TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, June 28, 2011

TLP WATWANGANA MBELE YA WAANDISHI WA HABARI


VIOJA na vurugu jana vilitawala katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), na kusababisha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kuingilia kati na kuwakamata baadhi ya wanachama wa TLP.

Vurugu hizo zilitokea jana kwenye mkutano na waandishi wa habari uliokuwa umeitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Hamad Tao.Taharuki ilianza pale Tao ambaye alikuwa na lengo la kumbomoa Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema kujikuta anatoa maelezo ambayo hayafanani na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa kwa waandishi wakati mkutano huo upokuwa ukiendelea.

Vurugu lilianzia pale mmoja wa waandishi alipohoji Tao kutoa maelezo yanayopingana na taarifa yake ya maandishi ambayo yeye mwenyewe ameisaini na kila mwandishi kugawiwa nakala.Tao alipoponyeshwa taarifa hiyo alitaharuki na kuanza kujaribu kuikanusha, lakini wanachama wengine wa TLP aliokuwa ameandamana nao walianza kupingana naye hali ambayo ilisababisha mkutano kuvurugika na kuondoa maelewano.

Tatizo hilo lilitokana na Tao kuandamana na wanachama wengine ambao wakati anaanza kutoa maelezo, waligawa karatasi hizo, lakini cha kushangaza ni pale maelezo yalipotofautiana huku taarifa hiyo ikiwa na saini ambayo Tao alishindwa kuikataa kuwa ni yake.

Hali ilikuwaje?
Hali yenyewe ilikuwa hivi, Tao aliwasili katika mkutano huo saa 5.00 na moja kwa moja alianza mazungumzo yake na waandishi wa habari kuhusu hali ya kisiasa ndani ya chama hicho.Pamoja na mambo mengine alimtaka kuwa Mrema si mwanachama wa TLP bali ni wa CCM na wala chama hicho hakijawahi kumpa nyumba kama yeye anavyodai.


Wakati akiendelea kutoa maelezo ya kumbomoa Mrema, kama dakika 20 baadaye kundi la wanachama wengine wa chama hicho ambao awali walikaa katika viti kama waandishi wa habari wakimsikiliza lilianza kugawa taarifa ya maandishi.

Watu hao walianza kuwagawia waandishi taarifa iliyosainiwa na Tao na wala yeye mwenyewe hakushtuka wala kupinga watu hao kugawa taarifa hiyo ya maandishi.Waandishi walipigwa na butwaa kuona taarifa hiyo inamsifu Mrema wakati Tao anamponda, ikabidi waanze kuangaliana na mmoja wao akaamua kupasua jipu na kumuuliza:“Naibu Katibu, unakanusha juu ya taarifa za Mrema kupewa nyumba na wanachama na unaeleza kuwa Mrema ni kada wa CCM. Mbona katika taarifa uliyotupa inakanusha yote na kuelezea kuwa Mrema alipewa nyumba na wanachama wote waliridhia?” alihoji mmoja wa wanahabari.

Swali hilo lilimfanya Naibu Katibu huyo ashikwe na butwaa na kushangaa juu ya maelezo hayo ya mwandishi wa habari ambao walimtaka kufafanua juu ya utata huo.Tao alijitetea, “Mimi sijui taarifa hizo na wala sikanushi maneno yangu kwani hata taarifa zangu za maandishi zinajieleza. Hawa wanaogawa taarifa hizi wametumwa na Mrema ili nisiseme ukweli wa mambo mabaya anayoyafanya ndani ya chama kwani amegeuza chama kuwa chake na si cha wananchi.”

Alipotakiwa kujieleza zaidi juu ya saini iliyopo kwenye taarifa hiyo alikanusha na kusema yeye hajui chochote na kuwa huo ni mchezo mchafu ulifanywa na Mrema ili kujisafisha.“Sahihi hiyo mimi siijui na maelezo yaliyomo humo ndani ya taarifa hiyo siyatambui,” alisema Tao.

Taarifa hiyo ambayo ilikuwa na sahihi ya Tao ilikuwa ikizungumzia nyumba anayoishi Mrema ambayo inadaiwa alinunuliwa na chama hicho na kwamba ni mali halali ya Mrema.Hali hiyo ilisababisha malumbano makubwa na mkutano huo kuvunjika huku waandishi wakabakia njia panda juu ya kipi ni ukweli hasa ikizingatia kuwa waliogawa taarifa hiyo waliandamana wote na kuingia kwenye chumba cha mkutano.

Baada ya kuona ubishi inazidi na maelewano hakuna huku munkari unazidi kupanda kila mmoja akitetea upande wake, maofisa wa Idara ya Habari (Maelezo), waliamua kumchukua Tao na wenzake na kwenda kuwaweka katika chumba kimoja.

Ujio wa FFU
Muda mfupi baadaye FFU, walifika na kuwachukua wafuasi wanne wa TLP waliokuwa wanapingana, akiwemo Tao.Walichukuliwa na kupakizwa katika gari ya polisi na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Waliochukuliwa askari hao ni pamoja na Naibu Katibu, Richard Lyimo, Katibu wa Wanawake Taifa, Nacy Mlikalia na mlinzi Anderson Temu.Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Maelezo, Raphael Hokororo alisema wamelazimika kuwaita FFU kutokana na mzozano makali ambayo waliona mwisho wake ungeweza kuwa ni mapambano, kujeruhi na uharibifu wa mali.

“Tumelazimika kuita watu wa usalama kutokana na vurugu hizi kwani watu hawa wameingia hapa na kumwambia mlinzi kuwa ni wa moja katika mkutano, lakini kumbe ni kinyume chake. Matokeo yake wamesababisha mtafaruku huu,” alisema Hokororo.

Alisema wamelazimika kufanya hivyo ili kuweza kulinda mali za waandishi na watu wote wanaokuja katika mkutano kwani ofisi hizo ni za Serikali na kwamba zinapaswa kuheshimiwa.

No comments: