala hawajui kutoa fadhila zaidi ya kulalamika kila kitu,’’ alisikika akisema mmoja wa wakuu hao wa wilaya.

Mwanzoni mwa mwezi, uongozi wa chuo hicho uliwafukuza wanafunzi zaidi ya 9,000 wa Chuo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano baada ya kufanya maandamano yaliyomtaka baadhi ya mawaziri wajiuzulu.

Waliwataja kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani , Shamsi Vuai Nahodha wajiuzulu kwa madai ya kuwadanganya.

Wanachuo hao walikuwa wakishinikiza kupelekwa katika mazoezi ya vitendo pamoja na kununuliwa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na kompyuta.

Wabunge wa Bunge la Muungano ambao wanaendelea na mkutano wao mjini Dodoma wamekuwa wakipiga kelele mara kwa mara wakitaka wanafunzi hao warudishwe chuoni hapo kwa madai kuwa walichokuwa wakidai ilikuwa ni haki yao.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema Serikali ilikosea kutowapeleka katika mazoezi ya vitendo wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuwa hiyo ni haki yao ya msingi.

Mukama aliwaomba radhi wanafunzi hao kwa upungufu huo na kutaka waipe Serikali mwaka mmoja ili ibadili mfumo unatumika kwa sasa.

No comments: