TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, June 18, 2011

Mbunge atishia kuwastaki mawaziri kwa JK

MBUNGE wa Gairo Ahmed Shabiby (CCM), amesema kuwa anapanga kwenda Ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili akawachongee Mawaziri na wasaidizi wa karibu wa rais huyo, kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakimpotosha katika mambo mengi.

Shabiby ambaye ni mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alitoa kauli hiyo juzi jioni bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, kuhusu makadirio ya bajeti ya serikali kwa 2011/2012.

Alisema Rais amekuwa akidanganywa na kushindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi kutokana na watu walioko chini yake kutomwambia ukweli.

“Pale kwangu Rais aliahidi kujenga barabara ya Chakwale-Lubeho pamoja na barabara ya Nongwe, aliahidi muda mrefu lakini ameshindwa kutimiza kutokana na kutoshauriwa vizuri au kukumbushwa na watu waliko chini yake," alisema mbunge huyo na kuongeza:

"Lazima siku moja nitakwenda Ikulu kuonana na Rais ili tuweze kuzungumza juu ya uzembe wa watu wake na namna wanavyoshindwa kutimiza hata kitu kidogo alichokiahidi,"alisisitiza Shabiby."

Mbunge huyo kijana alienda mbali zaidi na kueleza kuwa kutokana na rais kutoambiwa ukweli, kauli mbiu Kilimo kwanza ni siasa butu ambazo haziwezi kuwasadia Watanzania.

Mbunge huyo alisema kuwa kauli ya Kilimo kwanza katika nchi ya Tanzania haiwezi kufanikiwa kwani ipo kisiasa zaidi kuliko uhalisia.

Alisema kuwa kauli ya Kilimo kwanza pamoja na kauli nyingine ikiwemo Kilimo ni uti wa mgomo, Siasa ni Kilimo, zimekuwa zikiwalenga watu ambao tayari wana uwezo na kuwaacha wale ambao ni maskini siku zote.

“Nasema hivyo kwa sababu ni uhakika kuwa hata na ninyi mnajua kuwa hakuna wakulima wenye hati za nyumba ili waweze kupatia mkopo kitu ambacho kinatakiwa na mabenki sasa hapo tunalenga nani kama si watu wenye uwezo,” alihoji Shabiby.

Alitolea mfano kuwa katika jimbo lake mbunge huyo alisema ni nyumba tisa tu ambazo zina hati miliki hivyo kama ni kukopesha matrekta nyumba hizo ndizo zitaweza kukopeshwa na si vinginevyo.

Alisema hali hiyo inatokana na vitendo vya urasimu uliomo ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao wanashindwa kuvifikia vijiji vingi kwa ajili ya kupima ardhi.

Akizungumzia suala la uingizaji wa mafuta mbunge huyo aliitaka serikali kuwa na uamuzi mgumu katika mipango yake ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato huo ili nchi iweze kujikomboa.

“Nikiri kuwa na mimi ni mdau katika suala la mafuta kwa kuwa nafanya bishara ya mafuta, lakini nataka niseme kuwa tuwe na umaamuzi ma zito katika kuhitaji mabadiliko ya kibiashara kwa manufaa ya wananchi na hivyo mafuta tuagize sisi,’’ alisema Shabiby.

Mbunge huyo alisema kuwa hakuna kitakachoharibika iwapo serikali itaamua kuwafuta waagizaji wa mafuta na kutoa nafasi kwa watu wengine na kwamba wakifanya hivyo watakuwa wameikomboa nchi kiuchumi.

“Tusibembelezane katika suala la mafuta hivyo kama hayo makampuni yameshindwa basi tupo hata sisi tutaweza kuagiza mafuta hayo kwa wingi bila ya shida yoyote na kila kitu kitakwenda vizuri kuliko ilivyo sasa,’’aliongeza

No comments: