TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, June 17, 2011

Bajeti ya upinzani yalitikisa Bunge • Mashangingi yote kuuzwa

KAMBI ya Upinzani Bungeni, imesoma bajeti mbadala ambayo imefuta ada za shule, misamaha mikubwa ya kodi, mfumo wa kulipana posho za vikao (sitting allowances) kwa watumishi wa umma na kulipa pensheni kwa wazee wote nchini.

Eneo jingine iliyoligusa ni kutaka kuyauza magari yote ya kifahari (mashangingi) na serikali ianzishe utaratibu wa kukopesha magari ya kawaida kwa mawaziri na watendaji wote serikalini.

Bajeti hiyo pia imependekeza kupunguzwa kodi watozwayo wafanyakazi wote nchini na tatizo la umeme litangazwe kuwa janga la kitaifa.

Akisoma bajeti mbadala ya kambi ya upinzani jana bungeni, Waziri Kivuli wa Uchumi na Fedha, Zitto Kabwe, alipendekeza kufuta kodi zote za uanzishaji wa biashara ndogondogo ili kuchochea ujasiriamali nchini.

Akifafanua mpango wa ulipaji posho za wabunge na watumishi wote nchini, Zitto alisema kambi ya upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao (sitting allowances) uondoke katika utumishi wa umma.

“Ninaomba ieleweke kuwa hatupingi posho za kujikimu ambazo viongozi au maofisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi.

“Posho hizi zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa. Lakini posho za vikao zifutwe mara moja,” alisema Zitto.

Mbunge huyo ambaye kwa takriban wiki moja sasa amejikuta kwenye mzozo na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kuhusu posho za wabunge, alisema wabunge wanapaswa kuwa mfano wa kufyeka posho zao.

“Waheshimiwa wabunge, iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuwahoji na kuwawajibisha,” alisema Zitto na kushangiliwa na wabunge wa upinzani.

Huku akitibua nyongo za wabunge wa CCM, Zitto alisema mfumo wa posho za vikao ni rushwa ya kitaasisi wanayojipa watu wenye mamlaka.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema wakati kiongozi wa umma anapolipwa posho kwa kikao cha kufanya maamuzi yanayohusiana na majukumu yake ya kazi ambayo analipwa mshahara, polisi halipwi posho kwa kulinda, mwalimu halipwi posho kwa kuingia darasani wala muuguzi halipwi posho kwa kusafisha vidonda vya wagonjwa.

“Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kufanya marejeo ya mfumo wa posho na mfumo wa mishahara kwa watumishi wa umma. Suala hili ni lazima tulianze sasa na katika bajeti hii tunayoijadili.

“Lazima tuwaonyeshe Watanzania kuwa tunajali hali zao ili kurejesha imani ya umma kwa wanasiasa na viongozi wao,” alisema.

Zitto, alirejea hotuba ya bajeti ya Waziri Mkulo wakati akiahidi kupunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kudhibiti matumizi, lakini alisema bajeti ya serikali ya mwaka huu wa fedha imetenga sh trilioni 0.987, sawa na asilimia 13 % ya matumizi ya kawaida ya serikali na asilimia 6% ya bajeti yote kwa ajili ya kulipa posho.

“Kambi ya Upinzani inahoji, je, waziri atapunguza posho zipi na kwa kiasi gani wakati tayari ametenga kiasi cha sh trilioni 0.987 kwa ajili ya posho?” alihoji.

Dondoo za Bajeti Mbadala

Zitto aliahidi kuongeza mapato hadi kufikia sh trilioni 14.160 kutoka trilioni 13.525 za serikali.

“Tumeongeza mapato ya ndani hadi sh trilioni 8.68 kutoka sh trilioni 6.7 za serikali, tumeondoa kukopa mikopo ya kibiashara, hii inatokana na ukweli kwamba kufanya hivyo ni kuliongezea taifa gharama za kulipa madeni yenye riba kubwa na pia hili linafanya uchumi kuathirika, kwani serikali inakuwa ikishindana na sekta binafsi katika kuchukua mikopo kwenye taasisi za fedha, hivyo kuathiri uchumi,” alisema.

Zitto aliendelea kusema kuwa wameondoa posho mbalimbali ambazo ni sh trilioni 0.987 na kuzipeleka kwenye kuboresha mishahara ya watumishi wa umma na katika bajeti ya maendeleo.

Nyingine ni kupunguza matumizi ya kawaida ya serikali kutoka sh trilioni 8.6 na kuwa 7.9.

Alisema pia kuwa Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya umeme na kuchochea matumizi ya gesi majumbani.

“Pia tutakusanya mapato ya ndani kwa 22.84% ya Pato la Taifa ukilinganisha na serikali ambayo watakusanya 17%, tumepunguza misaada na mikopo kutoka nje na kuwa 27.54 % ya bajeti wakati ya serikali ni 29%.,” alisema.

Kwa mujibu wa Zitto, Kambi ya Upinzani imetoa vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaongeza sh trilioni 1.905.

Alitaja muhtasari wa vyanzo vipya vya mapato na kiasi kitakachoingizwa kuwa ni pamoja kodi ya misitu sh bilioni 100.

Chanzo kingine ni kurekebisha misamaha ya kodi (sh bilioni 658), mauzo ya hisa za serikali (sh bil. 550), kurekebisha kodi sekta ya madini (sh bil. 240), kuimarisha usimamizi wa mapato ya wanyamapori (sh bil. 81), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa kampuni za madini (sh bil. 59).

Kwa mujibu wa Zitto, chanzo kingine cha mapato kitatokana na usimamizi wa mapato katika utalii (sh bil. 68) na kuimarika kwa biashara na EAC (sh bil. 150). Vyanzo hivyo vyote vitaingiza sh bil. 1905.

Alisisitiza kuwa vyanzo hivyo ni vipya na ambavyo havikusanywi na serikali na kupanua wigo wa kodi.

Pia alipendekeza kurekebisha sheria za kuzuia ukwepaji wa kodi (anti tax avoidance measures) na kuboresha mfumo wa kodi.

Alisema Kambi ya Upinzani wamependekeza kurahisisha mfumo wa Kodi ya Mapato (Personal Income Tax) na kwamba sasa kila Mtanzania ajaze fomu za kodi (tax returns) kwa mujibu wa sheria hata kama hana kipato.

Alitoa mfano wa watu wenye nyumba za kupangisha mijini, alisema wanapata fedha nyingi na wengine hutoza kodi ya pango kwa kutumia dola za Marekani lakini hawalipi kodi ya mapato.

“Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili,” alisema.

Misamaha ya kodi

Kuhusu kiwango cha kodi, Zitto alisema misamaha ya kodi inayotolewa Tanzania ni kikubwa mno.

“Hii inaonekana wazi kwa kulinganisha kiwango cha misamaha ya kodi kinachotolewa Tanzania na kile kinachotolewa katika nchi za Uganda na Kenya.

Nchini Tanzania kati ya miaka ya 2005/06 na 2007/08 misamaha ya kodi ilikadiriwa kuwa wastani wa asilimia 3.9 ya Pato la Taifa. Mwaka 2008/09 misamaha ya kodi ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa na mwaka 2009/10 asilimia 2.3.

Ukilinganisha na Kenya na Uganda misamaha ilifikia asilimia 1 na 0.4 ya Pato la Taifa la kila nchi husika kwa mtiririko huo,” alisema.

Alisema kama Tanzania ingerekebisha viwango vya misamaha ya kodi ili kulingana na kiwango kilichofikiwa na Kenya, zaidi ya sh bilioni 600 zingeokolewa kwa mwaka 2007/08 peke yake.

Kwa mujibu wa Zitto, ukubwa wa kiwango cha misamaha inayotolewa nchini unaweza kuelezewa kwa kukilinganisha na malengo ya ukusanyaji wa mapato ya kodi ambayo Tanzania inashindwa kuyafikia.

Mfano katika mwaka 2008/09 na 2009/10, Zitto, alisema serikali haikutimiza lengo lake la mapato kwa wastani wa sh bilioni 453 kila mwaka.

Alisema katika kipindi hicho hicho, misamaha ya kodi iliyotolewa ilifikia wastani wa sh bilioni 724 kwa mwaka Juni 2011, msamaha wa kodi unakadiriwa kuwa sh bilioni 930.

Umeme janga la taifa

Katika hotuba hiyo ya Bajeti Mbadala, kambi ya upinzani imependekeza tatizo la umeme litangazwe kuwa janga la kitaifa.

Zitto alisema katika moja ya vipaumbele vya serikali mwaka huu Waziri Mkulo alitaja umeme.

Alisema Waziri Mkulo, alipendekeza kumaliza tatizo la umeme na kwamba ametenga sh bilioni 537 kwa ajili hiyo.

Hata hivyo alisema upembuzi uliofanywa na Kambi ya Upinzani kwenye vitabu vya bajeti vilivyotolewa na serikali, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa sh bilioni 402.4.

Alisema fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi ya kawaida sh bilioni 76.95 na kwa upande wa Bajeti ya Maendeleo zimetengwa sh bilioni 325.4.

Kwa mujibu wa Zitto, sh bilioni 325 zilizotengwa katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160 MW, 100 Dar es Salaam na 60 Mwanza.

Alisema hakuna mradi wowote mpya wa umeme unaoonekana katika bajeti hii.

“Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya mpango wa kwanza wa maendeleo wa miaka mitano, katika uzalishaji umeme ambapo kama taifa tumepanga kuzalisha megawati 1788 za ziada kutoka MW 1034 (installed capacity) zilizopo sasa, tunahitaji kuzalisha wastani wa MW 358 kila mwaka kwa miaka mitano.

Hivyo basi, ukiondoa mradi wa MW 160 ambao tayari umeanza na umetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu, tunahitaji mradi mwingine wa angalau MW 200 ndani ya mwaka huu wa fedha. Mradi ambao unaweza ukatekelezwa kwa haraka ni mradi wa Kiwira awamu ya kwanza MW 200,” alisema.

Alisema miradi iliyosalia ya Mchuchuma na Ngaka (makaa ya mawe), Mtwara - Somanga Fungu na Kinyerezi ( gesi asilia) na Ruhudji (maji), ielekezwe kwa taasisi zilizoainishwa kwa ajili ya utekelezaji na serikali kuingia makubaliano na taasisi hizo ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati.

“Mheshimiwa Spika, madhara ya ukosefu wa umeme kwenye uchumi wa taifa ni makubwa sana. Mamlaka ya Mapato Tanzania ilinukuliwa ikisema kuwa mgawo wa umeme uliotokea mwanzoni mwa mwaka huu unaweza kuikosesha mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 840.

Tumeona juhudi za Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la umeme lakini juhudi hizi hazionekani upande wa serikali na hasa Wizara ya Nishati na Madini.

“Mheshimiwa Spika, imefikia wakati sasa kutangaza kuwa umeme ni janga la taifa na kwamba Bunge lipitishe azimio la uzalishaji wa umeme kwa viwango vya mpango wa maendeleo na kuweka adhabu ya kumfukuza kazi waziri iwapo miradi hiyo haitakuwa imekamilika kila mwaka,” alisema Zitto.

Pamoja na kukosoa, Zitto alimpongeza Waziri Mkulo, kwa kusikiliza na kuyaingiza kwenye bajeti ya serikali baadhi ya mapendekezo yao.

“Ninachukua fursa hii kumpongeza waziri mwenzangu kwa kusikiliza maoni yetu kwenye baadhi ya mambo hayo na hivyo kuonyesha kwa umma moja ya faida ya mfumo wa vyama vingi.

“ Tunatarajia kuwa serikali itaendelea kusikiliza maoni yetu na kuyafanyia kazi. Changamoto hii na kwa uzito ule ule pia ipo kwetu sisi wa Kambi ya Upinzani kusikiliza pia maoni ya serikali.

“Ni kwa namna hii ndiyo tutajenga taifa la watu walio huru, lenye demokrasia, usawa na haki, na lenye kutoa fursa kwa wananchi wake,” alisema.

Akitangaza sura ya Bajeti Mbadala kwa mwaka huu wa fedha, Zitto alisema mapato ya ndani (sh trilioni 8.681), mapato ya halmashauri (sh trilioni 3.51), mikopo na misaada kutoka nje (sh trilioni 3.924), mikopo ya ndani (sh trilioni 1.204) jumla mapato yote ni sh trilioni 14,160.

Kwa upande wa matumizi, Zitto alisema matumizi ya kawaida ni sh trilioni 7.913 wakati matumizi ya maendeleo ni sh trilioni 6.247.

Zitto alimalizia kwa kusema: “Kila mtu akitimiza wajibu wake, tunaweza. Tukiacha kuwa taifa la walalamikaji, tunaweza. Tukiendeleza umoja wa kitaifa, mshikamano na kulinda haki za raia, tunaweza. Ninaamini, tunaweza!”

No comments: