TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 16, 2011

Kwa jicho laTGNP Kilimo Kwanza imemfanya mkulima mdogo kibarua

HUKU Bunge la Tanzania likiwa katika kikao cha bajeti kilichoanza wiki moja iliyopita huku sekta ya kilimo ikiwa mojawapo ya sekta ambazo zimetengewa kiasi kikubwa cha fedha, uwekezaji katika sekta hiyo kibiashara una dosari.

Baadhi ya wanaharakati wanaamini kuwa kumekuwapo na ongezeko kubwa la watu wanaonunua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya kilimo cha mazao ya nishati mbadala, huku wachache wakichukua aridhi hizo kwa ajili ya kilimo cha chakula.

Katika hali ya kawaida na hasa kutokana na ukweli kuwa mfumo dume bado unatawala katika jamii, wanaoathirika baada ya aridhi ya familia kuuzwa na wanawake na watoto kwani, walio wengi hawashirikishwi hata katika uuzwaji huo wa aridhi. Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Usu Mallya ana mtazamo gani?

Swali: Mkiwa kama mtandao wa jinsia mmeshafanya uchambuzi wa sera ya kilimo kwanza kuona kana inamchango gani wa kuwainua waneke na jamii kwa ujuma?
Jibu: Tumeipitia kwa umakini sera ya Kilimo Kwanza, tumeangalia maana na umuhimu wake kwa jamii iliyoko pembezoni, wanawake, wanaume wa Tanzania na ajira, maisha endelevu na biashara

Tumezindua muhtasari wa sera ambao unalenga kutoa uchambuzi yakinifu wa sera za serikali na mgawanyiko wa bajeti katika sekta hizi muhimu.Sekta ya ajira na maisha endelevu na kilimo, yanauhusiani wa karibu na maendeleo ya wanawake walioko pembezoni na pia kwa wanaume.Kila muhtasari wa uchambuzi wa sera tulioufanyia kazi, uliuliza maswali kadhaa kuwa ni kwa kiasi gani sera hizi zinaweka vipaumbele katika mahitaji muhimu ya wanawake hasa wa kipato cha chini wa vijijini na mijini, sio tu kinadharia bali kwa mikakati imara ya mgawanyo sawa wa rasilimali.

Swali: Katika uchambuzi wenu ni nini mlichokibaini?
Jibu: Kwanza, inatakiwa ujue kuwa, idadi kubwa ya wanawake wa Kitanzania wanategemea kilimo cha jembe la mkono kwa maisha endelevu, kama chanzo cha kujipatia kipato, pia kama chanzo cha chakula cha kila siku kwa familia na jamii.

Pia, idadi kubwa ya wanawake na wanaume bado imeendelea kutegemea sekta ya kipato isiyo rasmi kama chanzo cha kujipatia kipato kwa ajili ya mahitaji ya kila siku kwa wote wanaoishi vijijini na mijini.

TGNP katika uchambuzi huu wa sera hizi mbili, tumeona kuwa sera na bajeti zinaweka kipaumbele, madai na mahitaji ya makampuni makubwa ya nje na ndani kama msingi wa kuendesha na kukuza biashara ya nje.
Kutokana na kipaumbele hiki, umuhimu wa kusimamia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kujitegemea pamoja na mkakati wa maendeleo ya wananchi wenyewe, umesahaulika.

Lengo kuu la sera ya kilimo kwanza ni kuweka nguvu kwa wazalishaji wakubwa kwa kuwapa vipaumbele kutoka serikalini hasa katika maeneo ya mikopo, misamaha ya kodi, ruzuku na nyinginezo.

Swali: Huko kuweka nguvu kwa wazalishaji wakubwa, matokeo yake mnadhani ni nini?
Jibu: Wamekuwa wakitumia njia hiyo kudai soko huria katika ardhi, umiliki wa ardhi, kwa kigezo kuwa watawafikia wananchi wa hali ya kawaida walioko vijijini.

Changamoto kubwa katika sera hii ya sasa ya kilimo, ni jinsi inavyoonekana kukubali na kuukabiribisha mfumo mpya wa matumizi ya mbegu zilizorekebishwa “Genetically Modified Seed” (GM), maarufu kama “mbegu za miujiza” (Miracle Seeds), unaolenga kuzalisha mbegu za mazao katika maabara, kilimo cha mazao ya nishati (Biofuel), matumizi makubwa ya mbolea za viwandani na madawa ya kilimo.

Uchambuzi uliofanywa kuhusu mfumo huu hapa Afrika na Asia, umeweka wazi athari na changamoto za teknolojia hii ya uzalishaji mbegu inayomlazimisha mkulima mdogo kuwa na majukumu makubwa kinyume na uwezo wake.

Mfumo unaelekeza nguvu zake katika kilimo kikubwa wakati walengwa ni maskini, hatua hii inasababisha mashirika makubwa yanayojihusisha na kilimo na biashara kunufaika kupitia ukodishaji wa mashamba, uuzaji wa pembejeo, dawa na mbolea na kuwaacha wakulima masikini mikono mitupu.

Wakati mwingine hawa ndio wamekuwa wananunuzi wakubwa wa mazao yanayozalishwa kwa kulangua, mabenki makubwa pia yameonyesha kunufaika zaidi kuliko mwananchi maskini kutokana na kudai riba kubwa katika mikopo ya kilimo hasa hiki cha uzalishaji wa mbegu.

Swali: Mfumo wa uzalishaji wa mbegu hizo unafaida ama hasara?
Jibu: Mfumo huu wa mbegu za GM umekuwa kikwazo kwa wakulima wadogo kwa sababu hawawezi kuhifadhi mazao yao ili kuandaa mbegu kwa ajili ya msimu unaofuata.

Unawalazimisha wakulima hao kuendelea na mtindo wa kununua mbegu madukani kila mwaka badala ya kuzalisha za kwao kwa njia za asili.Athari nyingine ni matumizi ya zana kubwa katika kilimo kinachotumia mitambo na mafuta, hivyo kusababisha makampuni makubwa ya mafuta kujiingiza humo, kama wanufaika wakubwa na hivyo kujenga nguvu kubwa ya ushawishi ya kuendeleza aina hii ya kilimo.

Ili kutimiza hili, sehemu ya ardhi ya kilimo cha chakula lazima itumike, na hivyo mkulima kulazimika kugawa muda wake kati ya kilimo cha mazao ya biashara ambayo serikali inayataka, na kilimo cha chakula kwa ajili ya familia yake.
Kwa upande mwingine kukimbilia teknolojia hii, serikali inajivua wajibu wa kumwendeleza mkulima mdogo na kufungua milango kwa masetla; hivyo kumfanya abaki kibarua kwenye ardhi yake aliyoirithi.

Mfumo wa GM umekuwa ukishinikizwa Tanzania na nchi jirani na Jumuiko la Mapinduzi ya Kijani Kibichi Afrika, (AGRA), Ukuzaji wa Kilimo katika mwambao wa Kusini na mashirika makubwa ya kilimo cha biashara.

No comments: