TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 16, 2011

Wanafunzi 9,000 Udom watimuliwa


Wanafunzi wa Chuo cha Sanaa ya Lugha na Sayansi ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Dodoma wakiwa katika pilika za kuhamisha mizigo baada ya uongozi wa chuo hicho kuwatimua jana. Wanafunzi hao walifukuzwa baada ya kuendelea na mgomo


ZAIDI ya wanafunzi 9,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamefukuzwa kwa muda usiojulikana kuanzia jana kwa madai ya kuhamasisha mgomo usio halali.Habari zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kuwa wanafunzi hao ni wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Sayansi Asilia. Walitakiwa kuondoka chuoni hapo kabla ya saa 8:00 mchana.

Baada ya amri hiyo, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walionekana wakiwa wanarandaranda katika maeneo ya chuo hicho.hali hiyo ilichangia pia kuharakisha wanafunzi hao kuondoka chuoni hapo wakihofia kukumbana na kipigo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idriss Kikula alithibitisha kufukuzwa kwa wanachuo hao na kusema kuwa suala la kuwarejesha litatokana na utaratibu watakaoupanga baadaye.

Kufukuzwa huko kumekuja siku mbili baada ya kuanzisha maandamano yaliyoshinikiza kujiuzulu kwa viongozi waandamizi wa Serikali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwa madai kwamba wamewadanganya kuhusu malipo yao ya masomo kwa vitendo.

“Ni kweli kabisa kuwa tumewasimamisha kwa muda usiojulikana. Tutawarudisha kwa muda ambao tutaona unafaa,” alisema Profesa Kikula na kuongeza mtindo utakaotumika ni wa kuchambua na kurudisha mwanafunzi mmoja mmoja.

Katika madai yao, wanafunzi hao walisema wanasoma bila ya kufanya mazoezi ya vitendo kama ilivyo kwa vyuo vingine.Madai mengine ni pamoja na mazingira mabovu chuoni hapo pamoja na kutosoma baadhi ya masomo ambayo wanachuo wengine wanasoma.

Msimamo wa wanafunzi
Wakizungumza mara baada ya agizo hilo jana baadhi ya wanafunzi hao walisema kuwa hawaoni tabu kufukuzwa wakisema wao ni waathirika wanaotumika kwa maslahi ya wengine.

Walisema kuwa kufukuzwa kwao ni kwa ajili ya kudai maslahi ambayo wamekuwa wakiyatafuta wakati wote bila ya mafanikio na kwamba kama itabidi itakuwa bora waondoke.

“Sisi tunaondoka na wenzetu wengine walishaondoka katika Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta kwa hiyo kwa hali hii lazima chuo chote kitafungwa maana hali inakokwenda chuoni hapa ni siasa tupu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao na kuongeza:

“Ni bora turudi nyumbani kwa kuwa huwezi kusoma bila ya kufanya mafunzo kwa vitendo. Ni bora tukae nyumbani tu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao huku akiungwa mkono na wenzake.

Wanafunzi wa Kitivo cha Teknolojia ya Habari na Elimu Angavu walifukuzwa baada ya kugoma wakitaka walipwe fedha kwa ajili ya vifaa vya kujivunzia kwa vitendo.

Kufukuzwa kwa wanafunzi hao kulikuwa faraja kwa madereva wa teksi na pikipiki maarufu kama bodaboda ambao walifurika chuoni hapo kufanya kazi ya kuwasafirisha kwa malipo ya Sh10,000 kwa pikipiki na teksi Sh15,000

No comments: