TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, June 19, 2011

U-23 kiboko ya vigogo yaivaa Nigeria

Kocha Jamhuri Kihwelu

TIMU ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 23, leo itacheza mechi ya marudiano dhidi ya vijana wa Nigeria 'Dream Team' kwenye uwanja wa Samuel Ogbemudia mjini Benin kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya Olimpiki London 2012.

Vijana wa Tanzania waliwasili juzi mjini Lagos na kupanda ndege nyingine kuelekea kwenye mji wa Benin uliopo kusini mwa Nigeria katika Jimbo la Edo.

Kikosi cha Vijana cha Tanzania kilipofika mjini Benin kilifikia kwenye hoteli ya ISNO na kilifanya mazoezi jana jioni kwenye uwanja wa Samuel Ogbemudia kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ambayo wachezaji wa Nigeria wamepania kutaka kulipiza kisasi na kuibuka na ushindi.

Akilizungumzia pambano hilo kocha wa Vijana U-23 wa Tanzania, Jamhuri Kihwelu alisema,"Nafahamu tulishinda katika mechi ya kwanza iliyofanyika mjini Dr es Salaam, lakini hii ni mechi ya marudiano na natarajia itakuwa ngumu."

Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo za vijana wa Tanzania na Nigeria kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, vijana wa Tanzania walishinda bao 1-0, bao lililofungwa na Thomas Ulimwengu katika dakika ya 82.

Wakilizungumzia pambano hilo baadhi ya wachezaji wa timu ya vijana ya Nigeria hawakuficha hisia zao za hasira za pambano hilo ambapo kiungo wa timu hiyo aliyekuwa akichezea Inter Milan ya Italia, lakini hivi sasa amejiunga na klabu ya Parma ya Italia pia, Obiora Nwankwo alisema,"tunafahamu jukumu tulilonalo, wote tunafahamu tunatakiwa kushinda mechi hii na tumekuwa tukijiandaa vizuri tangu tuliporudi kutoka Tanzania katika mechi ya kwanza, tutajitahidi kuhimizana kucheza kitimu, tunayo mazingira yote ya kushinda na tupo tayari kwa pambano."

Mchezaji mwingine wa vijana wa Nigeria anayechezea Atletico Baleares ya Hispania, Edet Ibok alisema,"kwa morali tulionao kambini sidhani kama vijana wa Tanzania watatuweza, tunafahamu timu ya Tanzania ni imara, lakini tulipata nafasi nyingi za kuwafunga katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwao, lakini hatukuwa na bahati, tumefanyia mazoezi makosa yote yaliyojitokeza, ninaamini tutafanya vizuri."

Hata hivyo; kikosi cha vijana wa Nigeria kinasumbuliwa na wachezaji majeruhi wengi, ambapo mshambuliaji wao Ahmed Musa, kiungo wao Rabiu Ibrahim na winga wao anayechezea AC Milan ya Italia, Nnamdi Oduamadi wote ni majeruhi.

Lakini Nigeria inatamba kwa kuwa na hazina kubwa ya wachezaji wengi vijana hivyo imewaita mshambuliaji Ekigho Ehiosun anayechezea klabu ya Warri Wolves , mchezaji anayecheza Scotland, Sone Aluko, Gani Oseni anayecheza Vietnam na mshambuliaji Chrisantus Macauley aliyekuwa mfungaji bora katika mashindano ya vijana chini ya miaka 17 ya dunia yaliyofanyika 2007 huko Korea ya Kusini.

Naye kocha wa vijana wa Nigeria, Austin Eguavoen alisema,"Tunafahamu umuhimu wa mechi hii ya marudiano na Tanzania, hatutataka kupoteza nafasi, Wanaigeria wanaiamini sana timu hii hivyo hatutaweza kuwaangusha."

Vijana wa Tanzania walifika katika hatua hiyo baada ya kuichapa Cameroon 4-2, baada ya Tanzania kushinda katika mechi ya marudiano mabao 2-1, lakini katika mchezo wa kwanza uliofanyikia Yaounde, Cameroon ilishinda 2-1.

Mechi nyingine za kuwania kufuzu michezo ya Olimpiki ni Afrika Kusini itakuwa ikipambana na Benin, Algeria dhidi ya Zambia,Mali itakuwa ikiumana na Gabon, Senegal itapambana na Tunisia na Misri itacheza na Sudan, wakati DR Congo itaumana na Morocco.

Washindi wataingia kwenye hatua ya mwisho ya kufuzu kucheza michezo ya Olimpiki 2012.Kikosi cha vijana leo kinaweza kuwa hivi, Juma Abdul, Abuu Ubwa, Juma Abdul, Obadia Mungusa, Shomari Kapombe, Jabir Aziz, Jamali Mnyate, Sudi Mohamedy, Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na Mcha Hamis Mcha.

No comments: