TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, June 17, 2011

RPC Kilimanjaro afariki dunia ghafla

MJI wa Moshi na Vitongoji vyake, jana ulizizima kufuatia taarifa za kifo cha ghafla cha Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, aliyetarajiwa kustaafu rasmi Julai 1 mwaka huu baada ya kulitumikia Jeshi kwa miaka 37.

Taarifa za kifo chake zilienea na ilipofika saa 4:00 asubuhi tayari mji wa Moshi ulikuwa umegubikwa kwa simanzi na majonzi huku watu wakijikusanya katika vikundi mbalimbali wakitafakari kifo hicho.Baadhi ya wananchi walionekana wakitumiana ujumbe mfupi wa maandishi (sms), kuulizana kama kila mmoja amepata habari za kifo hicho huku wengi wakiwa hawaamini hasa wale waliokuwa naye jana yake wakitaka uthibitisho wa jambo hilo.

Habari zilisema Kamanda Ng’hoboko aliyekuwa kipenzi cha wanahabari mkoani Kilimanjaro, alifariki saa 2:00 asubuhi dakika chache baada ya kuchukuliwa kipimo cha malaria katika zahanati ya Jeshi iliyopo ndani ya kambi ya polisi.

“Aliposhuka kwenye gari aliwasalimia polisi wa vyeo vya chini aliowakuta hapo na kucheka nao kwa sekunde chache na kuwaambia anajisikia vibaya hivyo anataka kupima malaria na shinikizo la damu,”kilisema chanzo chetu cha habari.

Chanzo hicho kiliimbia Mwananchi kuwa baada ya kufika katika zahanati hiyo alichukuliwa vipimo vya damu ambapo wauguzi walimpa kiti apumzike wakati akisubiri majibu hayo, ili baadae apimwe pia shinikizo la damu.

Hata hivyo, wauguzi walishtuka kusikia kishindo cha kuanguka kwa kitu na walipoangalia ndipo wakamkuta Kamanda Ng’hoboko akiwa chini na harakaharaka wakashirikiana na dereva wake walimkimbiza KCMC.“Baada ya kufika KCMC madaktari walimpima na kugundua alikuwa amekwishafariki hata kabla ya kufikishwa pale hospitalini,”kilidokeza chanzo hicho cha habari.

Habari zaidi zilidai usiku wa kuamkia jana, Kamanda Ng’hoboko ambaye alikuwa katika likizo ya kustaafu, alianza kusikia hali asiyoielewa ikiwamo kuchoka na ilipofika asubuhi alimpigia simu dereva wake ili aende kumchukua.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, wakati akiondoka nyumbani hadi kufika katika zahanati hiyo, Kamanda Ng’hoboko aliyekuwa na cheo cha Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), hakuwa na mwonekano wa kuumwa.Chanzo cha kifo hicho bado hakijathibitishwa na madaktari, lakini taarifa za awali zilisema kifo chake kilitokana na kupatwa na kiharusi.

Mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kuwa ni Liston Ng’hoboko aliwathibitishia waandishi wa habari kuhusu kifo cha ghafla cha kaka yake na kufafanua kuwa hiyo jana ndugu walikuwa wakikutana kupanga taratibu za mazishi.

“Kwa hiyo kama mlivyosikia alianguka ghafla pale zahanati na alipofikishwa KCMC alikuwa tayari amefariki…leo (jana) ndugu tunakutana kupanga namna tutakavyosafirisha mwili wake kwenda kijijini Ngosila Kishapu Shinyanga,”alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Kalembo alisema kifo cha Kamanda Ng’hoboko kimeshtua wengi na bado wapo wanaojiuliza kama ni kweli kafariki, lakini akasema inabidi waamini hivyo.

“Ni kweli Kamanda Ng’hoboko hatunaye tena, ni vigumu kuamini, lakini inabidi tuamini hivyo kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu,”alisema Kalembo na kusema marehemu ameacha mjane na watoto sita.

Kikwete atuma salamu za rambirambi
Rais Jakaya Kikwete alitoa salamu za rambirambi kwa IGP, Said Mwema kufuatia kifo cha Ng’oboko.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu jana ilisema Kikwete amesikitishwa na kifo cha Kamanda huyo ambaye ni mmoja wa maafisa hodari na wachapakazi.

Taarifa hiyo ilisema marehemu alizaliwa mwaka 1951 katika kijiji cha Kofia (Ghofia) wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kwamba wakati mauti yanamkuta kamanda huyo alikuwa ameanza likizo ya kustaafu kazi tangu Juni 3, mwaka huu ambapo angestaafu kazi Julai mosi, 2011.


Ng’hoboko alihamishiwa mkoani Kilimanjaro mwaka 2006 akitokea Mwanza alikokuwa na wadhifa wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) ambapo wadhifa wa Ukamanda wa mkoa aliurithi kutoka kwa mtangulizi wake, Venance Tossi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,Yusuph Ilembo amethibitisha kufariki kwa bosi wake huyo na kufafanua kuwa alifariki njiani wakati akikimbizwa hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Mkewe alazwa ICU
Wakati huo huo, taarifa zilizotufikia baadaye jana jioni zilisema kuwa mke wa marehemu aliyetajwa kuwa ni Anna Robert jana alasiri alipata mshituko wa moyo na kukimbizwa KCMC.

Habari hizo zilizothibitishwa na ndugu na marafiki wa Kamanda Ng’hoboko, zilisema Anna alikibizwa KCMC saa 9;50 na kulazwa kwa muda katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

No comments: