TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, June 18, 2011

Familia ya Kawawa yangombea nyumba,

Mjane ataka aipangishe, watoto wamgomea

FAMILIA ya mwasiasa mkongwe nchini, marehemu Rashid Mfaume Kawawa, maarufu kama Simba wa Vita, imeingia kwenye mgogoro wa urithi wa nyumba ya kiongozi huyo, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, iliyopo Dodoma.

Mvutano wa nyumba hiyo iliyopo eneo la Kilimani Dodoma, sasa umeshika kasi na baadhi ya wanafamilia wamekusudia kwenda kumwona Rais Jakaya Kikwete ili awasaidie kuleta suluhu.

Wanafamilia hao wamesema ugomvi huo ni hatari na unamvunjia heshima baba yao aliyekuwa na anaheshimika na watu wengi nchini.
Mgogoro huo mezuka baada ya watoto wa Mzee Kawawa kubaini kwamba, mke mdogo wa baba yao ameazimia kubadili umiliki wa nyumba hiyo kwa maelezo kuwa kwa sasa ni mali yake.

Akizungumzia sakata hilo Mtoto wa marehemu Mzee Kawawa, Zainab Kawawa, alisema waliishi na baba yao katika nyumba hiyo kwa miaka kadhaa hivyo wanafamilia hawafurahishwi na mkakati anaotaka kuufanya mama yao mdogo Asina, kuhusu nyumba hiyo.

Zainab, ambaye ni mbunge wa viti maalumu (CCM), alifafanua kwamba lengo la familia ya Mzee Kawawa ni kuhakikisha nyumba hiyo haibadilishwi umiliki ili kuifanya iwe kumbukumbu ya baba yao.

Ilielezwa kuwa Mzee Kawawa aliuziwa nyumba hiyo mwaka 2007 na Serikali baada ya kuishi humo kwa miaka kadhaa wakati wa utumishi wake serikalini.
Alisema taarifa walizozipata ni kwamba mwaka huo, ulichukuliwa mkopo wa Sh350 milioni kutoka Benki ya CRDB, ambazo zilitolewa kwa awamu ukianza mkopo wa Sh74 milioni.

Zainabu alisema baada ya baba yao kufariki walichunguza kwa makini hati za mkopo huo na kubaini kwamba huo hauwezi kurejeshwa iwapo nyumba hiyo itabadilishwa umiliki, na mjane huyo kuwajibika kulipa mkopo huo.
Alisema hati hizo zinaonyesha kuwa kila mwaka benki hiyo ilikuwa inalipwa Sh8 milioni kila mwezi, lakini wanafamilia walisimamisha ulipaji huo wakitafuta uwezekano wa kulipa fedha zote kwa mkupuo.
Alisema benki hiyo tayari imefikia hatua ya kutaka kuipiga mnada nyumba hiyo ili irejeshe fedha zake kwa sababu ya mpangilio wa ulipaji kuzorota.
Zainab alifafanua kwamba kinachoishangaza familia hiyo ni namna Benki ya CRDB ilivyokubali kumpa mkopo baba yao wakati tayari alikuwa amestaafu.
Hata hivyo, Zainab alisema familia hiyo ipo tayari kulipa deni hilo, lakini sharti nyumba hiyo isibadili umiliki na iendelee kubaki kumbukumbu ya baba yao.

Alisema ana uhakika kwamba mjane huyo anaweza kujikuta katika wakati mgumu wa kulipa deni hilo la Sh350 milioni iwapo atabadili hati hiyo.
Alisema familia ya Mzee Kawawa ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kuipatia uhuru Tanganyika kutoka kwa wakoloni, haipo tayari kuvunjiwa heshima kwa deni hili kushindikana kulipwa na mali ya baba yao, kupigwa mnada.

Hata hivyo, mjane huyo alisema ana mpango wa kuipangisha nyumba hiyo na kuifanya mradi wa kuendeleza maisha yake kwa sababu kwa sasa ni mali yake.

Mjane huyo amejenga nyumba nyingine eneo karibu na nyumba hiyo, lakini familia hiyo imesema haina tatizo na uendelezaji huo ila wanachotaka ni nyumba waliyoishi na baba yao iendelea kuwa kumbukumbu yake.

Tayari Mkuu wa wilaya ya Dodoma, John Tupa, ameingilia kati ugomvi huo kwa kujaribu kuleta upatanishi.
Hata hivyo katika hali inayoashiria kuwa sakata hilo limezidi kupamba moto, Zainab alisema lengo lake kwa sasa ni kumwona Rais Jakaya Kikwete kuokoa mali za kiongozi huyo wa zamani wa Tanzania.

“Tunataka mama yetu mdogo atambue kwamba hatupiganii mali hizo za baba yetu kwa faida yetu bali ni kulinda heshima yake," alisema Zainab na kuendelea:
"Tunajua baba yetu wakati wote aliishi maisha ya kawaida na wala hakutumia muda wake kutafuta utajiri kwa mikopo ya thamani kubwa kiasi hicho."

No comments: