TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 16, 2011

SAKATA LA POSHO: Siri yafichuka • Makamba asema kukata posho ni ajenda ya kitaifa

WAKATI Spika wa Bunge, Anne Makinda, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakipinga kukatwa posho zao, wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho wamepitisha azimio la kuzifyeka posho zao.
Hatua hiyo huenda ikamuumbua Spika Makinda, Waziri Mkulo na wabunge wa CCM ambao kwa takriban wiki moja sasa wamekuwa kwenye mzozo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe aliyeibua hoja ya kutaka posho za wabunge, watumishi na watendaji wa serikali, zifutwe.

Duru za siasa kutoka ndani ya CCM, zilisema wajumbe wa sekretarieti hiyo inayoundwa na sura mpya za vijana, walipitisha azimio hilo kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa chama.

Wajumbe wa sekretarieti hiyo inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama, ni pamoja na Kapteni John Chiligati, January Makamba, Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba.

Inaelezwa kuwa katika moja ya vikao vya awali vilichofanyika jijini Dar es Salaam, wajumbe hao baada ya kumaliza kikao chao, waliletewa bahasha za posho na kutakiwa kusaini.

“Hapo ndipo hoja ya kufuta posho ilipoanza. Mmoja wa wajumbe alihoji sababu ya wao kuchukua posho kila wanapokutana hasa wawapo Dar es Salaam yalipo makazi ya wengi wao.

“…Katika hali ya kawaida wengi tunatoka Dar es Salaam, tuna magari ya chama ambayo yanajazwa mafuta, sioni sababu tena ya sisi kupata posho tukiwa hapa,” alikaririwa mmoja wa wajumbe wa sekretarieti katika kikao chao cha ndani.

Tangu wakati huo, habari zinasema kuwa wajumbe wa sekretarieti ya CCM hawachukui posho kwa vikao vinavyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alipoulizwa juu ya azimio la sekretarieti ya CCM kukataa posho, Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alikataa kutoa ufafanua kwa madai kuwa sio kila kitu cha chama kinapaswa kutolea taarifa.

Hata hivyo alirejea wito wake kuwa suala la posho linajadilika kwani sio kila jambo linalotoka upinzani ni mbaya. “Suala la chama kukataa posho sijui…lakini hoja hiyo inajadilika,” alisema Nape.

Kwa mujibu wa habari hizo, posho ya wajumbe hao ni sh 60,000 kwa siku na hukutana mara kwa mara kutokana na shughuli za uendeshaji wa chama.

Akichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM), alisema suala la kufuta posho ni ajenda ya kitaifa kwani imo ndani ya mpango wa maendeleo.

Hata hivyo hoja ya kutaka kupunguza posho za wabunge, iliasisiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, kwenye mikutano ya kampeni za urais.

Hivi sasa, mzozo wa posho za wabunge umefika pabaya baada ya Spika Makinda kusema Zitto na wabunge wengine watakaoshindwa kusaini daftari la mahudhurio wanakabiliwa na hatari ya kufukuzwa bungeni.

Tishio hilo limekuja baada ya Zitto hivi karibuni kutoa taarifa kwamba kuanzia sasa hatasaini daftari la mahudhurio kama njia ya kukwepa kulipwa posho (Seating Allowance).

Spika Makinda alisema Zitto asiposaini mahudhurio ya mikutano mitatu mfululizo, atafukuzwa bungeni.

Alisema Bunge lilishatoa utaratibu kwamba kama Zitto hataki posho zake, anaweza kuichukua mwenyewe na kuipeleka anakotaka.

Sakata la posho za wabunge lililoanzishwa na Zitto na baadaye kuungwa mkono na wabunge wote wa CHADEMA limeonekana kuwagawa wabunge wa CCM.

No comments: